2015-06-01 08:37:00

Fumbo la Utatu Mtakatifu ni kielelezo cha umoja, upendo na ukarimu wa kweli


Kanisa katika maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu linaungama Mungu mmoja katika Nafsi tatu: Yaani Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wanaoungana katika umoja na upendo. Yesu Kristo ndiye aliyewafunulia waja wake Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baada ya ufufuko, akawatuma Mitume kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa kuwafundisha na kuwabatiza watu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Hii ni amri ambayo Yesu mwenyewe amelikabidhi Kanisa kwa nyakati zote na kurithi kutoka kwa Mitume dhamana hii ya kimissionari inayopaswa kutekelezwa pia na kila Mkristo, kwani kwa nguvu ya Sakramenti ya Ubatizo, wote wanafanyika kuwa ni sehemu ya Jumuiya yake. Maadhimisho ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ni changamoto ya kujenga na kudumisha umoja na mshikamano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, kwa kuiga mfano wa Fumbo la Utatu Mtakatifu. Watu watambue kwamba, wanategemeana na kukamilishana, mwaliko wa kupokea na kushuhudia uzuri wa Injili kwa pamoja.

Baba Mtakatifu Francisko ameyasema haya, Jumapili tarehe 31 Mei 2015 wakati wa maadhimisho ya Sherehe ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwilisha upendo kwa watu wote; kwa kushirikishana furaha na mahangaiko; kwa kujifunza kuomba na kutoa msamaha; kwa  kuthamini karama mbali mbali ambazo Mwenyezi Mungu amewakirimia wafuasi wake, daima wakijiweka chini ya viongozi wao. Wakristo wamepewa dhamana ya kujenga Jumuiya ya Kikanisa kama familia yenye uwezo wa kutafakari utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na kuzama katika utume wa Uinjilishaji unaojikita si tu katika maneno, bali katika matendo kwa kuonesha nguvu ya upendo wa Mungu anayeishi ndani mwao.

Baba Mtakatifu anabainisha  kwamba, Fumbo la Utatu Mtakatifu ni hatima ya maisha ya waamini mara baada ya kuhitimisha hija ya maisha yao hapa duniani. Hija ya maisha ya Kikristo inajikita katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Roho Mtakatifu anawaongoza waamini kufahamu ukweli wote wa mafundisho ya Yesu pamoja na kuwakumbusha yale ambayo Yesu amewafundisha. Yesu alikuja ulimwenguni ili kuwawezesha watu kumtambua Mwenyezi Mungu na kuwaongoza ili waweze kumwendea na kujipatanisha naye. Maisha yote ya Kikristo yanafumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini  kuwa na mtazamo mpana zaidi kwa kukumbuka hatima ya maisha yao, ni utukufu gani ambao wanapenda kushiriki, wanapofanya kazi, wanapopambana, wanapoteseka; katika yote haya wanatamani kupata tuzo gani?

Mwishoni mwa Mwezi Mei, ambao umetengwa na Mama Kanisa, Baba Mtakatifu anapenda kuwaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria aliyebahatika kulifahamu, kulipenda na kuliabudu Fumbo la Utatu Mtakatifu. Awasaidie waamini kupokea uwepo endelevu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu katika matukio mbali mbali ya maisha kwa moyo wote, huku wakitembea ili kukutana na Fumbo la Utatu Mtakatifu, hatima ya maisha yao.

Waamini wamwombe Bikira Maria alisaidie Kanisa kuwa ni Fumbo la umoja na Jumuiya yenye ukarimu, mahali ambapo kila mtu, lakini zaidi maskini na wale wanaosukumizwa mpembezoni mwa jamii wanaweza kuonja ukarimu na kujisikia kuwa kweli ni watoto wa Mungu, anayewataka na kuwapenda.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, uliokuwa umesheheni umati mkubwa watu kutoka katika lugha, jamaa na kabila, Baba Mtakatifu aliwakumbusha waamini kwamba, Siku ya Jumapili, nchini Ufaransa, Mama Kanisa amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Louis-Edouard Cestac kuwa Mwenyeheri. Padre Cestac alikuwa ni muasisi wa Shirika la Watawa la Wahudumu wa Bikira Maria. Ushuhuda wake wa upendo kwa Mungu, jirani na Kanisa uwe ni chachu ya kuishi kwa furaha Injili ya Upendo.

Baba Mtakatifu amewakumbusha waamini kwamba, Alhamisi ijayo, anatarajia kuadhimisha Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jimbo kuu la Roma; Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na kufanya maandamano makubwa, ushuhuda wa uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kushiriki kikamilifu katika tukio hili la kiimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.