2015-06-08 09:01:00

Wananchi wa Sudan ya Kusini wamechoshwa na vita, wanataka amani!


Viongozi wa Baraza la Makanisa nchini Sudan ya Kusini, kwa mara nyingine tena wanawataka viongozi wa kisiasa na kijeshi nchini humo kusitisha mapambano ya silaha na kuanza kujikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kweli Sudan ya Kusini iweze tena kuanza mchakato wa amani, ustawi na maendeleo ya watu wake.

Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini, linapenda kuwa ni sauti ya wanyonge na watu wanaoendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo kwa sasa imekuwa kama wimbo usiokuwa na kiitikio. Wanasiasa na wanajeshi wameshikwa na uchu wa mali na madaraka kiasi hata cha kusahau mateso na mahangaiko ya watu wa kawaida. Habari zinazoendelea kusikika kutoka sehemu mbali mbali za Sudan ya Kusini zinaonesha kwamba, hali inazidi kuwa mbaya kila kukicha.

Viongozi wa Makanisa wanasema hakuna sababu ya kimaadili wala kisiasa inayoweza kuhalalisha vita inayoendelea nchini humo. Hadi wakati huu, mikataba ya amani na utulivu iliyotiwa sahihi kwa mbwembwe na bashasha kubwa kiasi cha kuwajengea wananchi matumaini ya kupata amani na usalama, imeendelea kuvunjwa kila wakati kati ya Serikali na upinzani na matokeo yake, kila upande unaendelea kujiimarisha kijeshi kwa kutaka kudhibiti maeneo yanayozalisha nishati ya mafuta, chanzo kikuu cha fedha zinazogharimia mapambano ya kijeshi; fedha ambayo inanuka damu ya watu wasiokuwa na hatia.

Baraza la Makanisa Sudan ya Kusini linasema kwamba, utajiri wa mafuta na rasilimali mbali mbali zinazopatikana nchini Sudan ya Kusini ni mali ya umma inayopaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Sudan ya Kusini na wala si kwa ajili ya mafao ya watu wachache wenye uchu wa mali na madaraka. Wananchi wanapaswa kulinda utajiri huu na kamwe usitumiwe kuwa ni uwanja wa fujo.

Kuna idadi kubwa ya wananchi wanaoendelea kuuwawa kikatiliki; wanawake na wasichana kunyanyaswa na kudhulumiwa kijinsia pamoja na watoto kupelekwa mstari wa mbele kama chambo cha mapigano, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Tangu Desemba 2013, mapambano yalipoibuka tena Sudan ya Kusini, zaidi ya wananchi millioni mbili wamelazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.