2015-05-29 09:23:00

Baa la njaa duniani ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa vitendo


Wakati wa uzinduzi wa Onesho la chakula kimataifa,  Expo Milano 2015, Baba Mtakatifu Francisko alitoa ujumbe kwa njia ya video na kwamba, Vatican pamoja na mashirika mbali mbali ya misaada ya Kanisa Katoliki yanashiriki katika onesho hili kwa kuonesha umuhimu wa mapambano dhidi ya baa la njaa duniani na kwamba, kuna mamillioni ya watu ambao wana njaa na kiu ya haki, amani na upatanisho, ili kuwa na matumaini kwa siku za usoni. Kanisa linashiriki kikamilifu katika mchakato wa mapambano ya baa la njaa na umaskini duniani, kwani Kanisa ni mtaalam wa maisha ya mwanadamu.

Ustawi na maendeleo ya mwanadamu ni kati ya vipaumbele vya Mama Kanisa kwa kizazi baada ya kizazi. Huu ni mwelekeo wa maisha ya kiroho, unaopania kuwasaidia watu kujenga mahusiano mema zaidi na Muumba wao pamoja na kushirikiana na binadamu wengine katika mchakato wa ustawi na maendeleo ya wengi. Lishe na nishati ni tema mbili ambazo zinapewa kipaumbele cha pekee katika onesho la chakula la Expo Milano 2015, ndiyo maana hata Baraza la Kipapa la haki na amani hivi karibuni limechapisha vitabu vinavyopembua kwa kina na mapana: Ardhi na Chakula; Nishati, Haki na Amani.

Huu ni mchango uliotolewa na Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani wakati wa uzinduzi wa kitabu kinachozungumzia  Ardhi na Chakula kwenye Onesho la chakula kimataifa huko Milano, Alhamisi, tarehe 28 Mei 2015. Tukio hili limehudhuriwa na wadau mbali mbali kutoka katika sekta ya kilimo na chakula nchini Italia.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wakati wa ufunguzi wa Onesho la chakula kimataifa, alisikitika kusema kwamba, dunia ina uwezo wa kuzalisha chakula cha kutosha kwa watu wote, lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, bado kuna umati mkubwa wa watu wanaokabiliwa na baa la njaa duniani. Ni matumanini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itajitahidi  kupambana na kashfa ya baa la njaa duniani kwa watu kubadilisha tabia na mawazo yao kwa kujikita zaidi na zaidi katika mfumo wa uchumi endelevu na unaozingatia usawa; hekima, ujasiri, uwajibikaji, mshikamano na udugu.

Kardinali Turkson anasema, Jumuiya ya Kimataifa inajiandaa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 60 ya Tamko la Umoja wa Mataifa kuhusiana na ushirikiano wa kimataifa katika mchakato wa kutafuta suluhu za masuala ya kimataifa katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kiutu, kwa kuheshimu  haki msingi za binadamu na uhuru kwa wote. Mambo yote haya yanapaswa kuvaliwa njuga, ili kweli yaweze kutekelezwa, vinginevyo yatabaki kwenye makaratasi.

Kardinali Turkson anabainisha kwamba, Serikali, Mashirika ya Kimataifa, Jamii, Familia pamoja na watu binafsi wanadhamana na wajibu wa kuhakikisha kwamba, wanalivalia njuga suala la uhakika wa usalama wa chakula duniani; kwa kuona, kuamua na kutenda, kwani ukosefu wa uhakika wa chakula na lishe ni chanzo cha umaskini. Maandiko Matakatifu pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa ni dira na mwongozo unaoweza kutumiwa katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani. Viwanda na wazalishaji katika sekta ya kilimo wanapaswa kujikita katika kanuni maadili, kwa ajili ya mafao ya wengi, ili kweli amani na ustawi viweze kupatikana.

Kardinali Turkson anasema kwamba, Mwaka 2015 ni mwaka wenye matukio makuu kimataifa kwani huu ni mwaka ambao: Jumuiya ya Kimataifa inafikia mwisho wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia. Ni mwaka utakaowakutanisha viongozi wakuu wa Jumuiya ili kujiwekea mikakati ya kudhibiti athari za tabianchi; ni mwaka wa kimataifa kwa ajili ya ardhi; tayari kuangalia mbele kwa matumaini zaidi.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha Wakristo na watu wote wenye mapenzi mema kwamba,  utunzaji bora wa mazingira na mapambano dhidi ya baa la njaa ni mambo ambayo wanapaswa kuyavalia njuga pasi na mzaha. Baraza la Kipapa la haki na amani kwa upande wake linaendeleza mchakato wa majadiliano kwa mwanga wa Injili na Kanuni maadili katika mapambano dhidi ya baa la njaa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.