2015-06-02 10:10:00

Askofu mkuu Paolo Rocco Gualtieri awekwa wakfu tayari kwenda Madagascar


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi tarehe 30 Mei 2015, katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amemweka wakfu Askofu mkuu Paolo Rocco Gualtieri aliyeteuliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Madagascar. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa Madagascar ambayo imebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na tamaduni, kuhakikisha kwamba, inalinda na kudumisha urithi huu kwa ajili ya mafao ya wengi.

Askofu mkuu Gualtieri amekumbushwa kwamba, katika maisha na utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Madagascar atakutana na Kanisa changa ambalo linaendelea kujikita katika utoaji wa huduma makini kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ni Kanisa ambalo linajibidisha kuwafunda vijana wa kizazi kipya kwa kuwapatia matumaini ya maisha bora, pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu.

Kanisa nchini Madagascar ni kielelezo cha upendo na mshikamano na waathirika wa majanga asilia na kwamba, linaendelea kujielekeza katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni Kanisa ambalo licha ya changamoto mbali mbali zilizoko nchini humo katika uwanja wa kisiasa, lakini limeendelea kuwa ni jukwaa la majadiliano ya kisiasa na kitamaduni miongoni mwa wanasiasa, ili kuimarisha amani na maridhiano kati ya watu, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kukaza kwa kusema kwamba, katika shida, migogoro na kinzani, kuna haja ya kumwilisha kweli za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kuonesha upendo wa dhati kwa Kanisa pamoja na kupokea kwa shukrani karama na mapaji mbali mbali ambalo limekirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Viongozi wa Kanisa hawana budi kujenga na kudumisha ndani mwao moyo na ari ya kuwa wachungaji wema, wanaojisadaka bila yakujibakiza kwa ajili ya mafao ya wengi.

Ibada hii imehudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa kutoka ndani na nje ya Vatican, lakini kwa namna ya pekee kabisa , Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Dominican ambalo limekuwepo hapa mjini Vatican kushiriki katika hija ya kitume inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano hapa mjini Vatican. Kardinali Parolin amemkumbusha Askofu mkuu Gualtieri kwamba, uzoefu na mang’amuzi ya huduma za kidiplomasia alizowahi kufanya sehemu mbali mbali za dunia, iwe ni chemchemi ya kutambua umoja na utoafuati unaojikita katika Kanisa la Kristo.

Mang’amuzi haya anasema Kardinali Parolin yanajikita katika furaha na machungu, lakini lengo kuu ni kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuliongoza Kanisa la Kristo, kwa kupokea na kutumia vyema utajiri na rasilimali mbali mbali zinazopatikana kwenye Makanisa mahalia. Utume huu haina budi kujikita katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu kwa kutekeleza dhama na majukumu haya kwa moyo mkuu na hali ya unyenyekevu; kwa kuwa shuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo kwa waja wake.

Mwishoni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amemkumbusha Askofu mkuu Paolo Rocco Gualtieri kwamba, Askofu, kimsingi anapaswa kuwa ni Baba mwenye hekima na busara na kamwe si mmiliki na mdhibiti wa imani ya ndugu zake katika Kristo. Uwakilishi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni huduma inayopania kujenga na kudumisha umoja, mshikamano na udugu kati ya Kanisa na Kiulimwengu na Kanisa mahalia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.