2015-06-01 07:55:00

Mahujaji katika njia ya amani wanahamasishwa kujenga misingi ya haki!


Shirika la Kimataifa la Pax Christi limehitimisha mkutano wake mkuu wa mwaka kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, likiwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete katika mapambano ya kudai misingi ya haki na amani kwa kukumbatia tofauti sanjari na kujikita katika misingi ya Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hii ndiyo dira na mwongozo wa Pax Christi katika maisha na utume wake kwa siku za usoni.

Hivi ndivyo wajumbe walivyoandika kwenye “Tamko la Bethelehemu” baada ya kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 70 tangu kuanzishwa kwake, mkutano ambao umehudhuriwa na wajumbe 150 kutoka katika nchi mbali mbali duniani. Tukio hili limeongozwa na kauli mbiu “Mahujaji katika njia ya amani”.

Shirika la Kimataifa la Pax Christi lilianzishwa kunako mwaka 1945 huko Ufaransa baada ya patashika nguo kuchanika ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Pax Christi, likaibuka kama chombo cha kutetea misingi ya haki na amani; maendeleo endelevu na mshikamano wa dhati pamoja na utunzaji bora wa mazingira, ambayo ni kazi ya uumbaji aliyokabidhiwa binadamu kuitunza na kuiendeleza kwa mafao ya kizazi cha sasa na kile kijacho.

Pax Christi ni Shirika la kimataifa ambalo linahimiza amani ilikuondokana na vita na kwamba, majadiliano katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi ni mambo msingi ili kujenga na kudumisha amani ya kweli. Hii ni sehemu ya mchakato makini katika mapambano dhidi ya umaskini, kinzani na utengano ili kuwajengea watu imani na matumaini ya maisha bora zaidi badala ya kukata tamaa na kujitumbukiza katika vita na kinzani, kwani kufanya hivi ni kuendeleza umaskini na utengano wa kijamii, sumu ya maendeleo endelevu.

Pax Christi linakazia umuhimu wa kuwekeza zaidi katika nguvu na matumaini ya vijana na kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, kama mkakati huu utafanyiwa kazi barabara, misimamo mikali ya kidini inaweza kupewa kisogo na badala yake, waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kushirikishana utajiri wa imani na mang’amuzi katika maisha yao ya kila siku. Hapa kuna haja ya kujielekeza katika mchakato wa majadiliano na ushirikiano kati ya vijana wa kizazi kipya na “vijana wa zamani”.

Kuwepo na ushirikiano kati ya vijana na viongozi bila kubeza mchango na dhamana ya wanawake katika kujenga na kudumisha amani duniani. Kutokana na changamoto hii, Shirika la Pax Christi katika kipindi cha miaka mitano ijayo, itaendelea kuwekeza katika majiundo makini kwa wanawake, ili waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki na amani.

Wanawake wawe mstari wa mbele kutetea haki msingi za wanawake sanjari na kuendelea kuwa waaminifu katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Pax Christi inapania pia kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kiislam, ili kudumisha amani, ustawi na maendeleo ya wengi, kwa kutambua kwamba, dini zina mchango mkubwa katika kudumisha amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.