2015-06-13 14:02:00

Yaliyojiri katika mazungumzo kati ya Papa Francisko na Wakleri! Pasaka: Afrika


Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa jioni tarehe 12 Juni 2015 ameshiriki katika mafungo ya maisha ya kiroho yaliyoandaliwa na Chama cha Uhamsho wa Kikristo Kimataifa kwa kushirikiana na Chama cha Udugu wa Kikatoliki. Baba Mtakatifu ametumia muda mrefu kujibu maswali kadhaa yaliyoulizwa na wakleri wanaoshiriki katika mafungo haya kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu ameulizwa namna ya kutangaza kwa ufanisi mkubwa Habari Njema ya Wokovu, kweli na kanuni maadili; namna ya kukabiliana na changamoto za umaskini kati ya Watu wa Mungu; majadiliano ya kiekumene na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mungu akipenda, Mwezi Novemba 2015 atafanya hija ya kichungaji Barani Afrika kwa kutembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na baadaye Uganda. Baba Mtakatifu amegusia umuhimu wa waamini walei katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema katika ukweli na uwazi kwamba, mchakato wa Uinjilishaji ndani ya Kanisa kama alivyokazia Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI unajikita katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Haya ni maisha ambayo yanaambata Heri za Mlimani ambazo kimsingi ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Yesu. Watu wafundishwe kweli na kanuni maadili kwa njia ya mifano halisi ya maisha, kwani watu wamechoka kusikia maneno matupu, ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa!

Waamini wajitahidi kuwa kweli ni Wasamaria wema kwa watu wanaoteseka na kutaabika sehemu mbali mbali za dunia. Kamwe wasiwe ni wepesi wa kulipiza kisasi kwa wale wanaodhani kwamba, ni maadui zao. Mtakatifu Charles de Foucauld awe ni mfano bora wa kuigwa. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa kumwilisha Injili ya Kristo katika uhalisia wa maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Baba Mtakatifu anasema, ulimwengu mamboleo umesheheni magumu na changamoto mbali mbali za maisha zinazowavunja watu moyo na ari ya kutaka kuendelea kuishi. Watu wengi wanakabiliwa na umaskini, magonjwa na njaa. Kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu, mambo yote haya yanaweza kushuhghulikiwa kwa kuwajengea watu matumaini, amani na usalama. Kanisa halina budi kuwa karibu na maskini na wote waliovunjika moyo, ili kuwajengea tena matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Utu na heshima ya binadamu vipewe kipaumbele cha kwanza vinginevyo kutakuwa na misigano ya kitabaka, kikwazo kikuu katika ustawi na maendeleo ya wengi. Heri za Mlimani ni mafundisho yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha kama alivyofundisha Yesu Mwenyewe. Kanisa lijitahidi kuwa ni chombo cha huduma ya upendo na mshikamano na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, anaweza kuwasamehe Mapadre wake wanaoelemewa na ubinafsi wao, lakini si rahisi kwa waamini walei kusamehe na kusahau kwa urahisi. Kanisa halina budi kuwa maskini kwa ajili ya kuwahudumia maskini, ili waweze kujisikia kuwa kweli wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu. Kuna maskini wa hali na kipato kuna maskini pia wa maisha ya kiroho, wote hawa wanapaswa kuhudumiwa na Mama Kanisa kwa ukamilifu, changamoto ni kutubu na kumwongokea Mungu ili kuonjeshwa wema na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kama ilivyojionesha kwa Zakayo mtoza ushuru. Maskini ni amana na hazina kubwa ya Kanisa, inayopaswa kutumiwa kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Kuhusiana na majadiliano ya kiekumene, Baba Mtakatifu Francisko anasema katika historia ya Kanisa: Roma, Costantinopoli na Moscow ilikuwa ni miji mikuu ambayo hadi leo hii inaongozwa na wakuu wa Makanisa ya: Kikatoliki kwa kuwa na Papa; Kanisa la Kiorthodox linaongozwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza pamoja na Kanisa la Kiorthodox la Moscow linaongozwa na Patriaki Kirill.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwamba, amemkaribisha Patriaki Bartolomeo wa kwanza kuja mjini Vatican tarehe 18 Juni 2015 wakati wa uzinduzi wa Waraka wake wa kichungaji kuhusu mazingira unaojulikana kama “Laudato si”, wimbo wa viumbe wote ulioimbwa na Mtakatifu Francisko wa Assisi. Waraka huu utawasilishwa na wajumbe kutoka Kanisa Katoliki, Kanisa la Kiorthodox na mtu asiye amini. Hii inatokana na ukweli kwamba, Patriaki Bartolomeo wa kwanza amekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea kazi ya uumbaji.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ana matumaini makubwa na Kanisa la Kiorthodox la Moscow kuhusiana na dhana ya Sinodi na kwamba, kuna mahusiano mazuri ya kiekumene na viongozi mbali mbali wa Makanisa; majadiliano ambayo kwa sasa yanajielekeza zaidi katika kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kwa kukazia utakatifu wa maisha. Makanisa yameonesha utashi wa kutaka kuadhimisha Siku kuu ya Pasaka kwa Wakristo wote siku moja, lakini bado kuna Jumuiya za Kikristo zenye misimamo mikali ambazo zinapenda kuendelea kutunza Mapokeo yake kama kawaida.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, anatarajia kufanya hija ya kitume Barani Afrika mwezi Novemba 2015 kwa kutembelea Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati na baadaye, Uganda ili kusherehekea Jubilei ya miaka 50 ya Mashahidi wa Uganda. Lakini hali bado ni tete pengine anaweza kufanya hija mapema zaidi nchini Kenya. Kutokana na uhaba wa Mapadre, Makatekista Barani Afrika wanachukua nafasi ya kwanza, kumbe kuna haja kwa Kanisa Barani Afrika kuhakikisha kwamba, linajielekeza zaidi katika majiundo makini na endelevu kwa Makatekista.

