2015-05-28 15:29:00

Muswada wa Katiba mpya, unawakanganya watu! Hakieleweki kitu!


Kuna Taifa moja Afrika baada ya kupata uhuru wa bendera, mhasisi wa Taifa hilo akawataka raia wake wajisikie kuwa jamaa moja kadiri ya falsafa ya mwafrika, na waitane “Ndugu.” Yeye mwenyewe ingawaje alikuwa msomi wa hali ya juu akawa mtu wa kawaida na kuvaa nguo za kawaida. Hakutaka kujimbikizia mali wala kutawala nchi kimabavu. Akaitwa “Ndugu Rais” na kwenye mikutano ya Chama cha siasa akawa anaitwa “Ndugu mwenyekiti.”  Wakati wake ingawa wananchi walikuwa maskini, lakini walipendana kama ndugu na jamaa moja bila kubaguana kiukwasi, kiimani au kikabila.

Falsafa hii pekee ya kiafrika ilishabikiwa na kupendwa ndani na nje ya nchi, kwani huo ulikuwa utamaduni wa kujivunia Mwafrika. Watawala waliofuata baada ya kifo cha “Ndugu Rais na Ndugu mwenyekiti” wakaonja utamu wa mali na wa madaraka, wakajisikia uhuru wa manyani ndani ya shamba la mahindi lisilo na mlinzi. Tofauti za maisha zikaonekana bayana. Jina “Ndugu” likabezwa na likafa kifo cha kawaida kama alivyofariki mhasisi wake. Watawala wa nchi hiyo wakaanza kuitwa “Mheshimiwa Waziri,” “Mheshimiwa Mbunge” “Mheshimiwa Rais,” nk. Punde si punde hata cheo cha “Mheshimiwa” nacho kikaja kupoteza hadhi kwani kilitumika na kila mtu. Kwa hiyo ili kujitofautisha zaidi na watu wengine viongozi wakaamua kuiga tamaduni za nchi za nje za kuitana kadiri ya madigrii ya kisomi kama vile Daktari au Professa, na kuvaa suti na tai ili kuwapugaza wananchi. Wakawa wanaitwa “Dakta Nanhii…,” au “Profesa Nanhii…” Rais wake pia anaitwa Dakta Nanhii….

 

Sasa hivi ukiipiga darubini nchi hiyo baada ya kulitupa jina hilo “Ndugu” utaangua kicheko cha masikitiko, kwani unawaona wananchi wake kama vile “wameachwa kwenye mataa.” Kwa hoja kwamba hawaelewi kinachoendelea hasa wanapowaona viongozi wao wote ni wasomi wakuu kwa kiwango cha udaktari lakini kuna wagonjwa wengi wanakufa na madaktari wenyewe wanamiminika kwenda kutibiwa nchi za nje, na wengi wao wanagongana nao kwa babu wa Roliondo. Aidha wanashangaa wanaposikia nchi imejaa maprofesa, lakini elimu inalalamikiwa kuwa imeshuka na waomba yala maskini wamejaa kibao.

 

Hali hiyo ya kupenda vyeo imekithiri pia ndani ya kanisa. Toka mkuu wa jumuia ndogondogo, mwenyekiti wa kigango hadi wa Parokia, kiongozi wa kwaya, katekista hadi mpiga kinanda wanataka kuonekana tofauti. Mapadre wanaitwa Reverend, na wengine wanataka pia kuitwa Dakta au Professa. Askofu anaitwa Your Excellency au Mhashamu, Monsinyori au Doctor of Divinity. Kardinali anaitwa Your Eminence au Mwadhama (kwa kiarabu maana yake mfalme).

 

Leo tutamsikia Mfalme wa Wafalme, na Kuhani mkuu wa makuhani, anawaita “Ndugu” watu walio chini yake tena wanafunzi wake. Mkuu huyo ni Yesu Kristu. Anatuita ndugu na anatupatia kila mmoja bila kutofautisha Katiba mpya ya kuishi kindugu.

