2015-05-27 10:48:00

Uchumi hauna budi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na mafao ya wengi


Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro hivi karibuni, umefanya mkutano wa kimataifa wa siku mbili uliokuwa unajadili umuhimu wa kufikiria tena masuala ya kiuchumi na maisha ya kijamii mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Lengo ni kuwajengea wanachama wa Mfuko huu kuendeleza mchakato wa majadiliano na waamini wa dini mbali mbali ili kutambua mambo msingi yanayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na mafao ya wengi.

Ni changamoto ambayo imetolewa na Bwana Massimo Gattamelata, Katibu mkuu wa Mfuko wa “Centesimus Annus”. Anaendelea kusema kwamba, Kanisa linapenda kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kujadiliana ili kuweza kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Muhtasari a Mafundisho Jamii ya Kanisa ni mwongozo ambao pia unaweza kutumiwa na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbali mbali ya Kikristo, mwaliko ambao pia unatolewa kwa waamini wa dini mbali mbali kwani lengo kumhudumia mwanadamu na kutafuta mafao ya wengi.

Hii ni changamoto ambayo inaonesha uwepo endelevu wa Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ni hazina ya mambo ya kale na  mambo mapya ambayo Kanisa linapenda kuwashirikisha waamini wa dini na madhehebu mbali mbali ya Kikristo. Majadiliano ya kidini na kiekumene yanaonesha umuhimu wa kuunganisha nguvu ili kukuza haki, amani, udugu na maendeleo endelevu ya binadamu.

Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika hotuba yake kwa wajumbe wa mkutano huu amekazia umuhimu wa Kanisa kuendeleza urithi  mkubwa ambao Mtakatifu Yohane Paulo II amewakabidhi wanachama wa Mfuko huu, ili kueneza Mafundisho Jamii ya Kanisa, dhamana ambayo walipewa kunako mwaka 1993. Lengo ni kuendeleza mchakato wa majadiliano na wataalam pamoja na kada ya wasomi kuhusiana na masuala ya kiuchumi, ili kupata muundo wa uchumi unaojikita katika maendeleo endelevu na ustawi wa binadamu.

Kardinali Parolin anabainisha kwamba, kiini cha majadiliano haya ni utu wa binadamu,  mafao ya wengi na kanuni maadili; mambo ambayo Jamii nyingi katika ulimwengu wa utandawazi wanataka kuyaangalia kwa “jicho la kengeza” pasi na kuyapatia uzito wa kutosha ingawa yana athari kubwa katika maisha ya Familia ya binadamu. Kanuni hizi ziwasaidie wengi kusimama kidete kwa ajili ya mafao ya wengi.

Kardinali Parolin amelishukuru jopo la majaji lililosimamia mchakato wa utoaji wa tuzo kwa washindi wa Mfuko wa “Centesimus Annus” kwa mwaka huu, kwa kuangalia mchango wa Kanisa katika masuala ya fedha na uchumi, ili kutoa kipaumbele cha pekee katika mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu. Mambo haya yasipotiliwa mkazo matokeo yake ni kudhalilisha heshima ya binadamu na kuanza kuabudu miungu ya uongo ambayo ni fedha na madaraka. Lakini fedha anasema Baba Mtakatifu Francisko inapaswa kuwa ni chombo cha huduma kwa binadamu, kwani utandawazi usiojali uwepo wa Mungu una mwelekeo pia wa kutothamini kanuni maadili na utu wema. Ikumbukwe kwamba, kila maamuzi ya kiuchumi yanayofanywa, yanafumbata matokeo ya kimaadili. Uchumi hauna budi kuzingatia ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili kama anavyokazia Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa kichungaji, Maendeleo ya Watu, Populorum Progressio.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.