Bara la Afrika bado linaendelea kusuasua kutokana na wajanja wachache wanaokwapua rasilimali na utajiri wa Afrika kwa mafao yao binafsi. Kuna haja ya kuanza mchakato wa kuwekeza zaidi Barani Afrika ili kusaidia mchakato wa maendeleo ambao utawawezesha wananchi kujipatia maendeleo yao wakiwa Barani Afrika na hivyo kuondokana na kishawishi cha kutaka kukimbilia Ulaya na Marekani ili kupata maisha bora zaidi.

Baba Mtakatifu ameipongeza Familia ya Mungu Barani Afrika kwa maadhimisho mazuri ya Ibada na Mafumbo ya Kanisa yanayogusa undani wa mtu: kiroho na kimwili. Vita, nyanyaso na madhulumu ya kidini ni mambo ambayo yanachafua mfungamano wa kidugu na kijamii. Misimamo mikali ya kidini ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika. Boko Haram imekuwa ni tishio la maisha na usalama wa wananchi wengi Kaskazini mwa Afrika.

Baba Mtakatifu anaendelea kulipongeza Kanisa Barani Afrika kwa huduma makini linayotoa katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii, changamoto na mwaliko wa kuendeleza majadiliano ya kitamaduni kwa ajili ya mafao ya wengi. Anawashukuru waamini walei ambao wameendelea kuwa vyombo vya huduma ya upendo katika majanga mbali mbali yanayowakumba wananchi Barani Afrika. Kwa miaka mingi, Ulaya imekuwa wakarimu kwa Afrika, lakini leo hii mambo mengi yamebadilika, Afrika imekuwa kama “kichwa cha mwendawazimu” kila mtu anajifunza namna ya kukwapua utajiri na rasilimali ya Afrika kwa mafao binafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, Kanisa Barani Asia ni ushuhuda makini wa waamini walei ambao wamewekeza katika maisha na utume wa Kanisa, kiasi kwamba linasonga mbele. Kazi ya katekesi inatekelezwa na waamini walei; wamissionari wanayo dhamana ya kuwaandaa watu kielimu, utume unaotekelezwa kwenye taasisi za elimu na vyuo vikuu vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa. Jambo la msingi anakaza kusema Baba Mtakatifu, ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kuamsha miito mitakatifu na maisha ya kiroho. Amani, utulivu na maridhiano ni mambo msingi katika kukoleza maendeleo ya watu. Misimamo mikali ya kidini ni hatari kabisa kwa ustawi na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha mchakato wa maswali na majibu kutoka kwa wakleri waliokuwa wanashiriki katika mafungo ya maisha ya kiroho kwa kusema kwamba, leo hii kuna waamini wengi wanaoendelea kumwaga damu yao Barani Afrika, damu ambayo itakuwa ni mbegu ya Ukristo kwa wakati wake. Korea ni nchi ya mashuhuda wa imani, kama ilivyo Japan na sehemu nyingine za Bara la Asia. Kwa hakika waamini walei wanaendelea kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.