2015-06-13 14:47:00

Mahakama zitekeleze dhamana yake si tu kwa kuhukumu bali pia kwa kuelimisha


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe  13 Juni 2015 amekutana na kuzungumza na Baraza la  kuu la Majaji lililoteuliwa na kukabidhiwa majukumu mbali mbali hivi karibuni nchini Italia na kwamba, linayo dhamana nyeti ya kuhakikisha kwamba, linaweka uwiano na utulivu wanapotekeleza majukumu yao ya kimahakama.

Uhakimu ni dhamana nyeti kwani kuna mambo mengi yanayoingiliana hapa, mengine ni kwa ajili ya mafao ya watu binafsi pamoja na haki; mambo ambayo kimsingi yanahitaji majibu muafaka kadiri ya kesi zilizopo. Utandawazi nao kwa namna ya pekee unachangia mkanganyo kiasi cha kukosa dira na mwelekeo sahihi wa maisha kwa kukumbatia sheria ambazo ni kinyume cha taratibu, mapokeo na mfungamano wa kijamii, mambo ambayo yanapaswa kuheshimiwa.

Wakati mwingine, kumekuwepo na mwingiliano wa tamaduni za mataifa mengine ambayo yamepiga hatua kubwa kiuchumi, lakini ni dhaifu sana kimaadili. Katika mazingira kama haya anasema Baba Mtakatifu Francisko misingi ya kitamaduni  inapokuwa imetikiswa, kuna haja kwa viongozi wa Serikali na mahakama, kukazia tunu msingi za maisha ya kiutu kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani.

Kwa kuzingatia kanuni maadili, hapo kuna uwezekano wa kupata ufanisi katika mchakato wa kushughulikia matendo ya uvunjifu wa sheria katika masuala ya uchumi na fedha; rushwa na ufisadi; mambo ambayo yanaendelea kuathiri hata maendeleo makubwa ya kidemokrasia yaliyokwishafikiwa. Jitihada hizi zinapaswa kumwilishwa katika sekta ya elimu kwa kuwajengea uwezo vijana wa kizazi kipya kuhusiana na masuala ya kiutu na mifano bora ya maisha, ili kujibu kikamilifu matamanio ya moyo wa mwanadamu.

Kutokana na changamoto hii, kuna haja kwa taasisi kuhakikisha kwamba, zinajiwekea mikakati ya muda mrefu katika mchakato wa kudumisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kusaidia maridhiano kati ya watu, ili amani iweze kutawala mioyoni mwao. Huu ni utume unaopaswa kutekelezwa kwa namna ya pekee na viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia na kutekekeza sheria za nchi.

Ni kweli kwamba, Mahakimu wanatekeleza kazi yao pale sheria inapovunjwa, lakini kipaumbele cha kwanza kiwekwe katika utekelezaji wa mafao ya wengi, ili kwamba, wananchi waweze kujisikia kuwa kweli ni sehemu ya sheria. Kwa njia hii, Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watu watathamini sheria na kuona kwamba, wao ni sehemu ya sheria hiyo.

Majaji na mahakimu wanapaswa pia kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kudumishwa kwa kutambua utu na heshima ya binadamu, lakini mwelekeo wa sasa katika masuala ya kisheria ni tishio kwa utu na heshima ya binadamu. Haki inapaswa kumwangalia mtu mzima: kiroho na kimwili; mtu ambaye ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kuna Mahakimu ambao wamesimamia tunu hii msingi katika maisha ya mwanadamu kiasi hata cha kuyamimina maisha yao; kati yao ni Bwana Vittorio Bachelet aliyeuwawa kikatili yapata miaka thelathini na mitano iliyopita. Ushuhuda wa maisha yake kama binadamu, mwamini wa dini ya Kikristo na Mwanasheria, uendelee kuwahamasisha wanasheria katika utekelezaji wa haki kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.