2015-06-12 16:13:00

Toeni huduma makini ya maisha ya kiroho kwa wasafiri kwenye viwanja vya ndege


Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum kuanzia tarehe  10 hadi 13 Juni linafanya semina ya kumi na sita ya kimataifa kwa ajili ya wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege. Semina hii imeongozwa na Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko Injili ya Furaha, “Evangelii gaudium” kwa kujiuliza swali la msingi, Je, Waraka huu unaweza kuwasaidia kwa kiasi gani katika utekelezaji wa shughuli za kichungaji kwenye viwanja vya ndege?

Semina hii imekuwa ni fursa kwa wajumbe kutoka sehemu mbali mbali za dunia kuweza kukutana na kubadilishana mawazo na mang’amuzi yao, tayari kujiwekea mikakati na sera za kichungaji kwa siku za usoni. Waraka huu ni muhimu kwa viongozi wa Kanisa katika ushuhuda wa maisha yao, ili kuwasaidia watu kufungua nyoyo na maisha yao kwa Kristo. Hii ni huduma makini ya maisha ya kiroho inayotolewa kwa watu wote bila ubaguzi wa kidini, kitamaduni, lakini kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 12 Juni 2015 kwa wajumbe wa Semina yak umi na sita ya wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege. Anasema, viwanja vya ndege ni mahali ambapo kuna watu wengi wanaosafiri kwa malengo mbali mbali kama vile: kikazi, kitalii, lakini hata wakati mwingine kuna wakimbizi na wahamiaji; wazee na watoto; makundi ya watu ambayo yanahitaji msaada maalum. Kuna makundi ya wafanyakazi yanayotekeleza wajibu wake kila siku kwenye viwanja vya ndege, kila kundi lina mahitaji binafsi na ya kitaaluma.

Baba Mtakatifu anasema, katika msafara wa wasafiri kwenye viwanja vya ndege kuna makundi pia ya watu wasiokuwa na nyaraka za kusafiria; wengi wao ni wakimbizi na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, ambao wamewekwa mbaroni kwenye viwanja vya ndege kwa kipindi kifupi au kwa muda mrefu, hata wakati mwingine pasi na msaada wa maisha ya kiroho na kiutu.

Katika maeneo ya viwanja vya ndege, wakati mwingine kunatokea ajali na majanga; mambo ambayo yanasababisha mahangaiko makubwa kwa watu. Hata katika mazingira kama haya, wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege wanaalikwa kuwapatia watu faraja na kuwatia moyo, kwani hata katika viwanja vya ndege, Yesu mchungaji mwema anataka kutoa huduma kwa Kondoo wake kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu, ili kuwaonjesha waamini huruma ya Mungu na kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Uinjilishaji kwa nyakati hizi ni kuwainua watu kutoka kwenye kongwa linalowakandamiza mioyoni mwao na katika maisha yao, kwa kuwapatia faraja inayobubujika kutoka kwa Kristo, chemchemi ya faraja na furaha ya kweli katika maisha ya mwanadamu. Umefika wakati kwa waamini kugundua tena sura ya huruma na upendo wa Mungu, hususan wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege wanapaswa kutekeleza dhamana hii kwa kuzingatia: umoja na utofauti, kwani maeneo haya ni kama majiji yanayokusanya watu kutoka katika dini, makabila na lugha mbali mbali na wanaunda Jumuiya inayopaswa kuhudumiwa kwa unyofu pamoja na kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anayeunda umoja katika utofauti.

Baba Mtakatifu anawahamasisha wahudumu wa maisha ya kiroho kwenye viwanja vya ndege kuhakikisha kwamba, wanawasaidia wasafiri kuwa na hamu ya kutaka kusoma na kulitafakari Neno la Mungu; ili waweze wao pia kuwa ni  vyombo vya faraja kwa jirani zao pamoja na kujiachilia mikononi mwa huruma ya Mungu, bandari salama kwa wanyonge. Huruma ya Mungu iko kwa ajili ya wote na inaonesha utashi wa Mwenyezi Mungu wa kutaka kuwakomboa wote.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema viwanja vya ndege vinapaswa kuwa ni mahali pa upendo na majadiliano yanayopania kukuza na kudumisha udugu, amani na maridhiano. Anawatakia wote wanaoshiriki katika utume wa Kanisa la Kiulimwengu, wawe kweli ni vyombo madhubiti vya kutangaza Habari Njema ya Wokovu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.