2015-06-11 15:07:00

Waondoleeni waamini ubaridi wa imani na kutopea katika mawazo mepesi mepesi


Hija za kitume zinazotekelezwa na Maaskofu mahalia walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican zinasaidia kuimaarisha kifungu cha upendo na udugu katika maisha na utume wa Maaskofu waliopewa dhamana ya kuhudumia Familia ya Mungu. Maaskofu wameteuliwa kwa ajili ya huduma za kichungaji ndani ya jamii ili kudumisha utu na heshima ya binadamu, uhuru wa kweli pamoja na kupambana dhidi ya ubaridi wa imani, kutopea katika mawazo mepesi mepesi pamoja na kumezwa na malimwengu.

Maaskofu wanahamasishwa kuwa na ujasiri, imani na matumaini wanapotekeleza dhamana na wajibu wao katika mchakato wa kutangaza Injili ya Kristo, Neno la uzima wa milele kwa watu wa kila nyakati na tamaduni. Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Maaskofu kutoka Lithuania na Estonia wanaoendelea na hija yao ya kitume hapa mjini Vatican. Anasema katika dhamana ya Uinjilishaji, Maaskofu watambue kwamba, wasaidizi wao wa karibu ni mapadre, hata kama ni wachache, wanapaswa kuwaonesha heshima, utii na ukarimu.

Kwa pamoja Wakleri wajielekeze katika mikakati ya shughuli za kichungaji ili kukuza na kudumisha miito, kwa kutambua kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache. Hii ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na Familia yote ya Mungu, ili kweli vijana waweze kuitikia wito wa kumtumikia Mungu na jirani zao.  

Mapadre wanapaswa kupewa majiundo makini na endelevu katika masuala ya Kitaalimungu na Kikanisa, ili waweze kupata ukomavu wa kiutu unaofumbatwa katika tasaufi ya ukweli na uwazi katika ulimwengu mamboleo. Waamini wasaidiwe katika malezi na makuzi yao katika maisha ya kiroho na kimwili, kwa kushirikiana kwa namna ya pekee na watawa mbali mbali, ambao Kanisa kwa mwaka huu linaadhimisha Mwaka wa Watawa Duniani.

Watawa ni wahudumu wa Injili wanaotoa huduma kubwa kwa ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu katika nchi husika sanjari na kushirikisha karama za Mashirika yao kama kielelezo cha ushuhuda wa Mashauri ya Kiinjili kwa wafuasi wa Kristo. Watawa wanapaswa kusaidiwa: kiroho na kimwili; kwa kushirikiana katika maadhimisho mbali mbali, ili kufahamiana na kuimarishana katika hija ya maisha na wito wa Kikristo kwa kumzunguka Askofu mahalia, ili kuonesha ile dhana ya kuwa ni sehemu ya Kanisa mahalia linalofurahia maisha na kuwajibika katika ujenzi wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kuwashirikisha kikamilifu waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwani wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao. Wasaidiwe na kuimarishwa katika maisha na utume wao kuanzia kwenye familia na vyama vya kitume pamoja na kuwaelimisha kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Waamini walei wajisikie kuwa kweli ni sehemu ya Kanisa pamoja na kuendeleza majadiliano ya kiekumene na waamini wa Makanisa na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, ili kujenga na kudumisha haki jamii ambayo wakati mwingine inatikiswa kutokana na tofauti za kikabila na lugha za watu.

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwani hapa ni mahali ambapo watu wanajifunza kuishi kwa upendo na mshikamano na wazazi kupata nafasi ya kurithisha imani kwa watoto wao. Utakatififu na heshima ya ndoa vinapaswa kukuzwa na kudumishwa badala ya kukimbilia katika mpasuko na kinzani za ndoa ziinazoendelea kuvunjika kila kukicha. Wanandoa watarajiwa waandaliwe vyema ili kukabiliana na wito pamoja na dhamana ya maisha yao ya ndoa.

Kanisa liendelee kuwasaidia wale wanaoishi katika mazingira magumu, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu na kamwe wasijisikie kutengwa na Kanisa. Viongozi wa Kanisa wawasaidie wanandoa katika safari ya imani na malezi ya Kikristo kwa watoto wao.

Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zimetikisa nchi zao kiasi kwamba, leo hii kuna idadi kubwa ya watu wanaohama na kukimbilia nje ya nchi kwa ajili ya kutafura fursa za ajira, matokeo  ni familia nyingi kuwa tenge, hali inayogumisha malezi na ustawi wa watoto ndani ya familia. Hizi ni familia ambazo zinapaswa kuonjeshwa upendo wa kichungaji, kwa kuungana na Jumuiya za Kikristo. Baba Mtakatifu anawashukuru Maaskofu kwa uwepo na faraja yao ya kidugu katika upendo na ushuhuda katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.