2015-06-03 08:53:00

Burundi inaendelea kugeuka kuwa ni uwanja wa fujo!


Umoja wa Mataifa umetoa kiasi cha dolla za kimarekani millioni kumi na moja kama sehemu ya msaada wa awamu ya kwanza kwa ajili ya wakimbizi kutoka Burundi wanaohifadhiwa nchini Tanzania na Rwanda. Machafuko ya hali ya hewa kisiasa yamepelekea zaidi ya wananchi sabini elfu kuyakimbia makazi kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Taarifa zinaonesha kwamba, watoto wengi waliowasili Tanzania na Rwanda wanaonesha dalili za utapiamlo wa kutisha.

Katika siku za hivi karibuni, Burundi imegeuka kuwa ni uwanja wa fujo na vurugu za kisiasa ambazo zinatishia uwepo wa vita na kinzani za kikabila, hali ambayo inaweza kuitumbukiza Burundi katika maafa makubwa. Maamuzi ya Rais Pierre Nkurunziza kuwania tena mabadaraka kwa awamu ya tatu kinyume cha katiba ni chanzo cha maandamano na fukuto la machafuko ya kisiasa nchini Burundi.

Kutokana na hali ya kisiasa kuendelea kuwa tete nchini Burundi, Rais Nkurunziza amewaonya wapinzani wake kutothubutu tena kufanya jaribio la kutaka kuipindua Serikali yake, vinginevyo, watakiona cha moto! Wapinzani nao wanasema, kwa sasa wanataka kuingia tena mitaani kwa maandamano makubwa ili kumshinikiza Rais Nkurunziza kuachia ngazi, ili demokrasia ya kweli iweze kushika mkondo wake.

Na Padre Richard A, Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.