2015-06-01 07:34:00

Kanisa litaendelea kuhamasisha majadiliano ya kidini ili kudumisha amani


Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini, hivi karibuni amefanya hija ya kichungaji nchini Marekani na hivyo kupata fursa ya kushiriki katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 ya Waraka wa Kitume uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali, hususan waamini wa dini ya Kiislam na Kiyahudi.

Akiwa nchini Marekani, Kardinali Tauran amekazia dhamana ya Kanisa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, wakati alipofungua kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Chuo kikuu cha George town cha Marekani kwa kushirikiana na Mtandao wa Kanisa wa masuala ya uchunguzi na tafiti za kimataifa, Chuo kikuu cha Maryland pamoja na Jimbo kuu la Washington, DC.  

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini litaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki duniani ili kuimarisha mchakato wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani, kwa lengo la kujenga na kudumisha maridhiano kati ya watu, amani, ustawi na maendeleo ya wote. Kardinali Tauran ameonesha pia utashi wa Baraza lake wa kuendelea kushirikiana na waamini wa dini ya Kihindi na Wajains kama ilivyobainishwa kwenye mikutano ya pamoja na waamini hawa iliyofanyika kunako mwaka 2011 na mwaka 2013.

Lengo kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko ni kujenga urafiki, udugu na mshikamano kati ya watu wa dini mbali mbali ili kudumisha amani na maridhiano. Majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Kihindu bado yanasuasua kutokana na baadhi ya waamini kuonesha misimamo mikali ya kidini. Kanisa bado halijakata tamaa, litaendelea kuhamasisha majadiliano haya kwa ajili ya mafao ya wengi.

Majadiliano ya kidini na waamini wa dini ya Jaini yanaendelea vyema na kwa mara ya kwanza kwa mwaka huu wamejadili kuhusu huruma na majadiliano; tema iliyochangiwa na wataalam mbali mbali kutoka katika dini hizi mbili. Kardinali Tauran anaridhika sana na mafanikio yaliyopatikana kutokana na ziara hii ya kichungaji nchini Marekani.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba, majadiliano ya kidini ni nyenzo muhimu sana katika mchakato wa Uinjilishaji mpya; mshikamano na umoja, udugu na mapendo kati ya watu; tayari kujikita katika mchakato wa kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na furaha duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.