2015-06-05 09:41:00

Bosnia-Erzegovina bado madonda ya vita na chuki hayajapata tiba muafaka!


Familia ya Mungu nchini Bosnia-Erzegovina, iko tayari kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya siku moja nchini humo, inayoongozwa na kauli mbiu, “amani iwe kwenu”. Askofu Tomo Vulksic wa Jimbo la Kijeshi nchini Bosnia-Erzegovina anamshukuru Mungu kwa uwepo wa amani kwa sasa. Hakuna tena vita wala mashambulizi, lakini bado kuna haja ya kuhakikisha kwamba, amani ya kweli inatawala katika mioyo na akili za watu.

Anasema bado hakuna haki wala usawa katika ushiriki mkamilifu katika masuala ya kisiasa, kitamaduni, kielimu wala matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii kwa ajili ya mafao ya wengi. Hii ndiyo hali halisi ambayo Baba Mtakatifu anakutana nayo wakati wa hija yake ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina, Jumamosi tarehe 6 Juni 2015. Ni matumaini ya Maaskofu Katoliki nchini humo kwamba, hija hii ya kitume, italeta mwamko mpya katika majadiliano ili kweli umoja na mshikamano wa kitaifa viweze kutawala, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi.

Imekwishagota miaka ishirini tangu Papa Yohane Paulo II alipofanya hija ya kitume nchini Bosnia-Erzegovina. Hiki kilikuwa ni kipindi cha vita kali, lakini kwa sasa mambo ni shwari, lakini bado madonda ya vita, chuki na uhasama hayajapa tiba kamili, kumbe bado kuna mambo mengi yanapaswa kufanyiwa kazi, ili kweli amani, upatanisho na msamaha wa kweli uweze kukita katika maisha na mioyo ya watu.

Hija ya Baba Mtakatifu itasaidia kuwaimarisha Wakristo katika imani yao; itakoleza mchakato wa majadiliano ya kiekumene na kidini, ili kweli Bosnia-Erzegovina iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Ni changamoto kwa taasisi mbali mbali nchini humo kufanya kazi kwa ushirikiano, kwa ajili ya mafao ya wengi. Wakatoliki nchini Bosnia-Erzegovina ni kati ya makundi yaliyoathirika sana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, kiasi kwamba, idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki imepungua sana kutokana na vita; kumbe, hiki ni kipindi cha kufufua matumaini na maisha mapya kwa Kanisa. Kwa waamini wengi, wanamwangalia Baba Mtakatifu Francisko kama Nabii wa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, licha ya kupita takribani miaka ishirini ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, lakini bado watu wengi wanabeba ndani mwao madhara ya vita, chuki na uhasama. Hii inatokana na ukweli kwamba, katika kipindi chote hiki, hakuna mchakato wa upatanisho na msamaha wa kitaifa ambao umetekelezwa. Matokeo yake, kuna mpasuko mkubwa katika masuala ya kisiasa, ingawa wanawake wanaendelea kuwa kweli ni vyombo vya upatanisho na maridhiano ndani ya jamii.

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko ina umuhimu wa pekee katika mchakato wa upatanisho, umoja, maridhiano na mshikamano wa kitaifa. Mwingiliano wa kijamii unaendelea kujikita katika masuala ya ndoa na familia, lakini sera na mikakati ya baadhi ya wanasiasa imeendelea kuwagawa watu kwa misingi ya ukabila na udini, kutokana na uchu wa mali na madaraka. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko iwe ni kikolezo cha ujenzi wa amani ya kweli kwa kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene; maridhiano na mshikamano wa kitaifa, kwa ajili ya mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.