2015-06-01 09:23:00

Mwenyeheri Oscar Romero ni shuhuda wa majadiliano ya kiekumene, haki na amani


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, linampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuamua kumtangaza Askofu mkuu Oscar Arnulfo Romero kuwa Mwenyeheri, kiongozi aliyetoa mchango mkubwa katika utume wa Makanisa ulimwenguni, kwa kukazia ari na moyo wa kiekumene kati ya Makanisa. Dhamana hii imefanyiwa kazi na Baraza la Makanisa Ulimwenguni huko Amerika ya Kusini. Askofu mkuu Oscar Romero aliuwawa kikatili wakati alipokuwa anaadhimisha Ibada ya Misa takatifu, siku hiyo watu wengine 35 walipoteza maisha yao.

Hii ni sehemu ya barua ambayo, Dr. Olav Fyske Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni amemwandikia Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la uhamasishaji wa umoja wa Wakristo, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumtangaza Askofu mkuu Oscar Romero kuwa ni Mwenyeheri, tukio ambalo limevuta hisia kwa viongozi mbali mbali wa Kanisa na kisiasa duniani.

Kati ya mapambano ya silaha na uvunjifu wa haki msingi za binadamu nchini El Salvador, Askofu mkuu Oscar Romero, akajipambanua kuwa kweli ni kiongozi na mchungaji mwema kwa mfano wa Yesu. Kwa njia ya maisha na utume wake kama Askofu, Mwenyeheri Oscar Romero amewahudumia na kuwaonjesha upendo maskini na wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii; akawajali na kuwaonjesha huruma wale waliokuwa wanaogelea katika dimbwi la vurugu na ghasia nchini El Salvador.

Mwenyeheri Oscar Romero alikuwa ni mtu mwenye ujasiri wa ajabu na kwamba, kifo chake ni kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji si tu kwa El Salvador na Kanisa nchini humo, bali kwa Wakristo wote duniani. Kutangazwa kwake kuwa ni Mwenyeheri, kusaidie kuganga na kuponya madonda ya kihistoria hata katika majadiliano ya kiekumene. Baraza la Makanisa katika mchakato wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho, linatiwa shime na ujasiri ulioshuhudiwa na Mwenyeheri Oscar Romero.

Askofu mkuu Oscar Romero, shuhuda wa imani na mfiadini ameacha urithi mkubwa na dhamana ya majadiliano ya kiekumene katika maisha ya kijamii ukanda wa Amerika ya Kusini. Tukio la kutangazwa Askofu mkuu Oscar Romero limepongezwa na viongozi mbali mbali wa Makanisa ndani na nje ya El Salvador. Huu ni mwaliko kwa Wakristo kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Mwenyeheri Oscar Romero awe ni kikolezo cha imani, matumaini na mapendo kati ya watu; awe kweli ni Pentekoste mpya kwa Kanisa la Kristo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.