2015-06-03 15:17:00

Adhimisho la Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu mjini Roma


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, jioni majira ya saa 1. 00 Usiku, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu; sherehe ambayo kwa Makanisa mengi duniani, itaadhimishwa rasmi, Jumapili ijayo, ili kutoa nafasi kwa waamini kuweza kushiriki kwa wingi katika Ibada na maandamano ya Ekaristi Takatifu, kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake.

Mara baada ya Ibada, kutakuwepo na muda wa kuabudu Ekaristi Takatifu, kabla ya kuanza maandamano makubwa kutoka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuelekea kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu. Hapa, Baba Mtakatifu anatatoa baraka la Ekaristi Takatifu. Ibada kwa Ekaristi Takatifu, isaidie mchakato wa Unjilishaji mpya na utamadunisho, ili kweli za Kiinjili ziweze kujikita katika maisha ya watu.

Waamini waongeze bidii katika uchaji wa Mungu, kama kikolezo cha utakatifu wa maisha, tayari kuyatakatifuza malimwengu. Waamini wazamishe mahusiano yao mema kwa Yesu Kristo. Ibada kwa Ekaristi Takatifu ilete mabadiliko katika maisha ya waamini kwa kukumbatia kanuni maadili na utu wema, unaopata chimbuko lake kwa kumkaribisha Yesu mioyoni mwao, kama alivyofanya Zakayo, mtoza ushuru. Ekaristi isaidie kusumisha ari na moyo wa Kimissionari, tayari kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ekaristi Takatifu, iwe ni changamoto kwa waamini kujitahidi kumpeleka Kristo kwa jirani zao, kwa kujitahidi kuwa ni Mkate uliomegwa kwa ajili ya uhai wa ulimwengu, changamoto ya kuonesha mshikamano na wote wanaoteseka kwa baa la njaa na umaskini duniani.  Ekaristi takatifu, iwachangamotishe waamini kulinda na kutunza mazingira, ambayo kimsingi ni kazi ya Uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu kuiendeleza kwa ajili ya mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho. Maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, iwe ni kumbu kumbu endelevu ya uwepo wa Yesu Kristo miongoni mwa wafuasi wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.