2015-06-01 15:26:00

Jaribio la kutaka kumuua Askofu mkuu Ngoyagoye wa Bujumbura lashindikana!


Habari kutoka Bujumbura, Burundi zinabainisha kwamba, jaribio la kutaka kumuua Askofu mkuu Evariste Ngoyagoye wa Jimbo kuu la Bujumbura, Burundi limeshindikana kutoka na ulinzi mkali uliotolewa na Vijana Wakatoliki Jimboni humo. Jaribio la mauaji haya lilikuwa litekelezwe wakati wa maandamano ya kufunga Mwezi Mei, uliotengwa na Mama Kanisa kwa ajili ya Ibada na heshima kwa Bikira Maria.

Baraza la Maaskofu Katoliki Burundi kwa nyakati tofauti limeonesha msimamo wake kwa kupinga kitendo cha Rais Pierre Nkurunziza kuwania tena madaraka kwa awamu ya tatu kinyume cha Katiba na Makubaliano ya Arusha, Tanzania yaliyosaidia kurejesha amani, utulivu na maridhiano nchini Burundi baada ya kipindi kirefu cha kinzani na misigano ya kisiasa. Mwanzoni mwa ghasia na vurugu, Maaskofu waliitaka Serikali kuhailisha uchaguzi mkuu kwani mazingira yaliyokuwepo yasingeweza kuwahakikishia wananchi usalama wa maisha yao. Pili, Maaskofu kwa kuonesha kutoridhika na mchakato wa uchaguzi mkuu, waliojitoa katika jopo la kusimamia uchaguzi mkuu.

Habari zaidi zinabainisha kwamba, viongozi wa upinzani hawakuridhika na maamuzi yaliyofikiwa na Marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kati waliokuwa wanakutana Jijini Dar es Salaam, mwishoni mwa juma. Viongozi hawa wameonesha udhaifu mkubwa katika maamuzi yao kwa kutaka uchaguzi mkuu uhailishwe kwa muda wa mwezi mmoja na nusu kuanzia sasa.

Uhuru wa vyombo vya habari na Rais Pierre Nkurunziza kushiriki katika uchaguzi mkuu kinyume cha Katiba, hayakujadiliwa. Kutokana na ukweli huu, viongozi wa upinzani wanasema, wanarejea tena mitaani kwa maandamano makubwa ili kupinga wazo la Rais Nkurunziza kuwania madaraka kinyume cha katiba ya nchi. Wachunguzi wa mambo wanasema kwamba, hali ya kisiasa na kiulinzi ni tete sana nchini Burundi na kwamba, hofu imetanda miongoni mwa wananchi kwani hawajui hatima ya malumbano haya ya kisiasa, kwani Waswahili husema, wanapopambana Tembo wawili zinazoumia ni nyasi”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.