2015-05-30 17:18:00

Mabadiliko yaliyofanywa na Papa katika Mfuko wa Pensheni wa Vatican


Baba Mtakatifu Francisko, tarehe 29 Mei 2015 amechapisha Barua ya Kitume inayoonesha nia yake ya kufanya mabadiliko makubwa katika Katiba ya Mfuko wa Pensheni wa Vatican. Mabadiliko haya yanagusa kwa namna ya pekee muundo ambao Rais wake atateuliwa na Baba Mtakatifu na kwamba, kuanzia sasa si lazima awe Kardinali kwani hata mwamini mlei anaweza kuteuliwa kutekeza dhamana hii. Baraza la Mfuko wa Pensheni wa Vatican, limeongezewa wataalam wanne kutoka nje ili kuweza kuratibu shughuli za Mfuko huu kwa kwa weledi, tija na ufanisi mkuu, anasema Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican.

Mabadiliko haya yanaanza mara moja kwa kuzingatia sheria na kanuni ambazo zimefafanuliwa na kupitishwa na Vatican katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni. Mabadiliko haya yamo kwenye Katiba ya Baraza la Kipapa la uchumi pamoja na Sekretarieti ya uchumi yanaosimamia na kudhibiti mwenendo wa Mfuko wa Pensheni wa Vatican. Mabadiliko haya anasema Padre Lombardi yanagusa muundo wa uongozi tu lakini kanuni na sheria za pensheni ya wafanyakazi wa Vatican zinabaki kama zilivyo kadiri ya sheria ya sasa. Mabadiliko yanajikita katika uongozi wa wale wanaopewa dhamana ya kusimamia na kuratibu Mfuko wa Pensheni wa Vatican.

Tangu sasa Rais wa Mfuko wa Pensheni wa Vatican anaweza kuwa mwamini mlei anayeteuliwa na Baba Mtakatifu kuongoza katika kipindi cha miaka mitano. Baba Mtakatifu atapelekewa walau majina ya watu watatu na kati ya hao anaweza kumchagua kiongozi mmoja atakayesimamia Mfuko wa Pensheni. Dhamana hii inatekelezwa na Baraza la Kipapa la uchumi kwa kushirikiana na Sekretarieti ya uchumi mjini Vatican. Hawa ni watu wanaopaswa kuwa na sifa na viwango vinavyotakiwa katika utekelezaji wa dhamana hii nyeti kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wafanyakazi wa Vatican.

Padre Lombardi anasema, mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Katiba ya Mfuko wa Pensheni wa Vatican ni kuingiza katika Baraza la uongozi wa Mfuko wa Pensheni wataalam wanne kutoka nje. Ni watu watakaoteuliwa kutoka katika mataifa mbali mbali kutokana na ujuzi, maarifa, uzoefu na weledi wao katika masuala ya Bima, Pensheni na Akiba. Ni watu ambao watasaidia kudumisha misingi ya ukweli, uwazi na ufanisi. Wajumbe wa ndani ni wale wanaotoka katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Tume ya mji wa Vatican, Mfuko wa Pensheni wa Vatican na Kiwanda cha Mtakatifu Petro. Hapa pia kuna wawakilishi wawili kutoka kwa wanachama wa Mfuko wa Pensheni wa Vatican, wanaoteuliwa na Katibu mkuu wa Vatican.

Padre Lombardi anaendelea kufafanua kwamba, mchakato wa kuratibu na kusimamia Mfuko wa Pensheni wa Vatican unaendelea kama ulivyo na kwamba, masuala ya vitega uchumi ni dhamana inayotekelezwa na Baraza la uongozi. Mfuko huu umeingizwa katika masuala ya fedha yanayosimamiwa na Baraza la Kipapa la Uchumi na Sekretarieti ya Uchumi, kila taasisi ikitekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya Sheria na Katiba. Mfuko unadhibitiwa pia na watu kutoka nje watakaoteuliwa na Baraza la Kipapa la Uchumi kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Uchumi. Kimsingi anasema Padre Federico Lombardi haya ndiyo mabadiliko makubwa yanayofanyiwa kazi kadiri ya mwongozo wa Baba Mtakatifu Francisko.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.