2015-06-11 16:00:00

Moto wa Injili, ari na mwamko wa kimissionari umewashwa mjini Roma!


Kama ilivyokuwa wakati wa Pentekoste, Bikira Maria bado anaendelea kuchukua nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliliwezesha Kanisa kutoka kifua mbele, tayari kujikita katika mchakato wa maisha ya kimissionari, ili kuwatangazia Watu wa Mataifa, Habari Njema ya Wokovu. Hapa waamini, lakini kwa namna ya pekee, Wakleri wanaalikwa kuamini katika nguvu ya mageuzi yanayojikita katika wema na uzuri, ili kujifunza kutoka kwa Bikira Maria, jinsi ya kulitafakari Fumbo la uwepo wa Mungu ulimwenguni.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa Jumatano tarehe 10 Juni 2015 na Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la walei katika ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa mafungo ya kiroho kimataifa, yaliyoandaliwa na Chama cha Kitume cha Uhamsho wa Kikristo Kimataifa kwa kushirikiana na Chama cha Udugu wa Kikatoliki. Mafungo haya yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano hapa mjini Roma, lengo kuu ni kuchuchumilia utakatifu wa maisha.

Ni matumaini ya Kardinali Stanislaw Rylko kwamba, siku hizi za mafungo ya kiroho kwa Wakleri zitaweza kuamsha ari na mwamko mpya wa maisha na utume wa kimissionari kutoka katika undani wa maisha yao, tayari kutoka kifua mbele kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili ya Furaha. Wakleri wasiwe tena na kishawishi cha kutaka kujifungia ndani mwao na kuanza kujitafuta, bali wawe tayari kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kama ilivyokuwa siku ile waliposikia na kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao ya Kipadre.

Kardinali Rylko anawataka Wakleri kukita maisha yao katika mchakato wa maisha na shughuli za kimissionari kwa kukazia furaha na matumaini, kwani mambo haya kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko ni vinasaba vya maisha ya Wakristo! Ukimwona Mkristo amenuna, tambua kwamba, hapo kuna jambo ambalo haliendi sawa sawa. Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa matumaini na furaha, hata pale wakati mwingine, wanapolazimika kutokwa na machozi ya damu kutokana na shida mbali mbali zinazomwandama mwanadamu.

Kwa namna ya pekee kabisa, Wakleri wanahamasishwa kurudi tena darasani kwenye shule ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, ili waweze kujifunza mbinu mpya za Uinjilishaji, kwa kuiga mfano wa maisha yake, katika unyenyekevu na upole, ili azma ya uinjilishaji mpya iweze kuambata furaha ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake.

Mara baada ya Misa takatifu, Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya kipapa amekazia umuhimu wa mafungo ya maisha ya kiroho kwa Wakleri kama sehemu ya mchakato unaolenga kupyaisha zawadi, maisha na utume wao kama Wakleri. Wajisikie kuchoka baada ya kuchakarika kuwahudumia Watu wa Mungu katika maisha yao ya kiroho na kimwili, ili hatimaye, waweze kupata mapumziko matakatifu. Vinginevyo, anasema Padre Cantalamessa kuna hatari kwa Wakleri kukata tamaa na hatimaye, kumezwa na malimwengu.

Padre Cantalamessa anabainisha kwamba, katika mafungo haya, Wakleri wajitahidi kuamsha ndani mwao ari na moyo wa kimissionari, kwa kuliwezasha Kanisa kuwa na malango wazi, tayari kuwaendea watu ili kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hili ni Kanisa maskini kwa ajili ya kutoa huduma kwa maskini; likionesha uwezo na jeuri ya kuandamana na watu katika shida na raha kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.