2015-06-13 11:55:00

Mapadre tokeni huko mlikojichimbia ili muwaonjeshe watu huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa jioni tarehe 12 Juni 2015 ameongoza Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya wakleri wanaoshiriki katika mafungo ya kimataifa yaliyoandaliwa na Chama cha Uhamasho wa Kikristo Kimataifa kwa kushirikiana na Chama cha Udugu wa Kikatoliki, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hapa mjini Roma.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amewataka wakleri kutafakari kwa kina upendo na tunza ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la kale, kwani tangu walipokuwa watoto wadogo aliwapenda, akawaokoa na kuwatoa utumwani Misri. Huu ni mwaliko wa kusikiliza na kujielekeza katika hija ya maisha ya kiroho kwa kuambata Roho Mtakatifu. Mwenyezi Mungu anapenda kuwaonesha mshikamano wa upendo unaojikita katika uhuru na wajibu wa kila mtu kutoa majibu sahihi kadiri alivyoguswa na upendo wa Mungu. Hii ni changamoto ya kila mkleri kuhakikisha kwamba, anaifahamu vyema historia ya maisha yake na jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu amemkirimia upendo usiokuwa na mipaka.

Mwenyezi Mungu ni mwema na kamwe hawezi kuwa ni adui, kwani anaambatana na waja wake wakati wa wasiwasi na mashaka, hata pale wanapokabiliwa na madhulumu, nyanyaso hata kifo kama ilivyotokea kwa mashuhuda 23 wa Kanisa la Kikoptiki waliouwawa kikatili nchini Libya, kwa sababu ya imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wema wa Mungu ni moto wa kuotea mbali unagusa na kuponya madonda na dhambi. Lakini Mungu hapendi kuwaona waja wake wakiwa wanaabudu miungu wengine wa uwongo, kwani Mungu wa kweli ni Mtakatifu na chemchemi ya upendo kama ule unaobubujika kutoka kwa Baba kwa ajili ya mtoto wake.

Baba Mtakatifu anawaalika wakleri kuwa na uchaji ili kuonja wema na huruma ya Mungu katika maisha yao, tayari kuwashirikisha wengine fadhila hizi, lakini kwa bahati mbaya anasema Baba Mtakatifu, wakleri wanajikuta wakiwa na shingo ngumu, wakatili na watu wanaowalaani wengine; hawa ni wachungaji wasiokuwa na huruma wala upendo wa Mungu; kamwe hawawezi kuthubutu kuwaacha kondoo 99 ili kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea, ili kumrejesha tena kundini kwa upole na ukarimu.

Baba Mtakatifu anawaambia wakleri kwamba, kwa bahati mbaya ni kundi la watu wanaoridhika kuona waamini wachache na wala hawajitaabishi kwenda kuwatafuta waliopotea na kumezwa na malimwengu. Waamini wanapokumbwa na upweke kwa kukosa dira na mwelekeo wa maisha, wanapaswa kuoneshwa njia inayowapeleka kwa Yesu Kristo mkombozi wa dunia, ili aweze kuwafariji.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka wakleri kwa namna ya pekee kuwa ni wachungaji wanaombata wema wa Mungu, tayari kuwasaidia hata wale wanaowaletea mateso na mahangaiko makubwa katika maisha na utume wao, kwani hiki ni kielelezo cha neema na huruma ya Mungu iliyomwilishwa kwa njia ya Yesu Kristo, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake. Yesu anaendelea kuwaalika wote wanaosumbuka na kuelemewa na mizigo waende kwake, ili aweze kuwapumzisha na kuwafariji, chemchemi ya upendo wa Mungu inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Itakumbukwa kwamba, Ijumaa tarehe 12 Juni 2015 Mama Kanisa ameadhimisha Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, sanjari na Siku ya kuombea Utakatifu wa Mapadre.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.