2015-05-29 15:17:00

Uinjilishaji mpya ni mchakato wa kutambua upendo wa huruma ya Mungu!


Kuna uhusiano mkubwa kati ya Uinjilishaji na Katekesi; tema ambayo imeongoza mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya, ambalo limepewa dhamana na Baba Mtakatifu Francisko kuhakikisha kwamba, linasimamia maandalizi na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; ili kweli zawadi ya huruma ya Mungu iweze kutangazwa na kushuhudiwa katika maisha na utume wa Kanisa, wakati huu ulimwengu unaposhuhudia mabadiliko makubwa.

Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 29 Mei 2015 wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya. Anasema, Kanisa halina budi kuendelea kusoma alama za nyakati, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa watu wa nyakazi hizi, kwa kuonesha mabadiliko katika lugha inayotumika, jambo ambalo linapaswa kutekelezwa kwa hekima na busara.

Hii ni changamoto ya kumwilisha tunu msingi za Kiinjili kwa watu wa nyakati hizi, kwa njia ya hija ya maisha ya imani inayowaunganisha wote. Kuna watu katika tabaka na mazingira mbali mbali wanaosubiri kuona nguvu ya Injili inayookoa na kuwaonjesha mshikamano wa upendo; Injili inayomwilisha upendo wa Mungu unaowashirikisha maisha ya Kristo. Uinjilishaji mpya ni mchakato wa kutambua upendo wa huruma ya Mungu, ili waamini waweze kuwa kweli ni vyombo vya wokovu kwa ndugu zao.

Mbegu hii ya utambuzi anasema Baba Mtakatifu Francisko imepandikizwa mioyoni mwa waamini tangu siku ile walipobatizwa, inapaswa kukua na kukomaa katika baraka ili iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa kujikita katika katekesi makini inayowawezesha waamini kukuza maisha yao, ili hatimaye, kuonja huruma ya Mungu inayojionesha katika udhaifu wa maisha ya binadamu. Kanisa linasali daima kuomba huruma na msaada wa Mungu unaopaswa kuwasaidia kuwa kweli ni watu wenye huruma na mapendo kwa jirani zao.

Papa Francisko anasema kwamba, Roho Mtakatifu ndiye kiongozi mkuu wa mchakato wa Uinjilishaji ndani ya Kanisa anayefungua na kufanya mabadiliko katika mioyo ya waamini, ili msamaha walioupata uweze kumwilishwa kama kielelezo cha upendo kwa jirani zao, dhamana na ushuhuda wenye mashiko. Urithishaji wa imani ni jambo muhimu ambalo linapaswa kutekelezwa kwa ujasiri, ugunduzi na maamuzi ambayo wakati mwingine yanapaswa kutekelezwa kwa kugundua njia mpya.

Katekesi ni sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji  unaowafundisha waamini jinsi ya kukutana na Yesu hai na anayetenda kazi katika Kanisa lake. Waamini wanapokutana na Yesu wanahamasishwa kumfahamu vyema zaidi na kumfuasa, ili waweze kuwa wafuasi wake amini. Hii ndiyo changamoto ya Uinjilishaji inayojikita katika Katekesi, inayowasaidia waamini kukutana na Yesu Kristo. Dhamana hii itekelezwe kwa umakini mkubwa na Jumuiya za waamini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.