2015-06-11 14:55:00

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujifunga kibwebwe kupambana na baa la njaa!


Umuhimu wa kutambua chakula na haki ya kupata chakula bora kwa wote; watu wabadilishe mfumo na mtindo wa maisha, ili kuwa na matumizi bora ya chakula; umuhimu wa mshikamano wa kimataifa katika kupambana na baa la nja na utapiamlo wa kutisha pamoja na uhakika wa usalama wa chakula duniani, ni kati ya mambo makuu ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyatoa kwenye hotuba yake kwa wajumbe wa  mkutano mkuu wa thelathini na tisa wa Shirika cha Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, Alhamisi, tarehe 11 Juni 2015.

Baba Mtakatifu Francisko bado anayo kumbukumbu hai ya mkutano wa pili wa lishe kimataifa uliofanyika mjini Roma kunako mwezi Novemba 2014, alipopata nafasi ya kuwahutubia wajumbe waliokuwa wanashiriki katika mkutano ule. Baba Mtakatifu anasema kuna mamillioni ya watu yanayoendelea kusubiri kwa hamu maendeleo makubwa katika sekta ya kilimo, ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula sanjari na mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Ni wajibu wa kimaadili kutambua kwamba, upatikanaji wa chakula ni haki msingi kwa wote na wala hakuna ubaguzi.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, takwimu zinaonesha kuwa kunako mwaka 1992 kulikuwa na watu millioni 200 waliokuwa wanasumbuliwa na baa la njaa duniani, idadi hii imepungua kwa kiasi kikubwa kwa sasa. Lakini kuna haja ya kujikita katika mchakato wa kuwa na matumizi bora na sahihi ya chakula kwa kubadili mfumo na mtindo wa maisha. Watu wapate chakula bora na kadiri ya viwango vinavyotakiwa ili kuwawezesha kuwa na afya bora. Hii ni changamoto kwa FAO kuhakikisha kwamba, inakuwa karibu na wakulima vijijini, badala ya wataalam wa kilimo, “kufunga tai na kula kiyoyozi mijini”.

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatisha, lakini rushwa na ufisadi ni saratani inayokwamisha maendeleo endelevu ya watu kwa kutambua kwamba, mazao ya nchi ni matunda matakatifu yanayopaswa kulindwa, kwa kutambua mahitaji ya wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kuhakikisha kwamba, malengo yaliyowekwa na FAO yanafikiwa kwa kiwango cha kuridhisha, ili hatimaye, kuwa ni kiwango bora cha maisha ya wananchi wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, ili kukabiliana kikamilifu na baa la njaa duniani kuna haja ya kujenga na kudumisha mshikamano wa dhati katika masuala ya rasilimali fedha na ujuzi; kwa kuwa waaminifu kwa fedha ya umma, ili kukoleza ushirikiano wa kimataifa. Sera na mikakati ya kiuchumi, isaidie mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, ili watu waweze kuonjeshana ukarimu, vinginevyo, itakuwa ni vigumu sana kutenga fedha ya maendeleo kwa ajili ya nchi hitaji. Umaskini ni tatizo la kijamii linalopaswa kushughulikiwa kikamilifu na kwamba, ushirikiano wa kimataifa ni njia pekee ya kupambana na changamoto mbali mbali duniani.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, kuna haja ya kuelimisha jamii kuhusu lishe bora na sahihi; kwa kuwa na chakula cha kutosha bila kutupa ovyo chakula pamoja na kuwawezesha wale wasiokuwa na chakula kupata mahitaji yao ili kuondokana na utapiamlo ambao una athari kubwa kwa watoto. Jumuiya ya Kimataifa iwe pia na matumizi sahihi ya maji, kwani maji ni haki msingi kwa wote na yanaweza kutumika kwa ajili ya kilimo cha kumwagilia mashamba, lakini daima mwanadamu apewe kipaumbele cha kwanza.

Baba Mtakatifu anakemea tabia ya ukwapuaji wa maeneo makubwa ya ardhi unaofanywa na Mashirika na Makampuni ya kimataifa kutoka kwa wakulima wadogo wadogo. Ikumbukwe kwamba, wazalishaji wakuu wa chakula ni familia zinazopaswa kupewa haki ya kumiliki ardhi kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao. Hii ni changamoto ya kimataifa inayopaswa kufanyiwa kazi, ili kuweza pia kuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani.

Dhana ya uhakika wa chakula inatofautina kati ya Nchi tajiri na zile zinazoendelea duniani, kwa matajiri, usalama wa chakula ni kuondoa lehemu ili watu waweze kuwa wepesi kutembea, kwa watu wanaotoka katika nchi maskini duniani, hapa ni kuwa na uhakika wa mlo wa siku. Mabadiliko katika mfumo na mtindo wa maisha ni muhimu sana anasema Baba Mtakatifu Francisko, mchakato unaopaswa kuanza kutekelezwa kila siku ya maisha ili kupambana na baa la njaa duniani. Inakadiriwa kwamba, ifikapo mwaka 2050 idadi ya watu duniani itakuwa imefikia watu billioni tisa, kumbe uzalishaji wa chakula hauna budi kuongezeka maradufu. Watu wawe na matumizi bora ya ardhi na rasilimali ya dunia; wajenge utamaduni wa kutunza chakula na kugawana na wengine.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.