2015-06-08 15:07:00

Dr. Graziano da Silva achaguliwa tena kuiongoza FAO hadi mwaka 2019


Wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, wamemchagua Dr. Graziano da Silva kuwa Mkurugenzi mkuu wa FAO kwa awamu ya pili yaani kuanzia tarehe 31 Julai 2015 hadi Julai 2019. Dr. Graziano da Silva ni kiongozi pekee aliyekuwa anawania nafasi hii na kwamba, amepata kura nyingi kuwahi kupigwa katika historia ya FAO.

Uchaguzi huu umefanyika siku ya kwanza ya mkutano mkuu wa FAO, uliofunguliwa rasmi hapo tarehe 6 Juni na unatarajiwa kuhitimishwa hapo tarehe 13 Juni 2015. Tangu Dr. Graziano da Silva kutoka Brazil alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuiongoza FAO kunako mwaka 2012 amefanya mabadiliko makubwa kwa kuiwezesha FAO kuguswa na mahangaiko ya wajumbe wake, tayari kuyafanyia kazi kwa kuibua mbinu mkakati.

Katika uongozi wake, ameendelea kuielekeza FAO kupambana fika na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha unaoendelea kunyanyasa utu na heshima ya mamillioni ya watu duniani. Ni kiongozi aliyejielekeza katika kanuni maadili na sheria za kazi, kiasi kwamba, amepunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji wa FAO ambazo wakati fulani zilionekana kuwa ni kero na “zigo” lisilobebeka na wanachama wa FAO, kiasi kwamba wakataka mageuzi makubwa katika udhibiti wa fedha ya kimataifa, vinginevyo, FAO ilikuwa inakosa sifa ya kuendelea kuwepo kwa ajili ya kupambana na baa la njaa duniani.

FAO pia imeendelea kuimarisha mahusiano yake na wadau mbali mbali kutoka nje ya wanachama wake sanjari na kukuza mahusiano kati ya Nchi zilizoko Kusini mwa Dunia. Dr. Graziano da Silva si mgeni sana katika shughuli za FAO kwani alianza kuwa ni mwalikilishi wa FAO kutoka nchi za Amerika ya Kusini na Caraibi kunako mwaka 2006, akachaguliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa FAO hapo tarehe 26 Juni 2011. Huyu ni mkurugenzi mkuu wa nane wa FAO tangu ilipoanzishwa kunako mwaka 1945.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.