2015-06-03 16:11:00

Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu!


Mpendwa mwana wa Mungu, ninakualikeni tukatafakari pamoja Neno la Mungu leo ikiwa ni sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu. Sherehe hii ni kati ya sherehe za Bwana na huadhimishwa Dominika inayofuta mara baada ya sherehe ya Utatu Mtakatifu. Ni sherehe ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja na Alhamis kuu ambapo fumbo la Ekaristi Takatifu linawekwa katika Kanisa na Yesu Kristu mwenyewe. Siku ya Alhamis Kuu hatukupata nafasi ya kusherehekea hasa kwa shangwe na nderemo kwa kuwa tulikuwa tayari katika wiki ya mateso ya Bwana. Kumbe Mama Kanisa anatujalia nafasi tena ya kusherehekea na kushangilia kwa vigelegele na hivi wote tunaalikwa kufanya hivyo.

Ndiyo kusema katika sikukuu hii tunafanya ukumbusho wa Karamu ya mwisho, ambapo Bwana alikula karamu hiyo pamoja na wanafunzi wake. Ni katika karamu hiyo aliweka sakramenti ya Ekaristi na sakramenti ya Upadre. Mama Kanisa hufanya maandamano katika siku hii ikiwa ni ishara ya ushuhuda wa imani tukitangaza ukuu wa Mungu kwa mataifa ambao hujidhihirisha kwa njia ya Ekaristi Takatifu. Ni ishara ya shukrani kwa Mungu kwa ajili ya zawadi ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo.

Mpendwa katika somo la kwanza tunawaona wana wa Israeli chini ya mlima Sinai wakifanya agano na Mungu. Mungu anawahaidi ulinzi na usalama kama watashika amri zake. Kwa kumshukuru Mungu kwa haya yote wanashangilia na kufanya sherehe kama kielelezo cha mwitiko wao mbele ya Mungu. Musa kiongozi wao anatolea sadaka na kutengeneza altare, anachukua damu ya wanyama na kunyunyuzia altare hiyo, iliyo alama ya Mungu, na damu nyingine ananyunyizia kwenye mawe yaliyo alama na kiwakilishi cha wanafamilia ya Mungu. Watu wanahaidi kushika agano hili. Maana ya tendo hili ni kwamba Mungu na Waisraeli wanakuwa kama mtu mmoja wakiwa wameunganishwa kwa njia ya damu.

Mpendwa mwana wa Mungu, agano hili liliharibika baadaye kwa sababu ya udhaifu wa mwanadamu na hivi Mungu kwa njia ya manabii anahaidi kufanya agano jipya. Mpendwa agano jipya sasa ni kwa njia ya Ekaristi Takatifu ambapo mwanadamu mpya badala ya kunyunyiziwa damu ya wanyama anakunywa Damu, iliyo Damu ya Mkombozi. Bwana akitaka kurudia maneno ya agano la kale anasema “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu” Kumbe daima na milele mwanadamu atafanya agano hilo, mpaka Bwana atakaporudi. Kushika vema agano hili ni kupata matunda yake na namna ya kulishika vema ni kwa njia ya kuwaosha watu miguu- kumbuka Alhamis Kuu.

Mpendwa, katika somo la pili toka Barua kwa Waebrania, tunamwona Kuhani Mkuu akiingia patakatifu pa patakatifu. Pale palisadikika kuwa sehemu ambayo Mungu alikuwa akikaa. Ni katika patakatifu kuhani alinyunyizia damu ya agano kila mwaka. Mwandishi anajaribu kuleta picha ya Yesu Kristo aliye Kuhani Mkuu hasa, na anatolea damu yake mara moja bila kurudia kwa maisha yote na kwa ajili ya wote. Damu ya Bwana inabadilisha maisha ya watu, inatakasa na kiumarisha upendo.

Ni kwa njia ya Damu ya Bwana sisi tumepata ukombozi na hivi leo anatualika kufanya kama alivyofanya yeye. Kufanya kama alivyofanya yeye Kanisa huadhimisha Ekaristi Takatifu toka mawio ya jua hata machweo yake bila kukoma. Kanisa halifanyi tu adhimisho bali pia hujitahidi kukua katika kuwa huduma na chakula, ekaristia safi kwa mataifa. Katika ngazi ya mtu mmojammoja mwaliko ni uleule wa kuwa Ekaristi safi, zawadi kwa wengine katika maisha ya jumuiya na kila siku.

Katika Injili, Bwana anawatuma wanafunzi kwa mtu mmoja huko mjini ili mtu huyo akawaoneshe wapi chumba cha kulia pasaka. Chumba hiki kiko katika ghorofa na tayari kimeandaliwa! Picha ya kwanza ninayoipata ni kwamba Ekaristi Takatifu ni sakramenti, karamu kuu ya Bwana ambayo lazima kuabudiwa kwa heshima ya juu. Chumba cha juu maanake ni utukufu na heshima kwa Ekaristi Takatifu. Daima Mapadre wasisitize hilo na waamini walishike kwa mapendo ya juu kiasi kwamba Kristu atukuzwe pote na siku zote.

Sehemu ya pili ya Injili ni kuwekwa kwa Ekaristi Takatifu kama sakramenti. Anaweka sakramenti hii iwe ni alama na chimbuko la Kanisa. Ni alama na ishara ya kujitoa sadaka Yesu Kristu bila kujibakiza kwa ajili ya ulimwengu. Ni ishara ya ulinzi kwa mwanadamu atakayepokea daima Mwili na Damu ya Bwana. Ni chanzo cha familia mpya ya wanadamu ambao watakunywa kikombe kimoja na kula mwili wake, wakijitahidi kujifananisha na Bwana, wakitoa na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Damu na Mwili wa Kristu ni kwa ajili ya kuunda jumuiya na hivi ni chakula neema unganishi kwa ajili ya wote bila ubaguzi.

Mpendwa msikilizaji tunaposherehekea tunapaswa kufikiri kwa undani sana nini maana ya fumbo hili kuu na mwisho lazima, tafakari yetu imalizikie katika neno moja “PENDANENI KAMA NILIVYOWAPENDA NINYI”. Ninawatakieni furaha tele waamini wote ambao parokia zao ziko chini ya ulinzi wa Mwili na Damu Takatifu ya Yesu, nikiwakumbusha fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu hadi nitakaporudi”

Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.