2015-05-28 15:50:00

Wakristo msiwe kikwazo cha watu kutaka kukutana na kuonana na Yesu Kristo


Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, Siku ya Alhamisi, tarehe 28 Mei 2015 anasema kwamba, Wakristo ambao wamemezwa mno na malimwengu, watu ambao wanatafuta masilahi yao binafsi na wapenda sheria lakini wanafiki, ni kikwazo kikubwa cha watu kukutana na Yesu katika hija ya maisha yao.

Injili ya siku inamwonesha Bartimayo, mwombaji kipofu liyelazimika kupiga kelele ili Yesu aweze kumponya kutoka katika upofu wake, kwani wafuasi wa Yesu walikuwa wamemwambia kukaa kimya. Hii inaonesha kwamba, kuna baadhi ya Wakristo ambao wanaojitaabisha kujenga na kuimarisha uhusiano wao na Yesu na kundi la pili ni la Wakristo ambao wamejifungia ndani mwao, na wala hawataki kusikia kilio cha watu wengine wanaotaka kukutana na kuonana na Yesu.

Kundi la tatu anasema Baba Mtakatifu ni la Wakristo ambao, hawasikii na wala hawaguswi na watu wanotafuta wokovu, kwani watu wanaojikita katika ubinafsi kwa kujitafuta wenyewe, kiasi hata cha kushindwa kusikia sauti ya Yesu. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kuna kundi jingine ambalo linasikia kilio cha watu, lakini linataka kuwanyamazisha, kama ilivyotokea kwa mitume kuwakataza watoto kukutana na Yesu, wakadhani kwamba, Yesu alikuwa ni kwa ajili yao peke yao. Kuna watu wanaoendelea kupaaza sauti wakitaka imani na wokovu.

Wakristo wanaolitumia Kanisa kwa ajili ya mafao yao binafsi, ni kikwazo cha kutaka kukutana na kuonana na Yesu, kwani hawana ushuhuda wenye mashiko na mvuto. Ni Wakristo wa majina, lakini wamemezwa na malimwengu na kwamba ni wanafiki. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru Wakristo ambao kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, wamekuwa kweli ni chachu na mlango wa watu wengine kukutana na kuonana na Yesu kwa njia ya Kanisa lake. Hawa ni watu wanaowasaidia jirani zao: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anawataka waamini kuchunguza dhamiri zao na kuona wanaangukia katika kundi gani, tayari kujirekebisha, ili kusikiliza kilio cha watu wanaotaka kuonana na kukutana na Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.