2015-06-12 16:44:00

Msiwanyanyase watoto kwa kuwafanyisha kazi za suluba!


Jumuiya ya Kimataifa tarehe 12 Juni, kila mwaka inaadhimisha Siku ya kupambana na kazi za suluba kwa watoto wadogo duniani. Shirika la kuhudumia watoto wadogo la Umoja wa Mataifa, UNICEF linabainisha kwamba,  kuna zaidi ya watoto millioni 150, wenye umri kati ya miaka 5 hadi 14 wanaofanyishwa kazi za suluba sehemu mbali mbali za dunia. Watoto wadogo wanaofanyishwa kazi hizi, wengi wao wamo kwenye hatari ya kudumaa na hivyo kuathirika katika makuzi yao anasema Bwana Giacomo Guerrera, Rais wa UNICEF nchini Italia.

Takwimu zinaonesha kwamba, Eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, Barani Afrika linawafanyisha watoto kazi za suluba kwa asilimia 25%. Hawa ni watoto wenye umri kati ya miaka 4 hadi 14. Bara la Asia lina idadi ya asilimia 12%, Bara la Ulaya ya Kati, watoto wanaofanyishwa kazi za suluba ni asilimia 5%. Kuna watoto ambao wamelazimika kuacha kuendelea na masomo kutokana na umaskini wa familia zao na matokeo yake wanajikuta wakifanyishwa kazi za suluba, wengi wa watoto wasichana wanafanyishwa kazi za majumbani.

UNICEF inasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujikita katika kampeni dhidi ya nyanyaso na dhuluma za watoto wanaofanyishwa kazi za suluba, kwa kuwahamasisha watu kutambua madhara ya kazi hizi katika malezi na makuzi ya watoto; kuzuia kazi hizi pamoja na kuanzisha mchakato utakaowasaidia watoto walioacha shule kuanza tena masomo kwa kutambua kwamba, elimu ndiye mkombozi wa wanyonge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.