2015-06-05 15:25:00

Msigeuze Mashirika ya Kipapa ya Kimissionari kuwa kama NGOs!


Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni kati ya wadau wakuu wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, kwa kutambua kwamba, mwanadamu ana kiu ya kutaka kusikia Neno la Mungu kwani mchakato wa Uinjilishaji ni kati ya vipaumbele vya Kanisa hadi wakati huu. Hizi ni juhudi ambazo zinapaswa kujikita katika furaha, ukarimu, ukweli, upendo na ushuhuda wenye mashiko.

Uinjilishaji ni chachu ya mageuzi katika maisha, utume pamoja na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa sanjari na mchakato wa maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili. Hii ni dhamana inayopaswa kutekezwa na mihimili yote ya Uinjilishaji hadi miisho ya dunia kwa kuendelea kuyasindikiza Makanisa machanga sehemu mbali mbali za dunia pamoja na kuwahamasisha waamini kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Roho Mtakatifu anaendelea kutenda miujiza katika Makanisa machanga ambayo kwa wakati mwingine hayana rasilimali fedha, lakini yanatekeleza dhamana hii kati ya watu; ni Makanisa ambayo wakati mwingine yanakumbana na dhuluma na nyanyaso kutokana na imani na uaminifu wao kwa Kristo na Kanisa lake. Ni waamini wanaoshibana na Neno la Mungu huku wakisimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Haya ni Makanisa yanayotekeleza utume wake pembezoni mwa jamii, huko ndiko wanakokutana na ndugu zao katika Kristo, wanaoishi bila nguvu, mwanga na faraja ya Yesu Kristo; wala Jumuiya ya Imani inayowapokea wala kuwa na mwelekeo wa maisha. Hii ni hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na Wajumbe wa mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa, POM, Ijumaa, tarehe 5 Juni 2015.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu na Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa ni wadau makini katika mchakato wa upyaisho wa Uinjilishaji unaoelekezwa kwa wote, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa kwa asili yanajipambanua kwa kuguswa kwa namna ya pekee na mahitaji ya Makanisa mahalia kwenye nchi za kimissionari, hasa miongoni mwa maskini. Ni kiungo cha upendo na mshikamano unaojengeka kwa kushirikishana rasilimali watu na mali kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Mashirika haya yanaendelea kuyasaidia Makanisa machanga, majiundo makini ya Majandokasisi na Wakleri katika Vyuo vya kipapa; dhamana inayotekelezwa kwa kuzingatia imani na upendo wa Kristo unaowawajibisha kutoka kimasomaso ili kutangaza Injili ya upendo, udugu na haki; dhamana inayotekelezwa kwa njia ya sala, ujasiri wa Kiinjili na ushuhuda wa Heri za Mlimani, ambao ni muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Wakurugenzi wa Mashirika ya Kipapa kwamba, fedha ni muhimu sana katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli za kichungaji, lakini kamwe wasiwe  ni watumwa wa fedha kwa kuipatia kipaumbele cha kwanza kama dira ya utume wao. Watambue kwamba, hii ni kazi wanayoitekeleza kwa niaba ya Yesu Kristo anayepaswa kuwa ni dira na mwongozo wa shughuli zao.

Viongozi wa Kanisa wanaojitafuta wenyewe, ni dalili kwamba, Kanisa halina matumaini ya kuendelea kuwepo kwa siku za usoni. Mchakato wa Uinjilishaji ni nguvu ya Roho Mtakatifu anayepyaisha na kulitikisa Kanisa ili liweze kutoka kimasomaso ili kutangaza Injili. Bikira Maria nyota ya Uinjilisjaji awasaidie daima kuwa na ari kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu, ili furaha ya Injili iweze kufika hadi miisho ya dunia, ili kamwe asiwepo mtu ambaye anashindwa kuona mwanga wa Injili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.