2015-06-04 08:18:00

Ishini Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa: kusadiki, kuadhimisha na kulimwilisha


“Tuishi Ekaristi tunayounganishwa nayo katika Fumbo la imani, tugeuze matendo yetu yote yawe sawa na Ekaristi, yaani mwili na damu ya Kristo; katika Ekaristi tunampokea Kristo, na tuishi kama Kristo Bwana”

Leo tunaadhimisha Karamu ya Bwana wetu Yesu Kristo, karamu hii huitwa Karamu ya mwisho ikiwa na maana ni Karamu ya mwisho ya Pasaka ambayo Kristo alikula pamoja na wanafunzi wake kabla ya kukamatwa kwake, kuteswa na kufa msalabani. Hii ni Ekaristi Takatifu, yaani, mwili na Damu ya Kristo katika maumbo ya mkate na divai. Sherehe hii kadiri ya utaratibu wa kalenda ya kiliturujia ya Kanisa huadhimisha siku ya Alhamisi baada ya Dominika ya Utatu Mtakatifu. Lakini pia kutoka na ukuu wake na umuhimu wake katika maisha ya kiimani, sababu za kichungaji ambazo hutokana na mazingira ya mahali husika hupelekea sherehe hii kuadhimishwa katika Dominika inayofuata baada ya Sherehe ya Utatu Mtakatifu.

Ekaristi Takatifu mlo wa kipasaka unabaki kuwa ni mlo wa kipasaka lakini unaunganishwa na Kristo mfufuka. Hivyo maumbo haya ya kawaida katika jamii ya mwanadamu yaani mkate na divai yanainuliwa katika hali ya juu kabisa na kupata hadhi ya juu. Hakika tunapaswa kujongea na kupokea katika hali ya uchaji mkuu, ni Yesu mfufuka, Yesu mzima ambaye amejitoa na amekufa kwa ajili yetu. Wanafunzi wake waliandaa mlo huo mahsusi kabisa kwa ajili ya Pasaka wakimuuliza Bwana wetu Yesu Kristo: “Ni wapi utakapo tuende tukuandalie ule Pasaka?”.

Hakika mlo huu wa kipasaka ni Yesu mfufuka kwani Yeye mwenyewe alisema kama tulivyosikia katika somo la Injili “huu ni mwili wangu .... hii ni damu yangu”. Hata baada ya ufufuko wake alidhihirisha muunganiko wa Kristo mfufuka na Kristo kabla ya ufufuko, aliwaonesha madonda yake mikononi na miguuni na pia pia ubavu uliotobolewa. Hapa walipata hakika ya Yeye aliyejitoa na kuteswa kwa ajili yetu na pia hapa mlo huu wa Kipasaka unapata maana kubwa na nzito, kuwa chakula cha wokovu wetu.

Maneno ya Kristo Yesu wakati wa Karamu ya Mwisho yaligeuza maumbo haya ya kawaida ya mkate na divai na kupokea hadhi ya juu kabisa. Mkate unageuka kuwa mwili wake mtakatifu sana na Divai inageuka kuwa Damu yake iliyo azizi. Chakula hiki cha kawaida cha kidunia kinageuka kuwa karamu ya mbinguni. Si mkate kama mkate wa kawaida, ingawa tunaonja mkate katika ulimi wetu; si divai kama divai ya kawaida ingawa tunaonja divai katika ulimi wetu. Ni mwili na damu ya Kristo. Ni Kristo mzima katika maumbo ya Mkate na Divai.

Hili ni Fumbo la imani! Kwa macho yetu hatuoni, kwa ulimi wetu hatuonji lakini kama isemavyo mojawapo ya tungo za kale juu ya Ekaristi “hakuna hata! Ni mkate lakini mwiliwe twakiri sote”. Hivyo kupokea elimu hiyo kubwa ya kimbingu inahitaji msaada wa kimungu, yaani neema, na fadhila ya imani. Imani hii kuu itatuweka katika hadhi ya kuitukuza tunu hii kubwa kabisa tuliyopewa wanadamu iliyo ishara ya upendo na kifungo cha umoja.

Somo la pili katika Sherehe ya leo linatuangazia juu ya nguvu ya chakula hiki cha kimbingu ambacho kinatutakasa na dhambi zetu. Dhambi ilimtenga mwanadamu na muumba wake. Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inamtakasa mwanadamu na dhambi zake. Neno la Mungu linatuambia kuwa sadaka ya Kristo Msalabani “itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai”. Ni sadaka ya utakakaso ambayo inamuunganisha Mungu na wanadamu, inaunganisha mbingu na dunia. Kifo cha Kristo msalabani kinaifuta ile dhambi ya kale na kutufanya sasa kuwa na uwezo wa kupokea ahadi ya urithi wa milele. Tunafanywa kuwa warithi pamoja na Mwana kwa sababu tunafana naye. Kwa kula mwili wake na kuinywa damu yake tunageuzwa nafsi zetu na kuwa kama Yeye, tukimtukuza na kumtii Mungu Baba yetu wa mbinguni.

Somo la kwanza linaiunganisha Sadaka hii ya Ekaristi Takatifu na matendo yetu wanadamu. Huu ni muktadha wa maisha ya kimaadili, yaani tunaelekezwa katika utendaji wetu kurandana kadiri ya amri na maagizo ya Mungu: “Wakasema, ‘Hayo yote aliyoyanena Bwana tutayatenda, nasi tutatii”. Chakula hiki ni agano tunaloliweka na Mungu la kutenda kadiri ya amri na maagizo yako. Tuulapo mwili wake Kristo na kuinywa Damu yake tunapokea uzima wa kimungu, Kristo mwenyewe anakuwa ndiye kanuni katika utendaji wetu kama Wakristo. Ushiriki wa chakula hiki unaambatana na wajibu wa kimaadili, wajibu wa kutenda katika ulimengu huu kadiri ya mwanga wa Injili. Hivi Kristo tunayempokea anakuwa si kanuni tu lakini pia kielelezo cha maisha yetu ya kikristo.

