2015-06-03 07:20:00

Bustani ya wito na maisha ya kipadre!


Wito na maisha ya Kipadre ni kama bustani, ambayo inaweza kutunzwa vyema lakini wakati mwingine inaweza kusahaulika. Kuna uhusiano mkubwa katika maisha na utume wa Kipadre unaofumbatwa katika huduma ya Kiinjili kwa ajili ya Familia ya Mungu. Pale ambapo Jandokasisi au Padre anapokosa mambo msingi katika ukuaji na ustawi wa maisha yake ya kiroho, hapo cheche za kuanza kumezwa na malimwengu zinaanza kujitokeza.

Huu ndio mwanzo wa kukauka na kunyauka kiroho kwa kutamani malimwengu ambayo kimsingi anapaswa kuyapatia kisogo; ni mwanzo wa kupatwa na msongo wa mawazo na upweke hasi na matokeo yake ni kuchanganyikiwa na kujutia maamuzi ya kujiunga na wito wa kipadre. Pale ambapo Padre anashindwa kusali, kutafakari na kuadhimisha barabara Mafumbo ya Kanisa, huo ni mwanzo wa kunyauka kwa maisha na utume wa Kipadre.

Kumbe, kuna haja kwa Mapadre na Majandokasisi kuchuchumilia maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu pamoja na Sakramenti za Kanisa: Ekaristi Takatifu inawakirimia chakula cha njiani; Sakramenti ya Upatanisho inawawezesha kuonja huruma na upendo wa Mungu, tayari kuwamegea waamini wanaowaendea kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Huu ni ushauri wa kina uliotolewa hivi karibuni na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati alipokuwa anazungumza na Wakleri pamoja na Majandokasisi, Jimbo kuu la Avana, Cuba.

Mapadre na Majandokasisi wanapaswa kukuza, kulea na kupalilia maisha na wito wao wa kipadre, ili kuhakikisha kwamba, ile mbegu ya imani na neema iliyopandikizwa ndani mwake inakua na kuchanua, ili hatimaye, iweze kuzaa matunda ya uadilifu na utakatifu wa maisha. Matunda ya Roho Mtakatifu katika maisha ya Mapadre ni: moyo wa ukarimu na sadaka; upendo na mshikamano wa kidugu; furaha na upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huduma ya Kiinjili ni kiini cha maisha na wito wa kipadre, kwani hii kimsingi ni hazina ambayo imefichika, inapaswa kuvumbuliwa na kufanyiwa kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu.

Kardinali Stella anawataka Mapadre na Majandokasisi kuhakikisha kwamba, wanakuza ndani mwao ari na moyo wa sadaka, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Yesu Kristo Mchungaji mwema, aliyejinyenyekesha, akawa mtii hata mauti ya Msalaba, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Maisha ya kujisadaka ni kiini cha miito mbali mbali ndani ya Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kwa Wakleri. Mapadre wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na utume wao kama njia ya kumwilisha upendo katika shughuli za kichungaji.

Kardinali Stella anabainisha kwamba, ili kuwapata Wakleri waliofundwa wakafundika, kuna haja ya kuwekeza katika majiundo makini ya Majandokasisi, kwa kukazia kwa namna ya pekee mambo makuu mawili: tasaufi ya kipadre na huduma ya kichungaji; mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika majiundo ya awali na endelevu, kwa Waseminari kutoka katika undani na ubinafsi wao, tayari kuambata tunu msingi za maisha ya Kiinjili, tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Familia ya Mungu.

Pili, Majandokasisi wanapaswa pia kuonesha ukomavu katika hija ya maisha yao kama wafuasi wa Kristo, ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Haya ni majiundo yanayofanyika kwenye taasisi za Falsafa, kwa kujipatia ujuzi na maarifa, tayari kwa ajili ya huduma ya Kiinjili. Tatu, majiundo ya Waseminari yanapata sura na mwelekeo mpya wanapokuwa katika taasisi za kitaalimungu, hapa wanapaswa kuonesha dalili za ukomavu kana kwamba, tayari wamekwisha kupata Daraja takatifu, hapa hakuna tena cha “Salia Mtume”.

Huu ni wakati wa kukuza na kuimarisha fadhila mbali mbali katika maisha ya Mseminari, kwa kutambua kwamba, wao wanapaswa kuwa ni wahudumu wa Injili, waadhimishaji na wagawaji wa Mafumbo ya Kanisa katika maisha na utume wao. Hatua ya nne anasema Kardinali Stella ni ni Daraja la Ushemasi wa mpito, mahali pa kukuza na kudumisha moyo, ari na tasaufi ya maisha na wito wa kipadre katika huduma makini kwa Familia ya Mungu.

Hii ndiyo Katekesi ya kina iliyotolewa na Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati alipokuwa anapiga mchapo na Wakleri pamoja na Majandokasisi kutoka Jimbo kuu la Avana Cuba, wakati wa hija yake ya kikazi nchini Cuba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.