2015-06-09 08:37:00

Taasisi ya Amani Eneo la Maziwa Makuu yaundwa, Bukavu, DRC.


Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, ACEAC, linaloundwa na Maaskofu kutoka Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Watu wa Congo, DRC, limeamua kuanzisha Taasisi ya Amani Eneo la Maziwa Makuu, ili kuharakisha mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Eneo hili limekuwa ni uwanja wa fujo, vurugu, vita na nyanyaso za kila aina.

Padre Edouard Mobili, Katibu mkuu wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati anasema kwamba, lengo la kuanzisha kituo hiki ni kusaidia mchakato wa haki, amani na upatanisho. Makao makuu ya taasisi hii yatakuwa ni Bukavu, kusini mwa Jimbo la Kivu; eneo ambalo limekuwa ni kitovu cha migogoro na vita nchini DRC.

Taasisi ya Amani Eneo la Maziwa Makuu inatarajiwa kuanza kutekeleza dhamana yake, Mwezi Oktoba, 2015, inapania kuwa ni chombo cha shughuli za kichungaji sanjari na majiundo ya kielimu. Hapa wanafunzi watapewa mafunzo kwa kina na mapana kuhusu amani, utawala bora, mazingira, rasilimali, jinsia; matatizo, changamoto na fursa za kifamilia; amani na vyombo vya mawasiliano ya kijamii; amani na utawala bora; amani na elimu ya uraia.

Taasisi hii itaendesha shughuli zake kwenye Seminari kuu ya Bukavu na hivyo, Taasisi hii itakuwa ninashirikiana kwa karibu zaidi na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Bukavu, Chuo Kikuu cha Kikatoliki DRC, UNESCO nchini DRC, Chuo Kikuu cha Rwanda pamoja na Chuo Kikuu cha San Diego, kilichoko nchini Marekani. Kifaransa na Kiingereza ndizo lugha zitakazotumika kufundishia masomo katika Taasisi ya Amani Eneo la Maziwa Makuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.