2015-06-07 14:41:00

Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu: haki na huruma ni chanda na pete


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi Hekimishi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Hazina yetu inakutakia amani na usitawi katika mwezi huu Juni, ambapo kadiri ya desturi Katoliki ni mwezi ambao kwa namna ya pekee tunauheshimu Moyo Mtakatifu wa Yesu. Ni moyo wa huruma, ni moyo wa Mapendo.

Huruma na upendo wa Mungu Baba vimemwilishwa kwetu kwa njia ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni kimwilishi cha Ujumla wote wa Nafsi ya Kristo, yaani Umungu wake na Ubinadamu wake, Mwili wake na Damu yake, Mafundisho yake na Miujiza yake, Mfano wa Maisha yake na Sakramenti zake. Moyo Mtakatifu wa Yesu ndio Chemchemi ya Sakramenti za Kanisa. Uzima wa Kanisa, umefumbatwa katika mpango wa Mungu iliodhihirika katika moyo wazi wa Mwokozi.

Moyo Mtakatifu wa Yesu, kama tusalivyo katika litania yake;  ni tanuru lenye kuwaka mapendo na pia ni chombo cha haki na upendo. Ni ni moyo wenye uvumilivu na huruma nyingi na hivyo ni chemchemi ya uzima na utakatifu; na katika ukamilifu wa huruma hiyo, Moyo wa Yesu ni sadaka ya sisi Wakosefu.

Mpendwa msikilizaji, sifa hizi za Moyo Mtakatifu wa Yesu ambazo zinapambwa kwa huruma yake na upendo wake, zituangaze nasi tunapotafakari juu ya huruma ya Mungu kwa Mwaka huu Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Tunataka kujibidisha japo kwa yodi mmoja tu, kuzimwilisha fadhila hizo za moyo wa Yesu, ambazo kwa uchache ni, upendo, huruma, haki, uvulilivu, uwajibikaji, huduma, utii, faraja, amani na upatanisho. Haya ni baadhi ya mambo msingi ambayo kwa Mwezi huu, kwa msaada na mastahili ya Moyo Mtakatifu wa Yesu tunasaidiwa vikubwa katika kuiishi huruma ya Mungu. Moyo  Mtakatifu wa Yesu ni huruma ya Mungu na Huruma ya Mungu ni katika Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Katika kipindi kilichopita ndani ya Misericordiae vultus yaani Uso wa huruma, Baba Mtakatifu Fransisko alitualika sote kuivaa huruma kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma, akisema “jinsi wa Baba apendavyo ndivyo watoto pia wapaswa kupenda na kama Baba alivyo na huruma, ndiyo nasi pia tulivyoitwa kuwa na huruma”. Basi kioo chetu ni Moyo Mtakatifu wa Yesu ambao umetuonesha mfano wa huruma katika matendo ya maishani mwetu, na sio huruma kwa mdomo bali huruma kwa matendo.

Hakika, kutamkatamka tu maneno mazuri yenye huruma na hekima haitoshi. Yafaa kutamka maneno mazuri na kutenda matendo mema. Tukikosa muunganiko kati ya maneno yetu mazuri na matendo ya maishanimwetu, hapo kuna hatari ya kufanana kwa ukaribu sana na mafarisayo. Huruma ya Mungu inashikika. Huruma ya Yesu inashikika.

Leo, Baba Mtakatifu anaendelea kutufundisha juu ya thamani ya Huruma. Anasema “Huruma ni msingi wa maisha ya Kanisa; ni msingi wa shughuli zote za Kichungaji”. Shughuli zote za kichungaji  ndani ya Kanisa lazima ziambatwe na huruma. Mafundisho ya Kanisa, na ushuhuda wa Kanisa kwa ulimwengu, visikose huruma. Unadhifu wa Kanisa unaonekana katika namna linavyojitahidi kuonesha huruma na upendo. Anasema, Kanisa lina shauku isiyokoma ya kuonesha upendo. Anaendelea kupembua [hali tunayokuwa nayo nyakati zetu hizi], labda ni kwa sababu kwa muda mrefu sana tumesahau kuonesha na kuishi kwa namna ya huruma.

Kwa upande mmoja anasema Baba Mtakatifu, kishawishi kilichopo mara nyingi ni ile hali ya kuzingatia zaidi haki [kuliko huruma],  hali inayotufanya kusahau kwamba haki ni hatua ya kwanza tu. Hata kama haki ni ya lazima, ni hatua muhimu katika utendaji wa Kanisa; Kanisa linapaswa kwenda mbele zaidi na kujibidisha kutafuta lengo la juu na lililo bora zaidi [ambalo ni wokovu wa roho za watu]. Lengo hili hufikiwa zaidi kwa njia ya huruma.

Tunayatafakari maneno ya mshairi mmoja aliyesema “Haki bila huruma inazaa  ukatiri wa hali ya juu”. Ni kweli! Kuna wakati tunaweza kuwa mafundi sana wa kutafuta haki tu. Niseme haki, nitendewe haki, haki kwa haki, sheria ni msumeno, jino kwa jino, wembe ni wembe, na maneno mengine mengi ya kigaidi kama hayo; lakini tunasahau Kristo anapotuasa “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni” (Mt. 5:20).

Tusisahau, mtu mwenye hekima na upendo, haonekani tu katika kufuata sheria na haki, bali anabainishwa katika kuweka katika mizani-ponyaji haki na huruma. Kuishi kwa haki peke yake, kuna hatari ya kuunda watu wanafiki na wagumu wa mioyo. Na kuishi kwa huruma peke yake bila haki kuna hatari ya kuunda watu wazembe wasiojali mambo, kwa sababu wanajua kwamba watahurumiwa tu.  Ndio maana Baba Mtakatifu amesema, “haki ni hatua ya kwanza” ya mahusiano. Ila Kanisa lazima “liende mbele zaidi”, yaani kuivaa huruma inayookoa. Bila huruma ya Mungu “nani atasimama”? Mzaburi anahoji. Sasa katika dunia yetu ya leo, wengi tunajifanya kuishi kwa haki na kusahau kabisa kama kuna huruma. Mshairi anasema “Haki na huruma ni mabawa yanayosaidiana kurusha maisha katika mruko unaotakiwa”.

Kwa upande mwingine, anaendelea kubainisha Baba Mtakatifu; inasikitisha [lakini] lazima tukubali kwamba, maisha ya huruma yanapunga mkono katika jamii kwa ujumla. Katika nafasi fulani yaelekea hata neno huruma lenyewe limepoteza maana kabisa na [halitumiki tena]. Hata hivyo, bila kuishuhudia huruma, maisha maisha yanakosa maana, yananakuwa ni maisha tasa, maisha yasiyo na matunda; yanakuwa kama maisha yaliyopandwa katika jangwa kame.

Baba Mtakatifu anakaza kusema “Wakati umefika kwa Kanisa kuitikia upya wito mfurahivu wa  huruma. Ni muda wa kurudi kwenye misingi, na kutwaa madhaifu na mahangaijo ya kaka na dada zetu. Huruma ni nguvu inayotuamsha katika maisha mapya na [pia ni nguvu] inayotujaza ujasiri kwa kuutazama wakati ujao kwa matumaini.

Mpendwa msikilizaji tukiwamo ndani ya mwezi huu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu tuendelee kusali tukisema “Ee Moyo Mtakatifu wa Yesu – Ufalme wako Ufike” na “Ufanye mioyo yetu ifanane na Moyo wako”. Asante kwa kuisikiliza radio Vatican.

Kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni Mimi Padre Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.