2015-06-09 15:48:00

FAO inahimizwa kujikita katika: sheria, usawa na hifadhi za kijamii


Viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa wanalitaka Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa, FAO kuhakikisha kwamba, linakita sera na mikakati yake kwa kuzingatia sheria, usawa na hifadhi za kijamii. Hayo yamebainishwa hivi karibuni wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa 39 wa FAO, unaowashirikisha wajumbe kutoka katika nchi 194 na kati yao kuna Mawaziri wa Kilimo 130, wanaoendelea kupanga sera na mikakati ya FAO kwa kipindi miaka minne ijayo.

Rais Sergio Mattarella wa Itali katika hotuba yake ya ufunguzi kwa mkutano mkuu wa FAO amekaza kusema kwamba chakula ni haki msingi katika kuendeleza maisha ya binadamu na kwamba, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuwa na amani ya kudumu, lazima ijifunge kibwebwe kupambana na umaskini, baa la njaa na utapiamlo wa kutisha. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujielekeza katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo endelevu, ili kuondoa mambo yanayosababisha mipasuko ya kijamii, tayari kucharuka katika ukuaji wa kiuchumi.

Rais Mattarella anasema kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi, uhaba wa rasilimali na ukosefu wa uhakika wa usalama wa chakula duniani pamoja na nishati ni mambo ambayo athari zake zinavuka mipaka ya nchi kijiografia. Kumbe hapa, watunga sera na wachumi wanapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi kwa kujikita katika ushirikiano na mshikamano wa kimataifa, kwa kukazia misingi ya haki, ruzuku kwa ajili ya mikakati ya maendeleo na teknolojia rafiki, bila kusahau wajibu wa kudhibiti uzalishaji wa hewa ya ukaa inayotisha usalama na maisha ya binadamu. Mambo yote haya yaangaliwe kwa kina na mapana, kwa ajili ya mafao ya wengi wakati wa mkutano wa kimataifa utakaozungumzia mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa.

Viongozi mbali mbali wa kimataifa waliopata nafasi ya kushirikisha mawazo na maoni yao, wamekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na sera makini zaidi na zenye ufanisi katika mikakati ya uzalishaji, ugavi pamoja na udhibiti wa lishe duni kwa maskini wanaojikuta wakielemewa na utapiamlo wa kutisha; lishe mbaya kwa watu wanaokula na matokeo yake kuwa na unene wa kupindukia, unaohatarisha maisha yao.

Ili kupambana na baa la njaa duniani, wanawake na vijana ambao ndio wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula, hawana budi kujengewa nguvu ya kiuchumi, ili kushiriki kikamilifu katika mapambano ya baa la njaa na utapiamlo. Wanawake wapewe haki zao msingi pamoja na kuondokana na mfumo dume, ambao umekuwa ni chanzo cha kudumaa kwa wanawake katika sekta mbali mbali za maisha. FAO iendelee kutoa msaada wa fedha na teknolojia rafiki kwa nchi wanachama katika mapambo dhidi ya baa la njaa na utapiamlo.

Kwa upande wake, Luiz Inacio Lula da Silva, Rais mstaafu wa Brazil anasema, nchi yake ilifanikiwa kupambana na baa la njaa na utapiamlo, kwa kuboresha maisha ya wananchi wa Brazil, hali ambayo imepelekea Brazil kupunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wananchi wake wanaokabiliwa na baa la njaa kwa kubakia na asilimia 5% peke yake, ikilinganishwa na asilimia 20% wakati alipokuwa anaingia madarakani.

Brazil imefanikiwa kupambana na baa la njaa kwa kuwajengea wananchi vijijini uwezo wa kiuchumi pamoja na kuwpatia pembejeo; Serikali ilibainisha sera na mikakati bora katika mapambano ya baa la njaa na umaskini; kwa kuboresha huduma za afya na elimu pamoja na kusisitizia ukweli na uwazi katika matumizi ya fedha za umma. Lakini jambo la msingi, lilikuwa ni kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu na heshima ya binadamu pamoja na kuangalia mahitaji yake msingi. Mapambano dhidi ya baa la njaa na utapiamlo duniani ni jambo ambalo kimaadili na kisayansi linawezekana kabisa, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.