2015-05-30 17:37:00

Akina Mama simameni kidete kupokea, kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa Jumapili tarehe 31 Mei 2015 linaadhimisha Siku ya Mama Kitaifa kwa kuwataka akina mama kusimama kidete ili kupokea zawadi ya maisha, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya Uhai. Tukio hili linavishirikisha vyama mbali mbali vya kitume ndani ya Kanisa Katoliki vinavyohamasishwa kutoka kifua mbele kutangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini.

Siku ya Mama Kitaifa ni fursa kwa waamini kushuhudia ukuu wa maisha ya binadamu ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayopaswa kupokewa kwa upendo na ujasiri mkuu, tangu pale mtoto anapotungwa mimba hadi mauti inapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu. Siku kuu hii inaadhimishwa kwa njia ya mikesha ya sala na tafakari ya kina kuhusu Injili ya Uhai na kwamba, sadaka na michango mbali mbali itakayokusanywa kutoka kwa waamini itapelekwa kwenye vituo vinavyotoa msaada kwa wanawake wajawazito wenye matatizo mbali mbali.

Itambukwa kwamba, kunako mwaka  1995 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II alichapisha Waraka wa Kitume, Injili ya Uhai, “Evangelium Vitae”, iliyowataka Maaskofu sehemu mbali mbali za dunia, kuhakikisha kwamba, walau katika kipindi cha mwaka wanasali na kutafakari kuhusu ukuu wa Injili ya Uhai, ili kuhamasisha utambuzi na changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kutangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waamini wanahamasishwa kuheshimu zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa kutambua umuhimu wa changamoto hii, likaamua kuadhimisha Siku ya Injili ya Uhai sanjari na Siku ya Mama Kitaifa, inayoadhimishwa kila mwaka, Jumapili ya mwisho wa Mwezi Mei, mwezi ambao pia ni kwa ajili ya heshima kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa.  Siku hii imekuwa ikiadhimishwa nchini Ufaransa kwa takribani miaka kumi na mitano sasa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.