2015-05-30 17:06:00

Hakuna majibu ya mkato katika Fumbo la mahangaiko na mateso ya binadamu!


Fumbo la Utatu Mtakatifu, Fumbo la Msalaba linaloonesha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; Fumbo la Ekaristi Takatifu ni kielelezo cha uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa watu wake na kwamba, mateso na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia kama vile watoto wadogo yataendelea kubaki kuwa ni sehemu ya mafumbo katika maisha ya mwanadamu. Hakuna akili ya binadamu inayoweza kufafanua kwa kina na mapana Mafumbo haya kwani yanapita uwezo na uelewa wa mwanadamu.

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kuzungumza na watoto wagonja, Ijumaa, tarehe 29 Mei 2015 kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko hapa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema anapoona mateso na mahangaiko ya watoto sehemu mbali mbali za dunia, anakumbuka kwa namna ya pekee, Fumbo la Msalaba wa Yesu pale Bikira Maria anapomwangalia Mwanaye akiwa ameenea madonda mwili mzima na kutokwa jasho la damu, akamkumbatia na kuyahifadhi yote moyoni mwake kama alivyokuwa ameambiwa tangu mwanzo alipopashwa habari ya kuzaliwa kwa Yesu.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, watoto wanapoanza kupata umri wa kudadisi mambo wanauliza maswali ambayo wakati mwingine hayana majibu kwani yanaendelea kubaki kuwa ni fumbo katika maisha ya mwanadamu. Wakati mwingine hawataweza kupata majibu muafaka wa maswali na udadisi wao, lakini wanapaswa kuendelea kujadiliana na Mwenyezi Mungu, ingawa Mwenyezi Mungu atawaangalia kwa huruma na mapendo.

Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwasifu wazazi na walezi ambayo wamethubutu katika shida na mahangaiko yao ya ndani kusimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya maisha badala ya kukumbatia utamaduni wa kifo unaojikita katika sera za utoaji mimba. Hawa ni wazazi wanaonesha ujasiri wa kutetea Injili ya Uhai. Matatizo na changamoto za maisha, haziwezi kupatiwa ufumbuzi kwa njia ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu anasema kwamba, anawasindikiza katika hija ya maisha yao ya kila siku yanayoonesha ujasiri unaoangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo kutoka kwa Mungu Baba Muumbaji, Mungu Mwana Mkombozi, Mungu Roho Mtakatifu mfariji.

Utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine unasababisha mateso makali moyoni. Baba Mtakatifu anapenda kuwapongeza na kuwatia moyo watoto wote wanaoteseka kwa sababu mbali mbali kwani wao, kweli ni mashujaa wa maisha yanaofumbatwa na upendo kutoka kwa wazazi wao. Katika mateso na mahangaiko ya binadamu, huruma na upendo wa Mungu ndiyo majibu muafaka, kwani haya ni mafumbo katika hija ya maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu ndiye anayeweza kuwafariji watu katika mateso na mahangaiko yao ya ndani, wengine wanapaswa kuwasindikiza kwa sala. Katika shida na mahangaiko yao, wawe wepesi kumkimbilia Mungu na kuomba huruma na msaada wake.

Watoto kwa upande wao, wanasema, wamebahatika kwa namna ya pekee kabisa kuonana na Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya pili. Katika kipindi cha miaka miwili, wameweza kupata nguvu ya kusoma na kujifunza kwa bidii na kwamba, wanapomwona kwenye Televisheni akiwabusu watoto wadogo, wanajisemea mioyoni mwao kwamba, walibahatika kuzungumza uso kwa uso na Baba Mtakatifu, tukio ambalo kamwe haliwezi kufutika machoni na mioyoni mwao.

Watoto wanampongeza Baba Mtakatifu kwa kutoa kipaumbele cha pekee ili kukutana na watu kutoka sehemu mbali mbali bila hata ya kujibakiza, kama amabvyo amewapatia upendeleo watoto wagonjwa ambao wamemtembelea mjini Vatican. Watoto hao wamemkumbatia, tendo ambalo pengine kutokana na magonjwa yao, ndugu na jamaa zao wanashindwa kuwapatia.

Wazazi wa watoto hao kwa upande wao, wanashuhudia kwamba, walionana na kuanza kupendana kwa mara ya kwanza wakati walipokuwa wanawahudumiwa watoto wagonjwa waliokuwa wanafanya hija kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lolero, hapo ndipo walipogundua Fumbo la mateso na mahangaiko ya binadamu. Wakapata shauku ya kujenga Familia inayozungukwa na Fumbo la Msalaba, huku wakionesha matumaini ya kujiachilia mikononi mwa Mungu.

Yasinta na Fabrizio waliopendana tangu mwaka 1999, baada ya safari ndefu ya uchumba, wakaamua kufunga ndoa kunako mwaka 2010; walibahatika kupata mtoto wa kwanza, lakini akafariki dunia; mtoto wa pili akagundulika kuwa na matatizo makubwa mwilini mwake hata kabla ya kuzaliwa, wakashauriwa na madaktari kutoa mimba, lakini wao wakakataa na kujiachilia mikononi mwa huruma na upendo wa Mungu.

Tarehe 11 Julai 2014 akazaliwa Andrea Maria, lakini ilimbidi kubaki akihudumiwa Hospitalini kwa muda mrefu na baadaye akaruhusiwa kurejea nyumbani. Hali yake ya afya bado ni mbaya, lakini anaendelea kuwa ni chemchemi ya matumaini ya huruma ya Mungu. Watoto wagonjwa ni kielelezo cha Fumbo la Upendo wa Mungu kwa familia zao. Leo hii fumbo la mateso na mahangaiko halina tena nafasi katika walimwengu, kiasi cha kusahau kwamba, maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.