 

Jina hilo “Ndugu” liliibuka siku ya jumapili ya ufufuko wake, pale alipowatokea wanawake na kuwaambia: “Msiogope; enendeni, mkawaambie “Ndugu zangu” waende Galilaya, ndiko watakakoniona.” Haitoshi, kuna pia sehemu nyingine Yesu anapotafutwa na mama yake na ndugu zake akawajibu wale waliotumwa kumwita: “Mama yangu na ndugu zangu ni akina nani?” Akawatazama wale walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, “Tazama, hawa ndiyo mama yangu na ndugu zangu!” (Mk. 3:33-35). Kulikoni Yesu anawaita wafuasi wake kuwa ndugu zake ingawaje hawakuwa wa ukoo mmoja. Aidha hata maisha yao yaonekana hayakuwa ya ukamilifu, kwani hata wanafunzi nao walitegemea watakuwa watu wa maana na kuitwa wakuu na kutofautiana na wengine.  

 

Hivi kwa vyovyote hata wao hawakulitaka jina hilo “Ndugu.” Tunasikia kwamba karibu wote walimtoroka yalipompata matatizo. Halafu toka mwanzo walikuwa mitume kumi na wawili baadaye wakabaki kumi na moja tu. Yaonekana mwanafunzi mmoja aliyekuwa pamoja nao kwa miaka ile mitatu aliamua kuachana na sera za Katiba mpya ya Yesu. Isitoshe akaamua hata kumsaliti kwa wakuu wa serikali na dini, yaani Mafarisayo na Makuhani wakuu, na Majalimu kwani hakutaka kupokea mswada wa Katiba iliyopendekezwa na Yesu. Yaonekana huyu mwenzetu yalimponza mali na ukuu.

 

Petro yeye pia ulimponza ukuu hata  akamkana Yesu mara tatu.  Kadhalika mitume hawa kumi na mmoja waliobaki, hawakuwa hodari licha ya kuishi na Yesu kwa miaka mitatu na sasa wanamwona kwa macho yao pale mlimani, lakini wanamwonea mashaka kama ilivyoandikwa: “Walipomwona wengine walimwabudu lakini waliona wasiwasi” (Mt. 28:17). Kwa nguvu za Roho ya Yesu tu ndiyo wakaimarishwa na kujisikia tena ndugu.

 

Ili tufanikiwe kuwa tena watu wa jamaa moja na wa kusaidiana kindugu na kwa haki na upendo, hatuna budi kumsikiliza Yesu anayetuagiza kwenda mlimani anakowaagiza kwenda mitume wake. Hebu fuatana na wanafunzi hao ili kupata uhondo. Imeandikwa: “Nao wanafunzi wakaenda mpaka mlima ule aliowaagiza Yesu.” Sikiliza kwa makini, imesemwa kwamba hao mitume walikutana juu ya mlima aliowaagiza Yesu na siyo kila aina ya mlima, bali mlima ule alioagiza, ambao Yesu mwenyewe aliwahi kuupanda na huko akalifanya tendo fulani la pekee tunalotakiwa kuliiga sisi.

 

Mosi, yabidi kwenda mlimani alikotunga Katiba Mpya: Mwenyewe alisema: “Amri mpya nawapeni.” Kwa hiyo ukitaka kupata mang’amuzi ya Katiba Mpya ya Yesu, huna budi kukwea katika mlima ule ambao Yesu alimwaga sera zake kama alivyofanya Mungu mwenyewe juu ya mlima Sinai alipozitoa amri kumi kwa Musa. Ukipanda mlima huo utayaona mambo kwa jicho la Mungu, yaani utaona heri nane za Kristu na kupata mang’amuzi ya mfufuka na utakuwa ndugu wa watu wote. Ukibaki bondeni mwa mlima huwezi kuelewa mawazo ya Mungu, na utaona mambo kwa jicho la ulimwengu wa uyakinifu.

 

Pili yabidi kupanda mlimani alikobadilika sura: Mara moja Yesu alipanda mlimani na huko akabadilika, akang’ara sura na mavazi yake yakawa meupe. Maana yake juu ya mlima kuna mabadiliko (metamorfosi). Asiyepanda mlimani, na kushuhudia mabadiliko ya kung’aa sura pamoja na mavazi yake, hawezi kumwona Yesu mfufuka. Kwa hiyo huwezi kuwa na mabadiliko au mageuzi yoyote yale katika maisha bila kupanda mlimani na kumshuhudia Yesu anavyobadilika. Yatubidi tubadilike, tumfuate Kristu mlimani ili tuweze kweli “kujivua magamba” na kubadilika.

