2015-06-12 16:29:00

SECAM na ushuhuda wa Injili ya Familia Barani Afrika! Utakatifu na ukuu wa ndoa


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, hivi karibuni limefanya mkutano wake mjini Accra, Ghana, ili kuangalia mchango ambao Kanisa Barani Afrika linaweza kushirikisha katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia kama sehemu ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba 2015. Sinodi hii inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa Familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo”.

Mkutano huu umefunguliwa kwa hotuba na tafakari ya kina iliyotolewa na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, kwa kuwataka wajumbe kuzungumza katika ukweli na uwazi; kwa kushikamana katika ushuhuda na upendo kwa Kristo na Kanisa lake. Amewataka viongozi wa Kanisa Barani Afrika kutambua kwamba wanayo dhamana kubwa na nyeti ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia wema na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, ambayo kwa sasa inakumbana na kinzani nyingi.

Viongozi wa Kanisa kamwe wasione aibu kukazia mafundisho ya Kanisa kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, wanapaswa kusimamia mafundisho haya pale yanapokabiliwa na kinzani kutoka na sera tenge zinazohatarisha ustawi na maendeleo ya binadamu kadiri ya mpango wa Mungu. Kuna sheria na matamko mbali mbali ambayo yanaendelea kuhatarisha utakatifu wa maisha ya ndoa na familia. Ukweli na uwazi, ziwe ni silaha makini katika kuanika mambo yote yanayosigana na ukweli kuhusu maisha ya ndoa na familia.

Kwa upande wake, Askofu Joseph Osei-Bonsu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ghana anakaza kusema, ndoa kadiri ya mpango wa Mungu inaundwa kati ya bwana na bibi wanaokubaliana na kushibana katika upendo. Kanisa Barani Afrika lisikubali kishawishi kinacholetwa na vyombo vya mawasiliano ya kijamii kutaka kuvuruga kanuni maadili katika maisha ya ndoa na familia kwa kutaka kupandikiza ndoa za watu wa jinsia moja, mambo ambayo kwa sasa Ulaya na Marekani yanaanza kuwa “eti ni fashion” na kielelezo cha haki msingi za binadamu. Hapa watu wanasahau kanuni maadili na utu wema.

Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema Barani Afrika wanapaswa kuishi na kujisikia kuwa kweli ni Familia ya Mungu inayowajibika, changamoto na mwaliko wa kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kirohio na kimwili; ili hatimaye, familia zenyewe ziweze kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji kwa kujikita katika ushuhuda unaopania kuyatakatifuza malimwengu.

Askofu mkuu Gabrieli Mbilingi, Rais wa SECAM analitaka Kanisa Barani Afrika kuhakikisha kwamba, linajielekeza zaidi katika mchakato wa maendeleo endelevu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Wakristo wawe kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kkristo, kiutu na kimaadili. Bara la Afrika wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu Familia, litazungumza kwa sauti moja, ili kuwakilisha matamanio ya Kanisa Barani Afrika katika mchakato wa Utangazaji wa Injili ya Familia. Kanisa litaonesha: matatizo, changamoto na fursa zilizopo Barani Afrika katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia.

Askofu mkuu Mbilingi anakiri kwamba, leo hii familia nyingi Barani Afrika zinakabiliwa na majanga mengi yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kuna biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo, kazi za suluba kwa watoto wadogo, utalii wa ngono na picha chafu; mwaliko kwa wanasiasa na watunga sera kuhakikisha kwamba, wanatumia madaraka na mamlaka waliyokabidhiwa na jamii  ili kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.