Uwepo huu wa daima wa Ekaristi takatifu siyo wa mapambo, si jambo ambalo linakosa maana. Kristo anajiweka kwetu kama mlo ili tuushiriki mlo huo na kuneemeshwa kwa chakula hiko cha mbinguni. Ekaristi Takatifu inatupatia wajibu wa kuunganika na Kristo na kuwa ishara ya Upendo wake kwa watu wote. Tunakuwa kile tunachokipokea. Kama vile chakula cha kawaida kinavyokuwa cha faida kwa miili yetu kwa kutupatia nguvu na kukua kwa mwili, ndiyo chakula hiki cha kiroho kinakuwa nguvu na kutukuza katika maisha ya kiroho. Tunaunganika na Kristo na kufanywa kuwa yeye, yaani, tunayapokea maisha yake na kuyafanya kuwa ni maisha yetu. Yeye anakuwa ndiye chanzo cha utendaji wetu wa kikristo, kwa kumpokea tunafanywa kuwa vyombo vya kuisambaza habari njema ya Kristo kwa wanadamu wote.

Mwenyeheri Mama Maria Crocifissa Curcio, ambaye alikuwa na ibada kubwa sana katika Ekaristi Takatifu aliwaambia masista wenzake maneno haya: “Ndugu zangu nawasihi na tena nawaambieni, upendo huu mnaouchota kila siku katika Ekaristi Takatifu uenezeni ulimwenguni kote”.Katika desturi ya tangu kale ya sherehe hii waamini hufanya maandamano ya Ekaristi takatifu wakiwa na lengo la kushuhudia imani yao katika mazingira ya kawaida ya wanadamu. Kwa shangwe kubwa huku wakiimba nyimbo nzuri na tenzi za rohoni wanambeba Kristo na katika ujasiri huo wanazunguka mitaani kwa lengo la kumfikisha huyu aliye Mwanga wa Ulimwengu katika maisha ya kawaida ya mwanadamu.

Tukio hili si la kuishia tu katika shangwe za siku moja bali linapaswa kuwa ukumbusho na kichocheo cha kumpeleka Kristo tumpokeaye kila mara katika mioyo yetu wakati wa ibada ya Misa takatifu katika maisha yetu ya kawaida/ kumpeleka huko majumbani mwetu, katika sehemu zetu za kazi, katika mazungumzo yetu ya kindugu na kirafiki na mahali pengine popote. Na ndiyo maana Mwenyeheri Mama Teresa wa Calcutta alisema kuwa yeye huabudu Ekaristi Takatifu kwa muda wa masaa 24, yaani masaa machache mbele ya Ekaristi Takatifu Kanisani na muda mwingine mwingi anapokuwa na wenzake na hasa anapokuwa anahudumia maskini. Yeye aliiona sura ya Kristo katika kila mwanadamu ambaye kwa hakika ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Hili linatupeleka kuunganisha fumbo hili ya Ekaristi Takatifu na Amri ya Mapendo.  Mtakatifu Augustino anatuambia maneno yafuatayo juu ya Ekaristi Takatifu, “Ni ishara ya Umoja na kifungo cha Upendo. Sakramenti ya Ekaristi ni Sakramenti ya Upendo. Bwana wetu Yesu Kristo anatoa fundisho la namna ambayo upendo huo unapaswa kuwa; ni upendo wa kujitoa katika ukamilifu wote, kujisadaka katika uhuru wako mithili ya mtumwa. Namna yake ya utumwa ni tofauti na utumwa ulivyozoeleka. Anajitoa katika hali ya utumwa kwa uhuru wote na Mapendo makubwa.

Anatambua wazi kwamba Yeye ni Bwana na mwalimu wao, ni mkuu wao na kwa desturi hakupaswa kuwaosha miguu walio chini yake. Hapa anatupatia shule kubwa sana ya namna ambavyo tunapaswa kujitoa kuwahudumia wengine katika hali ya Upendo mkamilifu. Siyo kuangalia nguvu zangu, mamlaka yangu, uwezo wangu n.k. bali ni kumwangalia mwanadamu mwenzangu aliye mbele yangu na anayehitaji huduma yangu, anayekuwa na hakika ya kupatiwa huduma hiyo kutoka kwangu.

“Tuishi Ekaristi tunayounganishwa nayo katika Fumbo la imani, tugeuze matendo yetu yote yawe sawa na Ekaristi, yaani mwili na damu ya Kristo; katika Ekaristi tunampokea Kristo, na tuishi kama Kristo Bwana”. Sherehe ya leo itufanye tuwe mashahidi wa Ekaristi katika maisha yetu ya kila siku. Leo tuupokee utume huu, utume wa kuwa Ekaristi inayozunguka katika maisha ya kawaida ya mwanadamu, Ekaristi ambayo inawagusa wote wenye shida: wahitaji, maskini, wajane, yatima na wengine wote wenye mahangaiko wanaohitaji kuuonja upendo wa kimungu ambao umeubeba moyoni mwako. Na mwisho leo pia tuwe tayari kumwona Kristo katika nyuso ya kila mmoja wetu tunayekutana naye na kumuabudu na kumtukuza daima kwa heshima na hadhi stahiki.

Kutoka Studio za Radio Vatican, mimi ni Padre Joseph Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.