 

Tatu inatakiwa kukwea mlima wa haki: Yesu alipanda mlimani alikoongeza mikate na kuwalisha lukuki ya watu wenye njaa. Yatubidi kuukwea mlima huo tunakoweza kumshuhudia Yesu akiwaonesha mitume wake jinsi Mungu anavyogawa raslimali za ulimwengu huu kwa haki na kwa upendo.

Tukiwa hapa duniani tuna njaa ya aina nyingi: njaa ya haki, ya elimu, ya amani, ya huruma, ya upendo nk. Yabidi tugawane raslimali za ulimwenguni kijamaa na kindugu kadiri ya mipango ya Mungu. Anayejikusanyia a kujilundikia mali za ulimwengu huu kibinafsi hawezi kumwona Yesu na hataweza kumpokea yeyote yule kama ndugu.

 

Tahadhari juu ya mlima wa kuabudiwa: “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake, akamwambia: “Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.” Ndipo Yesu alipomwambia, “Nenda zako, shetani” (Mt. 4:9). Huu ndiyo mlima pekee wa maangamizo, na anayetuongoza katika kupanda mlima huo ni ibilisi. Mlima huo tumeupanda wengi hasa wale tusiotaka kufuata sera za wahasisi wa nchi. Kwetu sisi wakristu tunaupanda kirahisi sana mlima huu kwa vile hatusikilizi maagizo ya Yesu ya kupanda mlima aliotuagiza.

 

Lakini Yesu ni ndugu yetu mwema, anamezea udhaifu wetu, kama alivyomezea udhaifu wa mitume wake kumi na mmoja aliowakuta mlimani, akawaita kuwa ni ndugu zake. Akawapa hata wosia ufuatao unaoongoza kwenye muungano wa upendo wa kindugu: Mosi, anawaambia: Enendeni ulimwengu kutangaza kwa watu wote Katiba mpya ya Mungu niliyowahubiria yaani, anawaagiza waende kwa watu na siyo watu waje kwao. Waende  na wafanye kama alivyofanya Yeye mwenyewe yaani, kupeleka ujumbe kwa watu wote kadiri ya utamaduni wanaoukuta huko.

ili, anawaambia: mkawafanye watu wote yaani mataifa yote kuwa wafuasi, maana yake wawe wasikilizaji na watekelezaji kwa vitendo. Wakifuata Katiba hiyo mpya kitaeleweka.Tatu, akawaagiza: mkawabatize, yaani wakawazamishe watu katika upendo wa kindugu na siyo kuwatia tu maji kichwani. Anaagiza “Mkawabatize Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu” yaani wamwingize mtu katika maisha ya undugu wa Utatu mtakatifu. Hivi ndivyo kazi ya jumuia ya kikristu, kujiingiza kidhati katika maisha ya upendo wa Utatu Mtakatifu. Nne, akaagiza tena: mkawafundishe kutimiza kile nilichowaagiza na kuwafundisha, yaani kwenda kupelekea Katiba mpya kwa watu wote.

Maneno ya mwisho ya wosia yanavunja rekodi na kupita sera na katiba za wahasisi wote pale Yesu anaposema: “Mimi niko nanyi hadi mwisho wa dahari.” Yaani katika msafara wa kuzinadisha sera za Katiba mpya Yesu mwenyewe yuko mstari wa mbele badala ya kutuachia wababaishaji. Hii ndiyo ahadi ya mfufuka kuonesha kwamba hajafa, bali yuko nasi daima akitutia tafu kama ndugu zake. Ama kweli Yesu ni Emmanuel “Mungu pamoja nasi.” Wewe ndiye rafiki wa kweli hata wakati wa dhiki zetu. Wewe ni ndugu halisi hata tunapokukana na kukusaliti. Ndugu zangu Heri kwa Sikukuu ya Utatu Mtakatifu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.