2015-06-09 08:18:00

Dhana ya usawa wa kijinsia isiwe ni kikwazo cha tunu msingi za maisha ya ndoa!


Simameni kidete kupinga dhana potofu ya usawa wa kijinsia; kuzeni ni kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; jengeni umoja na mshikamano ili kukabiliana na changamoto za kijamii; Maaskofu kama kielelezo cha wachungaji wema, wawe ni vyombo vya huruma ya Mungu, tayari kukuza na kudumisha miito mbali mbali ndani ya Kanisa.

Kwa ufupi, haya ni kati ya mambo makuu yaliyopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 8 Juni 2015 katika hotuba yake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Porto Rica, linaloendelea na hija yake ya kichungaji, inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Sakramenti ya Ndoa Takatifu inayoundwa katika upendo thabiti kati ya bwana na bibi.

Hii ni amana kubwa kwa Familia ya Mungu Amerika ya Kusini. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuendelea kujikita katika utume wa familia ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto kubwa zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi. Masuala ya hali ngumu ya kiuchumi, wahamiaji na wakimbizi; nyanyaso na ukatili wa majumbani; ukosefu wa fursa za ajira bila kusahau biashara na matumizi haramu ya dawaza kulevya; mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Lengo ni kutangaza na kushuhudia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Mwenyezi Mungu ameumba mwanaume na mwanamke ili waweze kukamilishana na kutakatifuzana; kazi hii ya uumbaji inatiwa majaribuni na kile kinachodaiwa kuwa ni usawa wa kijinsia, kwa kisingizio cha kutaka kujenga jamii iliyo haki na sawa. Lakini, ikumbukwe kwamba, tofauti za kijinsia si kwa ajili ya kusababisha kinzani na misigano; wala kumtweza mwanamke na badala yake, tofauti hizi zinapania kujenga na kudumisha umoja, kuendeleza kazi ya uumbaji, kwa kutambua kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu Katoliki nchini Porto Rica, kushikamana katika sala, urafiki na udugu, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza nchini mwao. Hakuna sababu ya kupoteza nguvu katika kinzani na migawanyiko isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Porto Rica.

Maaskofu wawe makini kung’amua sera na mikakati ya kisiasa inayotaka kuwagawa ili kupoteza dira na mwelekeo katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Kanisa halifungamani na chama chochote cha kisiasa, kama wanavyosema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili liweze kusimama kidete kulinda utu na heshima ya binadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu Katoliki wa Porto Rica kuwa ni mfano bora wa kuigwa na Wakleri wao, kwa kujikita katika mchakato unaolenga kuyapyaisha maisha yao ya kiroho, ili kugundua furaha ya kuongoza Familia ya Mungu ndani ya Kanisa.

Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Wakleri wanaalikwa kwa namna ya pekee kuwa ni wahudumu wa upendo na huruma ya Mungu, kwa kuwajalia waamini kushiriki kikamilifu katika Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Lakini ikumbukwe kwamba, wachungaji wema na watakatifu ni matunda na mikakati makini ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya miito mitakatifu. Majiundo makini yakuzwe kwa namna ya pekee Seminarini.

Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Porto Rica kwa kutaka waamini na vyama vya kitume nchini Porto Rica, wahamasishwe ili waweze kushiriki katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za maisha, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.