2015-06-09 15:23:00

Mkihitimu masomo, iweni wepesi kufunga vilago kurejea makwenu!


Chuo Kikuu cha Kimissionari cha Kipapa Kimataifa “San Paolo” kilichoko mjini Roma, kinaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kilipoanzishwa. Tangu wakati huo, kimeendelea kuwa ni kitalu muhimu cha majiundo kwa ajili ya Wakleri kutoka katika nchi za kimissionari. Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu katika mahubiri yake kama kilele cha maadhimisho haya amewataka Wakleri na Majandokasisi wanapomaliza masomo yao, wawe wepesi kurejea nchini mwao, ili kusaidia harakati za Uinjilishaji wa kina.

Kardinali anasema kwamba, wamissionari wazalendo wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa watu, ikilinganishwa na miaka kadhaa iliyopita, ambapo Makanisa machanga yalitegemea zaidi wamissionari kutoka nje ya nchi zao. Wamissionari wazalendo wahakikishe kwamba, wanapokea dhamana ya Uinjilishaji kwa ndugu zao kwa moyo wa shukrani na upendo.

Kardinali Filoni amepembua kwa kina na mapana historia ya Chuo kikuu cha Kimissionari cha Kipapa Kimataifa sanjari na maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mashahidi wa Uganda, waliotangazwa kuwa Watakatifu wakati wa fukuto la maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa lilionesha ari na mwamko wa kimissionari, dhamana iliyovaliwa njuga na Mwenyeheri Paulo VI, ambaye kwa namna ya pekee, aliwataka Wamissionari kutoka Barani Afrika kuwa sasa ni Wamissionari kwa ajili ya Bara la Afrika.

Hiki kilikuwa ni kipindi ambacho Makanisa mahalia yalianza pia kupata Maaskofu wazalendo, kielelezo cha kukomaa na kuimarika kwa maisha na utume wa Makanisa mahalia lakini kwa kuendelea kushikamana na Kanisa la Kiulimwengu chini ya uongozi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kardinali Filoni amekaza kusema kwamba, anaendelea kuwahamasisha Maaskofu, Mapadre na Majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanapohitimu masomo yao, mara moja wawe wepesi kurejea tena nchini mwao, tayari kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Fursa za masomo zinazotolewa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu sanjari na nafasi za masomo zinazogharimiwa na Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kwa mwaka zinafikia zaidi ya wanafunzi 500.

Kardinali Filoni anasema wengi wao ni: Majandokasisi, Mapadre na Watawa. Hawa ni matunda ya sadaka na majitoleo ya waamini wanaoendelea kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali kwa kuhakikisha kwamba, linapata viongozi waliofundwa barabara, tayari kurejea kwenye Makanisa mahalia, ili kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.