2015-06-04 15:47:00

Mambo msingi ya kuzingatiwa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Kardinali Orlando Quevedo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cotobato, Ufilippini, katika hotuba yake elekezi kwenye maadhimisho ya Mkutano mkuu wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa unaoendelea hapa mjini Vatican anakazia mambo makuu manane kama sehemu ya mchakato wa kutegemeza utume wa Kanisa leo na kesho. Malezi makini ya imani yanayojikita katika ari na mwamko wa kimissionari; upendo na mshikamano kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa familia kama kitovu cha Uinjilishaji mpya.

Kardinali Quevedo anasema, Kanisa haina budi kujenga na kuimarisha Parokia kama Jumuiya zenye chapa ya kimissionari, zinazowekeza zaidi kwa waamini walei katika medani mbali mbali za maisha, ili waweze kutoka kimasomaso kuyatakatifuza malimwengu, wakiwa wamesheheni moyo na tasaufi ya kimissionari. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee na mihimili yote ya Uinjilishaji ndani ya Kanisa, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa, kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Wainjilishaji hawana budi kujibidisha kukutana na Yesu Kristo, ili kukuza na kudumisha ari na mwelekeo wa kimissionari, kwa kuzingatia ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaojikita katika haki, amani na mafao ya wengi. Wakristo wanapaswa kujenga na kudumisha umoja, mshikamano, majadiliano na udugu, kwa njia ya unyenyekevu unaojikita katika unabii kwa kuguswa na kilio cha watu wanaoteseka kutokana na utandawazi usiojali.

Wawalinde na kuwatetea watu wanaonyimwa haki zao msingi sanjari na kuhakikisha kwamba, wanakuwa mstari wa mbele katika utunzaji bora wa mazingira. Waamini wahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda wa imani, hata kama ikiwabidi kuyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Haya ni mambo msingi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya ukizingatia athari zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Kardinali Quevedo anabainisha kwamba, Kanisa kwa asili ni la kimissionari na kadiri ya mtindo wake wa maisha, halimlazimishi mtu kupokea na kukumbatia imani ya Kanisa, kwani linatekeleza dhamana na utume wake kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika kweli za Kiinjili. Kanisa katika umaskini wake, linapania kuendeleza majadiliano katika maisha ya kiroho, kitamaduni na kiuchumi, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwaonjesha upendo wa Mungu unaofariji na kuokoa.

Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa anakaza kusema kwamba, wakati huu ambapo kuna myumbo mkubwa wa maisha ya kiimani na kimaadili, kuna haja ya kurejea tena kwenye msingi wa Maandiko Matakatifu; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Haya ni mambo msingi yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee kabisa na mihimili ya Uinjilishaji pamoja na kujikita katika kipaji cha ugunduzi. Wainjilishaji wasiridhike na mafanikio yaliyokwisha kupatikana, bali waendelee kuwa na mwelekeo mpana zaidi pamoja na kufungua njia mpya za ushirikiano wa kimissionari.

Askofu mkuu Rugambwa anawataka Wainjilishaji kuwa na mang’amuzi makini kwa kuondokana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea na kuanza kujielekeza zaidi mahali ambapo kuna kilio na mateso ya watu, tayari kuwasikiliza na kuwapatia majibu muafaka. Wakurugenzi wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa wawe makini katika kuratibu na kutumia fedha ya Kanisa pamoja na kuhamasisha umuhimu wa kujitegemea kwa kutambua kwamba, misaada kutoka ng’ambo inaendelea kupungua kila mwaka. Mihimili ya Uinjilishaji, ioneshe ari na mwamko wa kutaka kujitosa kifua mbele, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.