2015-06-08 11:54:00

Maisha ni mwendo mdundo, hakuna kusimama, ukianguka nyanyuka haraka sana!


Mahujaji kutoka Macerata mwishoni mwa juma, yaani Jumamosi, tarehe 6 Juni 2015 wametembea mwendo wa kilometa 27 kuelekea kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Loreto,Nchini Italia, hii ikiwa ni hija ya thelathini na saba. Mahujaji wametumia fursa hii kusali, kuimba na kutembea kwa ukakamavu pasi na kuchoka. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya mazungumzo ya simu na mahujaji hao kabla ya kuanza hija hii ya maisha ya kiroho inayofanyika kila mwaka kwa heshima ya Bikira Maria amekazia umuhimu wa hija ya maisha ya kiroho. Hiki ni kielelezo cha imani na upendo kwa Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu alipenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu katika hija hii, kwa kutambua kwamba, hija ni alama ya maisha yanayopaswa kusonga mbele bila kusimama kwani yakisimama hapo kuna hatari. Ni sawa na maji ya mto yanayotiririka, yakisimama, maji hayo yanachafuka na wala hayafai tena kwa matumizi ya binadamu. Maisha ya kiroho ni safari ndefu inayopaswa kujikita katika huduma kwa jirani, lakini zaidi kwa maskini; ni hija ya kumtafuta ili kumkumbatia Mungu katika maisha na kwamba, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu anayewaimarisha kiroho.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, binadamu katika maisha yake si mkamilifu anaweza kutekeleza na kuanguka, lakini anapaswa kusimama na kuendelea na safari ya maisha kwa nguvu na ari kuu zaidi. Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa alisikika mara kwa mara akiwahimiza waamini wake kuimba na kutembea katika furaha, hata pale moyo unaopoonekana kuwa ni mgumu au umeelemewa na simanzi. Wakati wa hija, waamini wajifunze pia kupumzika na kuvuta pumzi, tayari kujichotea nguvu ya kusonga mbele kwa imani na matumaini makuu.

Baba Mtakatifu anasema katika matembezi, mtu anaweza kukosea barabara na hapo ”pakawa ni patashika nguo kuchanika”, lakini waamini wanapokumbana na hali kama hii, wanapaswa kukimbilia kwa Yesu ili aweze kuwaonjesha tena huruma na upendo wake unaokoa. Katika hija ya maisha, Yesu anapenda kuwabembeleza waja wake kwa njia ya huruma, msamaha na upendo usiokuwa na kifani. Kila mwamini anafahamu historia ya maisha yake ya kiroho, awe ni mwepesi kukimbilia huruma ya Mungu pale anapotambua udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu.

Waamini watapata furaha na amani ya ndani kwa kukutana na Yesu katika maisha yao. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, hija hii ya maisha ya kiroho, itawasaidia kwa namna ya pekee kabisa kuboresha mahusiano kati yao na Mwenyezi Mungu, ili kweli waweze kuwa ni wajumbe wa Injili ya Furaha na vyombo vya huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.