2015-05-28 15:58:00

Kushabikia ndoa za watu wa jinsia moja ni dalili za kukengeuka kwa walimwengu


Ulimwengu umepigwa butwaa na kushangazwa na matokeo ya kura ya maoni nchini Ireland yaliyowapatia ushindi wananchi wanaotetea ndoa za watu wa jinsia moja. Hapa kuna mambo mengi yanayopaswa kufanyiwa tafakari ya kina, kwani hii ni changamoto kubwa na endelevu kwa Kanisa linalotaka kusimama kidete: kushuhudia na kutangaza Injili ya Familia kwa watu wa Mataifa. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano na vyombo vya habari anasema kwamba, kura hii ya maoni ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu, hali inayoonesha kukengeuka kwa binadamu na utu wema.

Wachunguzi wa mambo wanasema, idadi kubwa ya vijana wameshiriki katika kupiga kura ya maoni na matokeo yake na mapinduzi makubwa katika sera na mikakati ya maisha na kitamaduni nchini Ireland. Askofu mkuu Diarmuid Martin wa Jimbo kuu la Dublin, Ireland anasema Kanisa linapaswa kufanya tafakari ya kina ili kuangalia ni wapi ambapo limekosea, tayari kusimama tena na kuendelea na mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa kujikita katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko. Vijana walioshiriki katika kura ya maoni, wengi wao ni wale ambao wamesoma katika shule zinazosimamiwa na kuongozwa na Kanisa.

Hapa anasema Askofu mkuu Martin, matokeo ya kura hii ya maoni ni kuibuka kwa ubinafsi na ukakasi dhidi ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kiasi kwamba, ndoa tena haionekani kuwa ni kielelezo cha mshikamano na upendo wa dhati. Haki binafsi zinapewa kipaumbele cha kwanza na kusahau kanuni maadili, utu na heshima ya binadamu. Hata wanasiasa wenyewe wameshindwa kuonesha ushuhuda kwa kupinga hadharani ndoa za watu wa jinsia moja kutokana na kuogopa kupoteza masilahi yao kisiasa.

Kwa upande wake, Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anabainisha kwamba, hapa kuna haja ya kuendeleza majadiliano ya kina, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima ya binadamu na mafao ya wengi kama kanuni msingi katika kuendeleza mchakato wa kutangaza na kushuhudia Injili ya Familia. Haki binafsi zikipewa kipaumbele cha kwanza na kubeza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, hapo kuna hatari kubwa.

Ndoa za watu wa jinsia moja haziwezi kuwa sawa na ndoa kadiri ya mpango wa Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya binadamu. Watoto wanahitaji uwepo wa baba na mama katika malezi na makuzi yao na kwamba, dhamana hii haina mbadala. Katika wimbi la mwelekeo wa ndoa za watu wa jinsia moja kama sehemu ya haki msingi za binadamu kama wanavyodai baadhi ya watu, Jamii kwa sasa inaelekea wapi?

Wachunguzi wa mambo wanasema, ushindwa wa kura ya maoni kwa ajili ya ndoa za watu wa jinsia moja umechangiwa kwa namna moja au nyingine na kashfa ambazo kwa miaka ya hivi karibuni zimeliandama Kanisa nchini Ireland, ndiyo maana kuna haja ya kusimama kidete katika mchakato wa Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu, vinginevyo walimwengu wataendelea kukengeuka na kanuni maadili na utu wema kuwekwa daima rehani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.