2015-06-12 08:45:00

Ndugu wananchi naomba kutangaza "NIA", uwezo na sababu ninazo!


Katika kipindi cha kampeni za uchaguzi wa viongozi wa nchi, wagombea wengi wanajinadisha kwa mbwembwe, wakitoa ahadi nzuri kwa njia ya kauli mbiu na sera zinazojaribu kujibu kero za wananchi. Baada ya uchaguzi wananchi wanasubiri kwa hamu utekelezaji wake. Wanapokosa kuona matunda yaliyoahidiwa, wanananchi wanajiona wamehadaiwa na wanajiuliza: “Kulikoni mbwembwe zile zote?” Swali kama hilo wanaweza pia kujiuliza wazazi na walezi wengi kuhusu tabia za watoto wao. “Kwa nini watoto hawakui kadiri ya maadili ya malezi tuliyoyawekeza kwao?”

Kadhalika tunaweza kusema juu ya Injili ya Yesu. Ilikuwa imehubiriwa sana na Yesu mwenyewe na mitume wake, lakini hayakuonekana mabadiliko ya pekee. Jumuia ya kwanza ya wakristu ikawa inajihoji mstakabali wa maisha yao: Je, katiba mpya iliyonadishwa na Yesu inazaa au haizai matunda? Hata siku hizi, mtu anaweza kujiuliza: Kwa muda mrefu nimesikiliza Injili lakini kwa nini mambo hayabadiliki? Je, kuenea kwa Injili hiyo kunamtegemea nani? Au labda kuna njia mbadala wa kuifanya ikue haraka haraka, mathalani kwa kutumia mitindo ya kampeni za kisiasa, au hata kwa ukali, au kwa njia za uonevu na za kuua ili tu mradi ienee?

Leo Yesu anatoa majibu kwa maswali ya mtindo huo yanayowakera wafuasi wake juu ya hatima ya Katiba mpya ya utawala wa Mungu aliyoinadisha mwenyewe ulimwenguni. Majibu hayo yanaweza pia kutatua kero za mtindo huo katika uwanja wa siasa, dini au hata familia.  Yesu anajibu kwa kutumia mifano miwili iliyosukwa vizuri kutoka hali halisi ya maisha. Kabla ya kutoa jibu, anaanza kuujulisha Mswada wa Katiba yake mpya anaposema: “Hivi ndivyo ulivyo ufalme wa Mungu.” Hapa ni kama ilani ya kukitambulisha Chama kipya.

Ukweli ni kwamba Chama hicho ndicho pekee kinachotawala – kimeshika hatamu – mbinguni yaani binadamu atake asitake atakumbana nacho tu. Chama hicho kilishakuwepo hapa duniani na wanachama wake wa asili (waasisi) walikuwa ni binadamu. Lakini chama hicho kikaja kuchakachuliwa na shetani pamoja na wafuasi wake. Sasa yabidi kujiandikisha na kuanza kukiishi tena na baadaye kuendelea nacho huko mbinguni kiurahisi.

Chama hicho ni cha Ufalme wa Mungu unaoanza hapa duniani kama mtu anayemwaga mbegu ardhini, yaani kinatangazwa katika ulimwengu wa kawaida wa watu na wa wakati wake. Anayemwaga mbegu ya ufalme huo ni Mungu mwenyewe na mbegu yenyewe ni Yesu, na baada ya Yesu wanafuata wanafunzi wake, kisha tunafuata sisi sote. Kwa hiyo mbegu ni sisi sote tulioumbwa kwa mfano na sura ya Mungu, tumejaa neema ya Kristo ambayo ni Katiba ya Mungu. Kupanda huko kunamtegemea aliye na mbegu endapo anaamini kwamba zinaweza kuota. Yesu anapoongea juu ya kuota mbegu anafikiria ardhi ya nchi yake yenye mawe mengi, mvua haba, jua kali, kuna wanyama na ndege walio hatari kwa mazao.

Kwa hiyo yabidi kuiaminia mbegu na ardhi. Kutoiamini mbegu au kumwaga mbegu mbovu mapato yake unapata matunda mabovu na unaishia kulaumu ardhi na hali ya hewa. “Mbaazi ikikosa maua husingizia jua.” Mathalani, mwanasiasa anayemwaga sera mbovu kwa wananchi kwa mbwembwe na makelele kibao, matokeo yake yanaeleweka. Kadhalika mchungaji anayejitolea kufanya shughuli nyingi za kuchosha zisizohusiana na Injili matokeo yake yanaeleweka.

Kisha baada ya kumwaga mbegu ardhini Yesu anaendelea kusema: “mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara aupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika.” Mpandaji akishamwaga mbegu hajui kinachoendelea kufanyika ardhini au ndani ya mioyo ya watu. Hivi kazi ya mpandaji ni kupanda na kuvuna. Kazi inayoendelea ardhini ni ya Mungu. Anachotakiwa kufanya mpandaji ni kuwa na saburi na imani na kungojea kwenda kuvuna. Kwa hiyo, tusimwingilie Mungu kazi yake ya kuotesha mbegu ndani ya ardhi.

