2015-06-13 15:49:00

Ufalme wa Mungu hauna haraka, pole pole tu! Utazaa matunda kwa wakati wake!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa, tunaongozwa na vifungu vifuatavyo kutoka kwenye Maandiko Matakatifu:  Ezek. 17:22-24, 2. 2Kor. 5:6-10, 3. Mk. 4:26-34. Ufalme wa Mungu huja polepole na hukua na kuzaa matunda.

Ndugu mpendwa katika jumapili ya leo tunatafakarishwa na mifano miwili – mbegu inayoota yenyewe na mbegu ya haradali. Mifano hii yaonesha mwelekeo wa ukuaji wa ufalme wa Mungu. Au namna ufalme wa Mungu unavyokua.

Yesu anaposema ufalme utakua anamaanisha kuwa ufalme hata kama unahitaji ushirikiano wetu, kwanza ya yote ni neema na zawadi toka kwa Mungu. Siyo matunda ya nguvu za kibinadamu. Katika somo la kwanza, Nabii Ezekieli anaongea kuhusu ukombozi wa taifa la Israeli. Anaongea wakati taifa likiwa utumwani. Anawaimarisha. Anasema hata mti mkavu utastawi. Ukuaji wa ufalme ni kazi yake Mungu na mwanadamu hawezi kuzuia. Yule anayetambua mapenzi yake Mungu anaitwa kushiriki kikamilifu katika ukuaji huo.

Baba Mtakatifu Yohani wa XXIII akiwa amesongwa na kazi na uongozi mgumu wa Kanisa kiasi kwamba alikosa usingizi mara nyingi, usiku mmoja katika hali ya ndoto, aliambiwa na malaika wa Mungu asihangaike kiasi hicho. Aliambiwa akumbuke kuwa kanisa si mali yake. Alikumbushwa na huyo malaika kuwa Mungu ndiye kiongozi mkuu. Baada ya ndoto hiyo hali ya kukosa usingizi mara kwa mara ikapotea kabisa katika maisha yake.

Hata hivyo haina maana kuwa sisi hatuna cha kufanya katika ujenzi wa ufalme huo. Katika nafasi na tafakari ya dominika hii tunakumbushwa tena kazi ya uumbaji ambayo Mungu amemshirikisha mwanadamu. Nafasi yetu katika ujenzi wa huo ufalme iko wazi ila tunakumbushwa kuwa katika ushirika na Roho Mtakatifu. Yesu alipoita wafuasi aliwaalika kushiriki naye na hata baada ya safari yake ya hapa duniani anawakabidhi waeneze habari ya ufalme huo ulimwenguni kote. Siku ya kupaa kwake, ndiyo siku alipowakabidhi rasmi utume huo. Tukumbuke kuwa Mungu hufanya kazi pamoja nasi katika kuufanya ulimwengu huu mbingu ndogo.

Mfano wa mtoto mdogo wa darasa la tatu anayeingia katika ugomvi na watoto wenzake lakini wa darasa la sita. Akibaki katika msimamo wake, yule mdogo anachora mstari kwenye udongo na kusema kuwa kama yupo anayethubutu basi ana auruke ule mstari aingie upande wake. Kwa sababu ya kiburi cha ukubwa na kuona kudharauliwa, wale wakubwa wakavuka ili kuona huyu bwana mdogo atawafanya nini. Baada ya kuvuka, yule mdogo akawacheka sana na kuwaambia sasa mko upande wangu. Wakawa marafiki. Ugomvi ukaisha. Mungu anatuita tuingie upande wake. Kiburi chetu na hali yetu ya kibinadamu itapata maana ikiongozwa na Roho yake Mungu. Kwa namna hiyo, mbegu ya Mungu iliyosiwa ndani mwetu itapata kukua na kuzaa matunda.

Mifano hii ya mbegu katika jumapili hii ni juu ya ukuaji wa ufalme wa Mungu ambao ndiyo kiini cha fundisho la Kristo. Tukiyatimiza mapenzi yake Mungu, tayari tunashiriki katika ukuaji wa  ufalme wa Mungu.

Sifa za ufalme wa Mungu ni hizi: wongofu na toba, uanachama hai, yaani kuwa pamoja na Kristo na kujifunza daima toka kwake,  kuwa wafuasi na watumishi waaminifu, utumishi wa kimapendo ukiongozwa na pendo lake Mungu, ni kuishi sheria ya msingi inayojengwa na maisha mapya katika Roho. Ni ile sheria ya kuwa watoto wake Mungu na tano ni tabia au hali ya kuwa na maisha ya heri – Mt. 5:1-12.

Ili kushiriki katika ujenzi wa ufalme huu zipo njia nyingi na haadhi yake ni hizi: heshima kati yetu, mshikamano na maskini, uaminifu kwa Mungu na kati yetu.  Je, sifa hizi kama upendo, huruma, msamaha na upatanisho zipo kati yetu? Hizi ndizo mbegu hai. Hizi ndizo hali zinazotakiwa kuonekana na kukaa kati yetu. Hizi ndizo mbegu hai ambazo Yesu atualika leo kuwa nazo ili ufalme uweze kukua. Kama mfuasi wa leo wa Kristo unasaidiaje wengine kukua kiimani?

Kama mimi na wewe tunashiriki kiaminifu katika kueneza Imani hai ya kikristo basi tuwe na uhakika kuwa tunashiriki katika ujenzi wa ufalme huo. Hatuko mbali na ufalme wa Mungu. Katika somo la pili, mtume Paulo anaonesha wazi kilichowapata Waisraeli huko utumwani. Anawaalika wafuasi kutoka utumwani, katika dhambi na hali ya kifo na kuingia maisha mapya, maisha ya uzima. Tukiwa katika hali hii mpya inakuwa rahisi kushiriki kiaminifu katika ujenzi wa huo ufalme. Ile mbegu ya Imani iliyosiwa ndani yetu itakua na kuenea ulimwenguni kote.

Tumsifu Yesu Kristo. Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.