2015-05-30 16:36:00

Sayansi iwe ni kwa ajili ya huduma ya mwanadamu na wala si kinyume chake!


Huduma kwa ajili ya binadamu ni jambo ambalo linapaswa kupewa kipaumbele cha pekee na kwamba, kulinda na kudumisha uhai wa binadamu ni dhamana nyeti hususan katika ulimwengu mamboleo usioguswa na mahangaiko ya wengine. Vyama vya sayansi na maisha ni vyombo vinavyodumisha maisha. Hii ni changamoto kubwa kwa wanachama wa vyama hivi katika uhalisia wa maisha, ili kukuza na kujenga usawa ambao unaeneza pia joto la maisha ya binadamu.

Huu ni mchakato unaowapatia nafasi ya kutoka kimasomaso ili kukutana na hatimaye kuwainua wale wanaoteseka, kwa kutambua kwamba, kiini cha maisha na utume wao ni Yesu Kristo mwenyewe, changamoto ya kuwa na mwelekeo mpana katika maisha ya binadamu. Hii ni hotuba ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 30 Mei 2015 wakati alipokuwa anazungumza na washiriki wa mkutano ulioandaliwa na Chama cha Sayansi na Maisha.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, upendo wa Kristo unawawajibisha kuwa ni wahudumu wa binadamu wote hasa wadogo na wazee, ambao haki yao ya maisha inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee kwa kutambua kwamba, maisha ya mwanadami ni kiini cha utume wa chama chao cha Kisayansi kinachowasindikiza watu katika hija ya maisha yao, kwa kutambua na kuthamini muujiza wa maisha na uzuri wake.

Kwa njia hii, Yesu ambaye ni mwanga wa binadamu na ulimwengu anaiangazia njia yao ili kweli sayansi itambue kwamba ni chombo cha kuhudumia maisha. Kinyume chake anasema Baba Mtakatifu ni sayansi kushindwa kuwa karibu na maisha ya binadamu inadumaa. Hii ni changamoto na mwaliko wa kusimama kidete kudumisha utu wa kila mwanadamu, ili sayansi iweze kuwa ni kwa ajili ya huduma ya binadamu na wala si binadamu kwa ajili ya huduma ya sayansi.

Baba Mtakatifu anabainisha kwamba, tafakari za kisayansi zinatumia lensi inayokuza na kupembua kwa kina na mapana mambo maalum. Lakini, Kanisa linasema kwamba, Jamii inapaswa kutambua haki ya maisha tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwa kuzingatia muda unaounganisha mwanzo wa maisha na hitimisho lake. Maisha kwanza kabisa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayoibua matumaini kwa siku za usoni ikiwa kama inamwilishwa katika mahusiano ya kifamilia na kijamii, kwa kuwa na mwelekeo mpya.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, maendeleo na ustaarabu wa jamii yoyote ile unapimwa kutokana na uwezo wake wa kulinda maisha, hususan katika hatua tete, kuliko hata na maendeleo yanayoweza kujionesha katika vifaa vya teknolojia. Utoaji mimba ni kati ya majanga yanayotishia maisha ya mwanadamu; kama inavyojionesha kwa wahamiaji na wakimbizi kufamaji kwenye Bahari ya Mediterrania pasi na msaada; wafanyakazi wanaopoteza maisha yao kutokana na ukosefu wa sera na mikakati bora ya ulinzi na usalama kazini. Tatizo la utapiamlo ni janga ambalo linaendelea kutishia maisha ya binadamu, bila kusahau vitendo vya kigaidi, vita, uhalifu pamoja na kifo laini. Kupenda maisha ni mchakato unaojikita katika huduma kwa wengine, kwa kuwatakia mema, kuheshimu na kuthamini utu wao kama binadamu.

Baba Mtakatifu anawataka wajumbe wa chama cha sayansi na maisha kuhamasisha tena utamaduni wa maisha, kwa kuimarisha mtandao wa matumaini, amani, huruma, umoja na mshikamano wa dhati. Kamwe wasiogope kuanzisha majadiliano makini na ulimwengu wa sayansi bila kuwasahau hata wasioamini, lakini kutoka katika undani wa mioyo yao wanathamini Fumbo la maisha ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.