2015-06-07 07:51:00

Yakiteni maisha yenu katika utakatifu, kwa njia ya huduma kwa maskini!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 6 Juni 2015 wakati wa hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, amekutana na kuzungumza na Wakleri, Watawa na Majandokasisi kwenye Kanisa kuu la Moyo Mtakatifu wa Yesu, Jimbo kuu la Sarayevo. Hapa ni mahali ambapo kunako mwaka 1997 Papa Yohane Paulo II  alikutana na kuzungumza na Wakleri, wakati alipotembelea nchini humo.

Baba Mtakatifu Francisko alipowasili amepokelewa na viongozi wa Kanisa, akapata nafasi yak usali kidogo mbele ya Ekaristi takatifu pamoja na kusali kwenye kaburi la Mtumishi wa Mungu Askofu Giuseppe Stadler, Askofu mkuu wa kwanza wa Jimbo kuu la Sarayevo. Baba Mtakatifu amesikiliza shuhuda kutoka kwa Padre na watawa wawili. Amewashukuru viongozi wa Kanisa kwa huduma makini ambayo Kanisa linaendelea kutoa kwa ajili ya ustawi na maendeleo endelevu ya wananchi wa Bosnia-Erzegovina katika ujumla wao.

Hii ni huduma inayotolewa katika mazingira magumu, ndiyo maana anapenda kuwaimarisha ndugu zake katika imani, ili wadumu katika faraja na matumaini wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa Familia ya Mungu, hasa kwa kuzingatia kwamba, wao ni sehemu ndogo sana ikilinganishwa na waamini wa dini nyingine.

Mapadre na Watawa wanakumbushwa kwamba, mafanikio ya shughuli na mikakati ya kichungaji ni matokeo ya imani na upendo kwa Yesu pamoja na kuendelea kushikamana kidugu katika Kristo. Watawa wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa udugu, kwani wameacha yote kwa ajili ya kumfuasa na kumtumikia Kristo kati ya ndugu zake wadogo.

Kwa namna ya pekee kabisa, Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha Mapadre na Watawa kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya Watu wa Mungu; kwa kushikamana na maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; mambo msingi yanayowasaidia kukua na kukomaa katika hija ya maisha ya utakatifu, kwani hata maskini wanaweza kuwatajirisha katika maisha yao ya kiroho. Viongozi wa Kanisa wanahamasishwa kuwa ni wachungaji wa matumaini kwa wananchi wa Bosnia-Erzegovina.

Hii ni changamoto kwa viongozi wa Kanisa kutoka kifua mbele, ili kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, ili watu waweze kuiona njia inayowapeleka kwa Yesu Kristo, mkombozi wa dunia. Wahudumu wa matumaini, wanahamasishwa kuwaendea na kuwahudumia watu wanaohitaji msaada wa maisha ya kiroho na kimwili; hata wale ambao kutokana na sababu mbali mbali wanaona aibu kuomba; hao pia wanapaswa kusaidiwa.

Baba Mtakatifu anawahimiza viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanatoa kipaumbele cha pekee kwa majiundo makini ya waamini walei, ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika kuyatakatifuza malimwengu. Wawe ni watu wa matumaini kwa jirani zao.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anawaonya Mapadre na watawa wasidhani kwamba, wao ni “wateule” kiasi cha kujitenga na Familia ya Mungu, kwa kujifungia katika ubinafsi wao, bali wawe ni mfano wa huduma makini kwa watu: kiroho na kimwili, ili watu waweze kuonja: ukarimu, upendo na uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake.

Majandokasisi wameoneshwa ushuhuda uliotolewa na Mtumishi wa Mungu Petar Barbaric kiungo muhimu sana nchini Bosnia-Erzegovina. Alikuwa Mseminari aliyekuwa anajiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja Takatifu, kwa mfano wa maisha na karama zake mbali mbali anakuwa ni kielelezo na mfano bora wa kuigwa. Katika shida na magumu wasisite kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, anayewafundisha kusikiliza kwa makini na imani thabiti, ili kweli waweze kuwa ni vyombo vya matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.