2015-06-01 12:07:00

Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Justin, shahidi inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe Mosi Juni, amesema kwamba, mara nyingi waamini wamemkataa Yesu Kristo kwa kushindwa kulikumbatia Fumbo la Msalaba, linaloonesha huruma na upendo wa Mungu, kama walivyofanya wale wafanyakazi wa shamba waliowatesa na kuwauwa wajumbe wa Mungu.

Yesu Kristo ndiye lile Jiwe walilolikataa waashi sasa limekuwa ni jiwe kuu la pembeni na kwamba, Fumbo la Msalaba ni chemchemi ya historia ya ukombozi inayomjengea mwamini matumaini yanayobubujika kutoka katika upendo unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Kwa wengi Msalaba ni kielelezo cha kushindwa na wafanyakazi wakatili katika shamba la Mzabibu ni kielelezo cha kushindwa kwa ndoto ya Mungu kwa watu wake. Ni katika mauti haya, maisha mapya yanapata chimbuko lake.

Mwenyezi Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu aliwatuma Manabii na wajumbe mbali mbali ili kuwatangazia watu Habari Njema, lakini hawakuwasikiliza na matokeo yake, wakauwawa kikatili kama ilivyokuwa kwa Yesu Kristo, ambaye sasa ni Jiwe kuu la pembeni. Hii ndiyo ndoto ya Mungu inayojikita katika upendo, lakini mwishoni inaonekana kana kwamba imeshindwa, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, mwanadamu amekombolewa kutoka katika dimbwi la dhambi la mauti.

Baba Mtakatifu anasema hapa ni mwanzo wa mabadiliko katika historia ya ukombozi, Jiwe lile walilolikataa waashi sasa linakuwa ni jiwe kuu la pembeni, ajabu machoni pa mataifa. Mwenyezi Mungu anasikitika kuona maasi yanayofanywa na watu wake, lakini bado anawapatia nafasi ya kutubu na kuongoka. Fumbo la Msalaba ni kashfa kwa wasioamini, lakini ni chemchemi ya upendo, mwaliko kwa waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuona ni mara ngapi wamewafukuzia mbali Manabii na wajumbe waliotumwa na Mungu kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Hapa wamemfukuza na kumkashfu Yesu wakitaka ajiokoe na kushuka Msalabani.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Fumbo la Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wake. Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu amekuwa ni jiwe kuu la pembeni na chemchemi ya wokovu kwa watu wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.