2015-06-01 08:08:00

Changamoto katika maisha na utume wa Kanisa, Jamhuri ya Wadominican


Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Dominican linafanya hija ya kitume mjini Vatican kwa kukutana, kusali na kushirikishana maisha na utume wa Kanisa mahali na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake. Kanisa nchini humo limeendelea kuwa kweli ni sauti ya kinabii katika maisha na utume wake, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Ni Kanisa ambalo limeendelea kumwilisha Injili na Mafundisho Jamii Kanisa katika vipaumbele vya maisha ya mwanadamu, kwa kukazia kanuni maadili, utu wema na mafao ya wengi katika maisha ya hadhara.

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Dominican limezikabili changamoto za kijamii kwa kuzingatia misingi ya ukweli, uwazi na majadiliano, licha ya changamoto nyingi zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa wanandoa na familia. Baada ya wananchi kukumbatia kwa miaka mingi Injili ya Uhai, kwa sasa wanakabiliwa na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba. Familia nyingi nchini humo zinaendeshwa kwa nguvu ya wanawake na athari zake zinajionesha kwa namna ya pekee katika malezi na makuzi ya watoto.

Takwimu zinaoneshwa kwamba, asilimia 40 ya wananchi wote wa Jamhuri ya Watu wa Dominican wanakabiliwa na umaskini, magonjwa na ujinga. Kuna idadi kubwa ya wananchi ambao bado hawana fursa za ajira na wengine wanaendelea kufanyishwa kazi za suluba kwa mshahara kidogo. Usalama wa raia na mali zao uko mashakani kutokana na kuongezeka kwa wimbi la biashara haramu ya dawa za kulevya na michezo ya kamali inayowadanganya watu kwamba wanaweza kupata mafanikio ya maisha kwa njia ya mkato.

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Dominican linasema kwamba, kuna changamoto kubwa wanazokabiliana nazo katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; uharibifu wa mazingira na pengo kubwa kati ya maskini na matajiri, hali ambayo inaendelea kujenga wasi wasi mkubwa kati ya wananchi. Kuna idadi kubwa ya wahamiaji kutoka Haiti wanaotafuta hifadhi ya kisiasa na kijamii. Mazingira yote haya ni changamoto kubwa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Tabia ya watu kukengeuka, ubinafsi pamoja na kupenda mno starehe na anasa pasi na kufanya kazi halali ni mambo ambayo yanalitendea pia Kanisa katika maisha na utume wake. Kanisa linaendelea kujikita katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya ushuhuda wa maisha, ilikujenga umoja na udugu pamoja na kuendelea kumwilisha imani katika matendo kadiri ya mikakati ya shughuli za kichungaji zinazopaswa kuboreshwa na kuimarishwa zaidi.

Maaskofu wanakiri kwamba, kutokana na ukosefu wa rasilimali watu, fedha na vitu, inakuwa ni vigumu kuweza kutekeleza sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ambayo imeamriwa na Familia ya Mungu nchini Jamhuri ya Watu wa Dominican. Majiundo makini na endelevu ya mihimili ya Uinjilishaji bado yanakwama licha ya uwepo wa utashi wa kutaka kutekeleza mambo yote haya. Maaskofu wanakiri kwamba, kuna ongezeko kubwa la idadi ya miito ya Kipadre na kitawa nchini humo na kwamba, wanaendelea kuhamasisha Mashirika ya Kimataifa kujitamadunisha, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Maaskofu wanasema, changamoto nyingine wanayokabiliana nayo ni kutaka kushiriki kikamilifu katika vyombo vya habari, ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwa watu wake pamoja na kusaidia kueneza Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa umati mkubwa zaidi wa watu. Maaskofu wanataka kujenga na kukuza majadiliano ya kina na vijana wa kizazi kipya, ili kuwashirikisha maisha na utume wa Kanisa, tayari hata wao kuwatangazia vijana wenzao Injili ya Furaha.

Kanisa linaendelea kujipambanua kwa njia ya huduma makini katika sekta ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Ni kimbilio na msaada kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea utu, heshima na mafao ya wengi na kwamba, Kanisa kweli ni chachu ya maendeleo endelevu nchini Dominican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.