2015-05-30 16:21:00

Changamoto zinazomkabili Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria wakati huu!


Baada ya kupita takribani miaka thelathini tangu Rais Muhammadu Buhari alipoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi nchini Nigeria, Ijumaa tarehe 29 Mei 2015 amekula tena kiapo cha kuwaongoza wananchi wa Nigeria kwa kulinda Katiba na kudumisha umoja wa kitaifa. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi wa Serikali kutoka ndani na nje ya Afrika.

Rais Buhari anaingia madarakani baada ya kumbwaga Rais mstaafu Goodluck Jonathan, kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwishoni mwa Mwezi Machi, 2015. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Nigeria, kiongozi wa upinzani kumshinda Rais aliyekuwa madarakani. Rais Buhari, mbele yake kuna changamoto kubwa zinazomkabili kwa sasa. Anaingia madarakani wakati Nigeria ikiwa imesambaratika kutoka na udini, umajimbo na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha Boko Haram. Saratani ya rushwa imeenea katika sekta mbali mbali za maisha nchini humo.

Kuna idadi kubwa ya watu wasiokuwa na makazi na wakimbizi ambao bado wako nje ya Nigeria wakihofia usalama wa maisha na mali zao. Takwimu zinaonesha kwamba, Boko Haram imesababisha mauaji ya watu zaidi ya elfu kumi na tano na wengine millioni moja na nusu hawana makazi maalum. Kuapishwa kwa Rais Muhammadu Buhari kunafungua ukurasa mpya wa matumaini yanayojikita katika mabadiliko, kauli mbiu iliyoongoza kampeni za uchanguzi mkuu nchini Nigeria.

Kardinali John Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, umefika wakati kwa viongozi wa kisiasa nchini Nigeria kutekeleza kwa vitendo ahadi walizotoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu nchini humo. Wananchi wanataka kuona mabadiliko ya kweli yatakayowawezesha kuwa na uhakika wa usalama wa maisha na mali zao. Kuona saratani ya rushwa na ufisadi ikishughulikiwa kikamilifu na wahusika kufikishwa kwenye mkondo wa sheria ili sheria ifanye kazi yake, kuliko ilivyokuwa kwa siku za nyuma, mafisadi na wala rushwa waliendelea kutanua na kuneemeka kwani walikuwa na jeuri ya fedha na uchumi, wakaogopwa kama ugonjwa wa “Ebola”.

Kardinali Onaiyekan anafafanua kwamba, Nigeria kwa sasa imegawanyika sana kutokana na udini na umajimbo; mambo ambayo hayana tija wala mashiko kwa ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Rais Buhari anapaswa kutoa kipaumbele cha pekee katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa sanjari na kukoleza maridhiano kati ya wananchi wa Nigeria, ili misingi ya haki, amani na upendo viweze kushamiri tena katika mioyo ya watu.

Kardinali Onaiyekan anakaza kusema, rushwa na ufisadi vimeota sugu nchini Nigeria kutokana na Katiba ya nchi kumpatia madaraka makubwa Rais, kiasi kwamba, wakati mwingine madaraka haya yametumiwa vibaya kwa ajili ya mafao ya watu binafsi. Changamoto kubwa kwa sasa ni kuanza mchakato wa mabadiliko ya Katiba itakayokuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto ambazo zinaendelea kujitokeza nchini Nigeria. Utawala bora unaozingatia misingi ya ukweli na uwazi, sheria na mafao ya wengi ni muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya wengi nchini Nigeria.

Kuna umati mkubwa wa wananchi wa Nigeria ambao walilazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Serikali haina budi kuwahakikishia usalama, ili waweze kurudi na kuendelea na maisha yao kama kawaida. Kuna makundi makubwa ya wananchi ambayo yamekimbilia mijini ili kupata hifadhi kwa ndugu na jamaa zao. Kumbe, Serikali haina budi kudhibiti vitendo vya kigaidi ili watu waweze kuendelea na maisha yao.

Rais Buhari amechaguliwa na wananchi wote wa Nigeria, jambo la msingi hapa ni kuhakikisha kwamba, wananchi wanajenga na kudumisha utamaduni wa maridhiano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana, daima wakishikamana kwa ajili ya mafao na ustawi wa wengi. Haya ndiyo matumaini ya Kanisa na wapenda amani na maendeleo nchini Nigeria. Dhana ya kuendekeza udini ni kutaka kulitumbukiza taifa katika maafa na majanga makubwa.

Kardinali Onaiyekani anasema matumaini yake yako kwa Mwenyezi Mungu aliyeumbwa mbingu na dunia. Ni matumaini yake kwamba, Mwenyezi Mungu atawaongoza wakuu wa nchi ili waweze kutenda mambo kwa haki na kwamba, wale wote wanaowazunguka ili kuwapatia ushauri wafanye hivyo daima kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya wengi badala ya kujitafuta wao wenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.