Mungu anamwaga mbegu ya neema ndani mwetu ili ichipue. Kazi ya ardhi ni kupokea na kukomaza mbegu iliyopandwa. Watu wote ni kama ardhi ambayo Mungu anamwaga mbegu. Ndani mwao Mungu anakaa na kukomaa. Mambo ya Mungu, na sera au neema zake zinamea na zinakua kwa nguvu ya ajabu bila mbwembwe na kelele.

Kadhalika kwa wachungaji na wazazi, kama wamepanda mbegu nzuri, basi wawe na saburi, kwani hawajui kinachotokea moyoni mwa mtu. Sababu za kukosekana matokeo au matunda ya malezi waliyowekeza kwa watoto wao zaweza kuwa nyingi kwa vile watoto nao siyo maamuna. Watoto nao ni watafiti na wapembuzi wa mambo. Wanawajua watu wanaoishi na kuamini mambo wanayoyafundisha na wanawajua watu wasioishi wanayofundisha. Kama wazazi na walezi ni ovyo au wamefilisika kiimani, kimaadili na utu wema hao watapanda mbegu ovyo na matokeo yake ni mabovu. Kama umepanda mbegu nzuri hapo hata kama wewe upo macho au umelala, iwe usiku au mchana, mbegu inachipua na kukua, kwa vile nguvu iko katika mbegu na siyo kwa mpandaji.

Mfano wa pili, Yesu anaulinganisha Ufalme wa Mungu na mbegu ya Haradali iliyo ndogo sana. Mlinganisho huo ni kinyume kabisa na fikra za Wayahudi. Picha iliyokuwa inatumika na wayahudi kuhusu Mungu na ufalme wake ilikuwa ni kuulinganisha na mti mkubwa wa mwerezi ya Lebanoni (Ezekiele 31:3 na Ezekieli 17:22-23). Kumbe kinyume chake Yesu analinganisha Utawala wa Mungu na mbegu ndogo sana, jinsi inavyoweza kukua polepole na kuenea. Hapa Yesu anataka kulifuata kabisa wazo hili la kutisha la mti wa mwerezi. Hapa mierezi inaweza kulinganishwa pia na sera nzito lakini sera hewa zisizotekelezeka zinazoahidiwa na viongozi wa nchi.

Kisha Yesu anaonesha kwamba mharadali huo utatoa kivuli kizuri na katika matawi yake ndege watajenga viota. Ufalme wa Mungu unaonekana kuwa mdogo sana na wa kudharaulika, lakini ndiyo polepole utabadilisha hali ya nchi na hali ya mambo. Mbegu hii ina nguvu ya kimungu na inatoa mapato ya pekee, siyo kadiri ya vigezo  vya fikra za walimwengu. Kuhusu ndege wa angani kujenga vioto vyake. Katika Biblia ndege wanatokea pale wanapomkorofisha Abrahamu anapotolea sadaka. Ndege hao wanawakilisha wapagani, watu dhaifu, hao wote watapata makao katika matawi ya mti huu wa mharadali.

Mbegu hiyo ndogo ya mharadali iko ndani yetu na ambayo tunadhani haiwezi kuokoa ulimwengu. Lakini Yesu anasema, itakapoota, itakuwa mmea ambao ndege wa angani watakuja na kujenga viota. Chini ya kivuli chake wahitaji wengi watajisikia raha na kutulia. Katika mfano huu unaona wazi jinsi Mungu anavyoweza kutumia njia nyonge na za kimaskini sana kueneza ufalme wake. Anawapenda watu wanyonge na wanyenyekevu kama alivyosali Mama Maria: “Ameangalia unyenyekevu wa mtumishi wake” (Lk 1:48), na kwamba ufalme huo unakua kwa nguvu ya maajabu ya siri ya mambo madogomadogo, ya kutakiana mema, ya ukweli, na ya haki.

Mifano ya leo inatutaka tujue kwamba kila mmoja wetu anayo nguvu ya Mungu ndani mwake, nguvu ya upendo, haki na amani nk.Kwa hiyo yatubidi kumwiga Kristo kuiishi na kuimwaga kwa uhodari na kwa uaminifu wote ulimwenguni. Mbegu hiyo ni ndogo sana na inakua polepole moyoni mwetu. Ikikua itakuwa ukombozi kwa wote. Kinyume chake ukipanda mbegu mbovu usishangae na kusikitika unapoona mavuno mabovu. Tuaminie nguvu ya vitu vizuri. Mungu anafanya kazi ulimwengu kimyakimya na taratibu na kwa kutumia mambo madogo na manyonge.

Na Padre Alcuin Nyirenda. OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.