2015-06-10 15:01:00

Familia ni madhabahu ya Injili ya uhai, shule ya imani na utu wema!


Baraza la Maaskofu Katoliki Congo, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa 43 wa Mwaka uliokuwa unafanyika mjini Brazzaville kwa kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, changamoto ya kupambana na mambo yanayoendelea kusababisha umaskini wa hali na kipato; kukuza na kudumisha haki, amani na upatanisho kama sehemu ya mchakatowa Uinjilishaji mpya sanjari na kukataa kishawishi cha kupokea misaada inayofumbatwa katika utamaduni wa kifo.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linafafanua kwamba, familia ni madhabahu ya maisha ya mwanadamu, shule ya imani na utu wema; msingi wa jamii na mahali muafaka pa kujifunza na kurithisha tunu msingi za maisha ya kimaadili, kiroho na kiutu, tayari kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu. Ukuu na ubora wa jamii yoyote ile unapimwa kwa kuzingatia ubora wa maisha ya familia na kwa namna ya pekee kabisa, familia za Kikristo ni Kanisa dogo la nyumbani.

Kwa njia hii, wanafamilia wanaweza kukabiliana kikamilifu na mila pamoja na desturi zilizopitwa na wakati, kwa kukataa sera za mfumo dume, ubinafsi, tamaa mbaya, mambo yanayodhoofisha dhamana n anafasi ya wazazi katika malezi na makuzi ya watoto wao. Familia zijenge utamaduni wa kuwaheshimu na kuwaenzi wazee pamoja na kudumisha usawa kati ya Bwana na Bibi.

Ikumbukwe kwamba, ndoa ya Kikristo ni kati ya Bwana na Bibi, kadiri ya mpango, utu na heshima ya binadamu na wala si vinginevyo. Familia ina dhamana na wajibu wake msingi, mambo ambayo kamwe hayawezi kuondoshwa kwao. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kuendelea kuimarisha utambulisho wa familia ya Kikristo, unaojikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linabainisha changamoto ambazo zinaendelea kuikabilia Familia ya Mungu nchini humo. Imani za kishirikina, elimu makini kwa watoto na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato. Kuna haja ya kujifunga kibwebwe kupambana na umaskini, ili kuendeleza familia, kwa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na huduma za tiba. Familia ziwajibike barabara katika kutoa lishe bora kwa watoto wao, dhamana inayoweza kuboreshwa zaidi kwa kushirikiana na asasi mbali mbali zilizopo.

Maaskofu wanazitaka Familia kutambua dhamana na mchango wake katika kuelimisha amani na kwamba, katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, familia za Kikristo hazina budi kuwa vyombo makini vya Uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika maisha, umoja na upendo. Wawe ni vyombo vya majadiliano katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, ili kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Wazazi wawaelimishe watoto wao kuwa na matumizi bora na sahihi ya vyombo vya upashanaji habari na mitandao ya kijamii.

Maaskofu wanawakumbusha wakleri na watawa kwamba, Uinjilishaji mpya unatoa kipaumbele cha pekee kwa familia, kumbe, wanapaswa kuzisaidia na kuziwezesha familia kutekeleza dhamana hii nyeti katika maisha na utume wa Kanisa. Wawasaidie wanafamilia kuwa na majiundo pamoja na katekesi endelevu inayozingatia mafundisho tanzu ya Kanisa; umuhimu wa kujikita katika kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Serikali kwa upande wake, itunge sera na sheria zinazozingatia mahitaji ya familia, kwa kuheshimu kanuni maadili za maisha ya ndoa na familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linasema, kuna haja ya kuwafunda vijana katika kanuni maadili na utu wema; kwa kukazia umoja na mshikamano wa kitaifa ili kupambana na: ukabila, udini, chuki na uhasama unaoweza kupelekea kutoweka kwa amani na utulivu. Kamwe vijana wasikubali kutumiwa na wanasiasa “uchwara” kwa ajili ya mafao yao binafsi. Waendelee kujikita katika majadiliano mbali mbali katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi.

Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Congo linaitaka Serikali kuwa makini na Mashirika pamoja na Jumuiya za Kimataifa zinazotoa misaada ya masharti, kiasi cha kuhatarisha kanuni maadili na utu wema. Kamwe wasikubali kupokea misada inayokumbatia utamaduni wa kifo. Familia ni mahali patakatifu kwa ajili ya kukuza na kudumisha Injili ya Uhai, amani, haki, upendo na udugu. Haya ndiyo mambo msingi ambayo Maaskofu Katoliki Congo wanataka yapewe msukumo wa pekee na Familia ya Mungu nchini humo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.  








All the contents on this site are copyrighted ©.