2015-06-01 07:09:00

Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ni mtaji mkubwa kwa maendeleo!


Maisha ya ndoa na familia yanayojikita katika upendo kamili kati ya Bwana na Bibi ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, kwani wanandoa kimsingi wanashiriki katika kazi ya uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi binadamu. Agano la ndoa, ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili mafao yao na kwa ajili ya kuza na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti.

Ni agano ambalo linajikita katika uaminifu na udumifu mambo msingi katika upendo unaohimizwa na Mama Kanisa kwa watoto wake. Hii ndiyo changamoto kubwa inayotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama anavyobainisha Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa linalohamasisha umoja wa Wakristo, wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kuadhimisha awamu ya pili ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia.

Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kufanya maamuzi machungu katika maisha yao kwa kuchagua na kuamua kufunga Sakramenti ya ndoa, inayodumu hadi pale kifo kitakapowatenganisha, hapa watu wanapaswa kuachana na tabia ya kubabaisha bila ya kuwa na msimamo thabiti wa maisha, kwa kutambua kwamba, uaminifu na udumifu ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.

Leo kuna watu wengi wanaosita kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuogopa kushindwa katika maisha; kwa kugubikwa na ubinafsi pamoja na uchoyo unaohofia kuharibu uhuru wa mtu. Hapa Mama Kanisa hana budi kujiwekea mikakati ya kichungaji itakayosaidia kuwahudumia waamini waliotalakiana na kuamua kuoa au kuolewa tena. Maaskofu waangalie uwezekano wa waamini hawa kuruhusiwa kushiriki katika Mafumbo ya Kanisa.

Mikakati hii iwasaidie wanandoa watarajiwa kujiandaa kikamilifu katika utume na maisha ya ndoa na familia. Matunda ya muungano kati ya bwana na bibi ni watoto, ambao wote hawa wanaunda na kujenga familia, tayari kurithisha zawadi ya uhai. Familia ina umuhimu wa pekee kwani huu ni urithi wa binadamu wote anasema Kardinali Kurt Koch. Bila familia, matumaini ya mwanadamu yako mashakani kama anavyobainisha Kardinal Walter Kasper.

Idadi ya wazee Barani Ulaya inazidi kuongezeka maradufu, lakini watoto wanaozaliwa ni wachache sana. Hii ni changamoto kubwa kwa familia nyingi Barani Ulaya. Hii ni kutokana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, kiasi kwamba, wazazi wenyewe hawana matumaini, kumbe wasingependa watoto wao baadaye kuteseka na kuhangaika. Lakini, waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kufanya maamuzi yanayowawajibisha, kwa kuwa na matumaini pamoja na ujasiri wa kurithisha zawadi ya uhai kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kizazi kijacho.

Familia nyingi Barani Ulaya zina idadi ndogo sana ya watoto, changamoto na mwaliko kwa Wakristo kuendelea kutangaza Injili ya Familia kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya imani inayomwilishwa katika matendo. Ubaridi kwa ajili ya maisha ya ndoa na familia unasababisha changamoto kubwa katika maisha ya kijamii, kiasi kwamba, leo hii familia ni kati ya taaisis zinazoshambuliwa na kukashfiwa sana.

Dhana ya ukanimungu inajionesha na kugusa pia maisha ya ndoa na familia, lakini watu wakumbuke kwamba, vistisho dhidi ya maisha ya ndoa na familia ni vitisho dhidi ya binadamu mwenyewe kama alivyosema Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa nchini Ufilippini. Uelewa sahihi wa familia, unamwezesha mwamini kutambua dhamana na wajibu wake katika jamii. Mababa wa Sinodi ya maaskofu kwa ajili ya familia wanayo dhamana kubwa mbele yao katika mchakato wa kulinda na kujenga tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; kwa kuendelea kujikita katika utangazaji wa Injili ya Ndoa na Familia.

Wanandoa wenyewe wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa uaminifu, upendo na udumifu, tayari kuwapokea, kuwatunza na kuwaelimisha watoto ambao ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Familia si kitisho kwa maisha ya mwanadamu anasema Kardinali Kurt Koch. Uhuru na uaminifu ni chanda na pete, kwani gharama ya uhuru ni kubwa kwa mtu ambaye ni mwaminifu na kwamba, uhuru ni zawadi ya uaminifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.