2015-06-12 09:08:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 11 ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa


Ni siku nyingine tena tumejaliwa na Mwenyezi Mungu na hivi tunaalikwa kwa furaha kuingia katika uwanja wa upendo tukitafakari Neno lake. Ni Dominika ya kumi na moja ya mwaka B. Katika masomo yetu Mama Kanisa apenda tutambue kuwa Ufalme wa Mungu huja polepole na hukua na kuzaa matunda. Ujumbe huu tunaupata katika somo la Injili ambapo Mwinjili Marko anafananisha ufalme wa Mungu na mbegu ndogo ya haradali ambayo ikishapandwa hukua na kuzaa mti mkubwa na wa ajabu. Kwa hakika ndivyo ufalme wa Mungu unavyokua mioyoni na maishani mwetu na hasa lengo likiwa ni kubadirisha maisha yetu toka maisha ya zamani na kuelekea maisha mapya.

Katika Somo la kwanza Nabii Ezekieli anaagua juu ya ukombozi wa taifa la Israeli toka utumwani Babeli. Anaagua juu ya uwezo wa Mungu wa kuweza kuleta mabadiliko katika maisha ya watu. Anatoa mifano kadhaa ambayo yaonesha uwezo wa ajabu wa Mungu akisema, Mungu tastawisha mti mkavu na kukausha mti mbichi, atashusha chini mti mrefu na kuuinua juu mti mfupi! Kwa hakika uaguzi huu unakuja kwa sababu Waisraeli wako katika taabu, wamekata tamaa na kupoteza imani katika Mungu na hivi Nabii anawaimarisha kwa neno la matumaini na hasa akionesha kwamba Mungu hawezi kumwacha mteule wake, na pia ni mwenye nguvu. Nabii anatumia mfano wa tawi kama kielelezo cha taifa la Israeli, yakwamba, Mungu atatwaa tawi hili toka katika mazingira ya ukame na jangwa ndiyo utumwa na kulipandikiza juu ya mlima ili lionekane mbele ya mataifa na kuwa kielezo cha upendo wake kwa mataifa yote.

Kwa hakika Yesu Mwana wa Mungu anapozaliwa katika ukoo wa Daudi miaka mingi baadaye ni ukamilisho wa unabii wa Ezekieli na ufalme wa Mungu unakamilika katika yeye. Mwaliko kwetu hivi leo, ni uleule ambao Nabii aliwapa wana wa Israeli wakati ule. Wakati wetu zipo shida nyingi zinazoonesha kuwa katika utumwa, nahivi zaweza kutufanya kukata tamaa na kusahau kuwa Mungu ni mwenye nguvu na ni upendo mkamilifu. Shida zilizopo siku hizi twaweza kuziangalia kwa ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukosefu wa uadilifu katika maisha ya kila siku, hali ngumu ya uchumi kiasi kwamba tunakosa mahitaji yetu muhimu, shida za hali ya hewa kwa ujumla, na zaidi sana mkanganyo unaotokana na kile kinachoitwa upako na nguvu za kutoa pepo na kutenda maajabu machoni pa watu! Haya yote ni matatizo ambayo yadai zaidi kumtegemea Mungu yaani kuwa na imani thabiti na hivi polepole kukabiliana nayo.

Katika Somo la Pili, Mtume Paulo anaonesha hali ileile iliyowapata Waisraeli huko Babeli. Kwa sababu ya madhulumu mbalimbali anajiona yuko utumwani nje ya nchi yake, na hivi anatamani kurudi nyumbani. Anaweka mbele yetu tafakari nzito ya kuwa nyumbani si hapa tunapoishi kwa mwili bali nyumbani hasa ni kukaa na Baba mbinguni. Ni kutoka katika maisha ya kifo na kuingia maisha ya uzima, ni kutoka maisha ya dhambi na kuingia maisha ya neema za Mungu. Kumbe, ni kuyatakatifuza malimwengu ambapo mwisho wake ni kurithi uzima wa milele mbinguni.

Katika Injili ambapo ndipo kiini cha ujumbe wa leo kimelala, tunapata kuona alama mbalimbali. Alama ya mbegu ni Neno la Mungu ambalo likishapandwa hukua polepole bila kumtegemea aliyelipanda yaani mhubiri, kwa maana lenyewe ni nguvu inayojitegemea, ni Kristo mwenyewe. (Yn. 1:1-). Mbegu hii lazima ipandwe katika udongo, kumbe, inahitajika kazi ya kimisionari ya kueneza na kupanda Neno la Mungu katika mataifa na katika mioyo ya watu. Hata hivyo wahubiri watambue kuwa matunda ya Neno hayaji kwa nguvu bali kwa utaratibu na upole.

Ndiyo kusema wanapohubiri wasikate tamaa wanapoona matunda hayatokei mapema. Angalia duniani leo kuna vita, vurugu na machafuko kana kwamba Mungu na Neno lake hawapo! Kwa hakika wapo, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kama mbegu ya haradali na hivi uingia katika mioyo ya watu kwa upole na unyenyekevu na watu watakiwa polopole kuukuza kwa matendo ya huruma na majitoleo yao ya kila siku na matokeo ni makubwa kuliko ile mbegu iliyopandwa mwanzoni. Kupokea imani huanza na mafundisho yaani katekesi na humalizika katika hatua ya kwanza na ubatizo. Baada ya ubatizo mmoja hupokea majukumu mbalimbali ya kitume, akipokea pia sakramenti nyingine katika safari hiyo na hualikwa kuvumilia na kushika safari mpaka mwisho wa nyakati. Safari hii haijulikani huisha lini na haina haraka. Kwa kielelezo hiki mmoja aweza kuelewa jinsi ufalme wa Mungu unavyokua na kuzaa matunda.

Mpendwa, ninakutakia matumaini daima na hasa wakati wa taabu ambapo kuna kishawishi kikuu cha kupoteza imani na tumaini kwa Mungu. Tukutane tena siku nyingine kama hii tukiwa bado katika tumaini la Bwana.Tumsifu Yesu Kristo. 

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd. Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.